MAELFU ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, jana walijitokeza kwa
wingi katika siku ya kwanza ya uandikishaji wapigakura katika mfumo wa
kisasa wa kielektroniki (BVR), licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa.
Katika vituo vingi, licha ya wananchi kujitokeza kuanzia mapema
alfajiri, changamoto kadhaa zilijitokeza, ikiwemo mashine kushindwa
kufanya kazi kutokana na hitilafu, hivyo kuchelewesha uandikishaji,
ingawa baadaye ufumbuzi ulipatikana.
Wachangishana pesa
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Tabata Kisukuru, Manispaa ya Ilala,
licha ya kituo kuwa na mashine mbili, zote zilishindwa kuwaka kutokana
na kutokuwa na umeme huku kifaa cha umemejua kikielezwa kuwa na
hitilafu.
Kutokana na hali hiyo, wananchi walihamasishana kuchanga Sh 100 kila
mmoja ili kupata Sh 30,000 za kulipia umeme uliokuwa umeombwa na
watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoka nyumba ya jirani.
Baada ya mjadala, baadhi ya wananchi hao waliofikia 800 waligoma
kulipa wakidai Serikali ilishatenga fedha za uandikishaji wapigakura.
Hali hiyo ilisababisha kuchelewa zaidi kwa kazi ya kuandikisha
wapigakura.
Pamoja na kuchelewa huko, baadhi ya wananchi hawakukata tamaa, mpaka
alipokuja ofisa mwingine wa tume aliyetengeneza vifaa vya umeme jua na
ndipo uandikishaji ukaanza majira ya saa saba.
Wachezeana rafu
Wakati wakisubiri kuandikishwa, baadhi ya wananchi walijikuta
wakitafuta mbinu ya kuwahi kuandikishwa, kwa kughushi namba zao,
mathalani, aliyekuwa kwenye nafasi ya 300 na kupewa namba 300, alifuta
sifuri moja ili isomeke 30.
Kuna waliofanikiwa, lakini wengine walikwama kutokana na kutumia wino
tofauti na ule ulioandikwa katika karatasi za awali na wahusika.
Pugu ‘ngoma’ yalala
Katika kituo cha Pugu Stesheni, wananchi wapatao 500 waliowahi katika kituo hicho kujiandikisha, walitakiwa kurudi nyumbani na kurejea leo kutokana na mashine kusumbua na kuwa itaandikisha watu 10.
Pugu ‘ngoma’ yalala
Katika kituo cha Pugu Stesheni, wananchi wapatao 500 waliowahi katika kituo hicho kujiandikisha, walitakiwa kurudi nyumbani na kurejea leo kutokana na mashine kusumbua na kuwa itaandikisha watu 10.
Kituo cha Mistuni A na B kulikuwa na misururu kutokana na kazi ya uandikishaji kutoanza kutokana na ubovu wa vifaa.
Mpaka mtandao huu unafika kwenye vituo hivyo viwili majira ya saa 6
mchana, hakuna mwananchi yeyote aliyeandikishwa kutokana na mashine ya
kituo cha Mistuni A kusumbua kamera huku Mistuni B mashine ya kuchapa
karatasi kukorofisha.
“Mpaka sasa bado hatujaanza kuandikisha, mashine moja kamera
inasumbua, na mashine nyingine inasumbua na ndio mafundi wanahangaika
kutengeneza. Muda wowote mashine zitakapotengamaa basi tutaanza
kuandikisha,” alisema ofisa wa tume ambaye alikataa kutaja jina lake.
Katika
kituo cha uandikishaji cha Majengo Vingunguti, mtandao huu ulishuhudia
umati wa watu wakizozana wakiwa kwenye mstari, hali ambayo
imechangiwa na kuchelewa kuanza kwa kazi hiyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa wa Majengo Vingunguti, Chande Msoke
alisema kumekuwapo na tatizo la kuchelewa kwa vifaa, jambo ambalo
limefanya kazi hiyo ianze kwa kuchelewa saa tatu, jambo ambalo
limesababisha mizozo ya hapa na pale.
“Watu wamefika hapa saa 11: 30 asubuhi, vifaa na ufungaji wa turubai
umechelewa jambo ambalo limesababisha vurugu za hapa na pale.
Tulichofanya tuliwaandikisha wale waliofika mapema na pale kazi ya
uandikishaji ilipoanza ndio walioanza kuhudumiwa.
Aliongeza: “Kutokana
na kuchelewa kuanza watu wamekuwa wakali kiasi ambacho hata akija mama
mjamzito, mzee au mlemavu wanakataa kumpisha, haya yote yanachangiwa na
kuchelewa jambo ambalo linafanya watu kukaa sana kituoni."
Kuhusu kasi ya kuandikisha, Msoke alisema imekuwa ikienda taratibu
kutokana na mashine kushindwa kutambua alama za vidole kwa baadhi ya
watu ambao inawachukua dakika 45 kukamilisha kazi hiyo.
“Wale ambao mashine inashindwa kutambua alama za vidole, tunawataka
wakanawe mikono na sabuni, na kama bado itakuwa shida, basi tunamtaka
arejee kesho,” alisema.
Katika kutuo cha Mchafukoge, Mnazi Mmoja, kazi ya uandikishaji
ilichelewa na ilianza saa 3 asubuhi kutokana na kuchelewa kufikishwa
vifaa huku kazi hiyo ikifanyika taratibu sana.
Katika kituo cha Majani ya Chai, Kipawa, shughuli ya uandikishaji
ilianza saa tatu asubuhi na baada ya kuhudumia watu watano mashine
ilikorofisha hivyo kufanya kazi hiyo kusimama kwa muda.
Ubungo yale yale
Wakati hayo yakitokea katika Manispaa ya Ilala, katika wilaya ya
Kinondoni nako uandikishaji ulianza kwa kusuasua, licha ya wananchi
kujitokeza kwa wingi. Ilielezwa uchelewaji huo ulitokana na mashine hizo
kuletwa juzi usiku na hivyo kazi ya ufungaji kuchelewa, ikielezwa kila
kituo kina mtaalamu mmoja wa teknolojia ya habari na mawasiliano (IT).
Katika kituo cha kujiandikisha cha shule ya msingi Ubungo Plaza,
Mwandishi Msaidizi wa kituo hicho, Charles Samson akiwa na wenzake
wawili, walionekana kukaa bila kufanya jambo lolote huku amezongwa na
watu na kusema mashine hizo zilipokelewa juzi usiku, hivyo hazijawekewa
software.
Alisema hatua hiyo inatokana na kuwa mtaalamu wa IT kutoka NEC kuwa
mmoja katika kata hiyo ya Ubungo, hivyo walimsubiri hadi alipokamilisha
kazi na uandikishaji kuanza baada ya saa nne.
Aidha, ilielezwa baadhi ya
watu waliokuwa na haraka za kuendelea na shughuli zao, walishindwa
kusubiri wakiahidi kurudi baada ya mambo kuwa sawa.
Nako Mbezi Beach katika eneo la Miti Mirefu mpaka kufikisha saa nne
asubuhi uandikishaji ulikuwa haujaanza kutokana na kuwa vifaa hivyo
vilikuwa havijafika, jambo lililofanya watu kuondoka katika vituo huku
wengine wakibaki na kupigwa na jua.
Huku eneo la kawe walichelewa kuanza uandikishaji licha ya vifaa
hivyo kuwa vimefika kutokana na kudaiwa kuwa umeme ni mdogo hivyo
mashine hizo hazikuweza kufanya kazi mpaka kufikia saa nne asubuhi.
Temeke nao wachelewa
Kama ilivyokuwa Ilala na Kinondoni, wakazi wa Temeke nao walijitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali vya uandikishaji, huku changamoto ikiwa vifaa, ingawa baadaye ilipatiwa ufumbuzi.
Kama ilivyokuwa Ilala na Kinondoni, wakazi wa Temeke nao walijitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali vya uandikishaji, huku changamoto ikiwa vifaa, ingawa baadaye ilipatiwa ufumbuzi.
Katika kituo cha Mtaa wa Mwembebamia kata ya Chamazi, baadhi ya watu
wananchi waliojitokeza kujiandikisha walililamikia ucheleweshwaji
uliofanywa na waandikishaji hao kwani hadi kufikia saa 3 asubuhi
uandikishaji ulikuwa bado haujaanza.
Wakizungumza na mtandao huu, walidai kuwa walifika mapema katika
kituo hicho kwa matarajio kuwa waandikishaji hao wangefuata ratiba na
kuanza saa 2 ili waweze kuwahi katika shughuli zao zingine.
Ramadhani Issa, mkazi wa Mwembebamia B, alidai licha ya utaratibu wa
kutoa namba kwa kila mwananchi anayefika kuwa mzuri, lakini utaratibu
huo una dosari kubwa kwani baadhi ya watu walifika mapema lakini
walipewa namba za mwishoni tofauti na waliochelewa, suala linaloonekana
kuwa ni kama kuna upendeleo.
Katika Kata ya Maganga iliyopo Temeke watu waliojitokeza na
walilalamikia waandikishaji kwenda taratibu kutokana na mashine
kuchelewa kufanya kazi, huku mtu mmoja akilazimika kutumia hadi dakika
20 ili kupiga picha. Kwa upande wa kata ya Azimio, watu wengi pia
walijitokeza huku changamoto ya kuchelewa kufika kwa wahusika na mashine
kuwa chache.
Wanung’unikia mashine
Wananchi wa Kata ya Mzinga Manispaa ya Ilala, wamelalamikia usumbufu
walioupata kwa mashine za uandikishaji kugoma kufanya kazi kutokana na
tatizo la mtandao, jambo lililosababisha uandikishaji kuanza saa tano
asubuhi kwa kutumia mashine moja.
Akizungumza na mtandao huu jana, mkazi wa kata hiyo, Saidi Ndembo
alisema wananchi wa kata hiyo walipata usumbufu mkubwa kwasababu
walifika kituoni hapo kujiandikisha alfajiri, lakini mashine hazikuwa
zikifanya kazi.
Alisema kutokana na mashine kusumbua na kulazimika kutumia mashine
moja badala ya mbili zilizokuwepo kituoni hapo, wananchi walitangaziwa
kuondoka kituoni na kubaki watu 150 ambao wataandikishwa na wakati huo
kituo kilikuwa na watu zaidi ya 500 kitendo ambacho kilizua mzozo.
No comments:
Post a Comment