Wanasiasa wakongwe nchini, Christopher Mtikila na John Lifa- Chipaka wametupwa nje ya kinyang’anyiro cha kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na kushindwa kutimiza vigezo vya kisheria.
Mchungaji
Mtikila anawakilisha Chama cha Democratic Party (DP) na Chipaka
anawakilisha Tanzania Democratic Alliance (TADEA). Vyama vyote hivyo
vilianzishwa mara tu Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa, Na. 11 ya
1992, ilipopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kupitia
sheria hiyo, ndiyo ilitolewa ruhusa ya kisheria ya kuanzishwa kwa mfumo
wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania. Kabla ya sheria hiyo, masuala
ya siasa yalikuwa si katika mambo ya Muungano.
Pigo
la kukosa kuteuliwa kugombea urais, pia lilimpata Dk. Godfrey Malisa
Kahangwa aliyewakilisha Chama cha Kijamii (CCK), chama kilichoanzishwa
miaka michache iliyopita, baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.
Akitangaza
matokeo ya maombi ya vyama hivyo vitatu jioni hii, Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema ombi la
Mchungaji Mtikila limekataliwa kwa sababu ameshindwa kuwasilisha tamko
la kiapo la Mahakama Kuu, ingawa yeye aliapa lakini mgombea mwenza wake
ambaye hakutajwa jina, hakufika na hakuna kiapo chake.
Jaji
Lubuva ambaye alifikia ngazi ya jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania,
amesema Dk. Kahangwa hakutimiza idadi ya watu wanaotakiwa katika
udhamini na amekosa mgombea mwenza kutoka upande wa Zanzibar.
Kwa
Lifa-Chipaka, ilielezwa kwamba hakutimiza vigezo kwa vile alishindwa
kuwasilisha orodha ya wadhamini kutoka Zanzibar. kisheria walitakiwa
watu 200 wenye kadi za kupigia kura.
Wakati
Chipaka amekosa wadhamini Zanzibar, upande huohuo chama hicho
kimesimamisha mgombea urais, ambaye ni Juma Ali Khatibu, Naibu Katibu
Mkuu.
Mchungaji
Mtikila alilalamika mara tu alipotangaziwa uamuzi na Jaji Lubuva,
kwamba alicheleweshwa kwa utaratibu tu wa ofisi ya Tume kwani alifika
mapema na kuripoti ofisini kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kwemboy.
Mtikila
alidai kuwa hakufika na mgombea mwenza wake kwa wakati kwa kuwa amepata
tatizo la kuumiwa mkewe na kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi na
kuamua kuahirisha safari.
“Tulijitahidi
hata kumtumia tiketi ya ndege lakini hakuwahi hapa. Hili tatizo ni la
asili ambalo mtu analifahamu linaweza kutokea wakati wowote. Lakini mimi
nimewahi hapa na jaji alinikubalia kuapa na kushauri nije kukujulisha
kuwa mkinipa muda kusubiri kidogo nitakamilisha na kurudia kwake niape
na mgombea mwenza akiwa amewasili,” alisema Mtikila katika kilio ambacho
hakikuzingatiwa na Tume.
Jaji
Lubuva alisema kwa wote walioshindwa kutimiza masharti, maana yake
wamekosa kuteuliwa kwa mujibu wa sheria kwa kuwa kwa utaratibu
ulioandaliwa, hakuna muda wa kuwasubiri kukamilisha taratibu.
Vyama
vilivyofuzu kuteuliwa wagombea wao ni pamoja na Chadema, Edward Lowassa
(mgombea mwenza Juma Duni Haji) wanaowakilisha Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA); ACT-Wazalendo Anna Mghwira na mgombea mwenza Hamad
Mussa Yussuf na Dk. John Magufuli (na mgombea mwenza Samia Suluhu
Hassan) wa CCM.
Kampeni za urais zinaanza rasmi kesho.
No comments:
Post a Comment