MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe
amesema pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika Ukawa, lakini
wanajitahidi kumpata mgombea mmoja.
Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho
uliofanyika jijini Mwanza, ambapo pia aliwatambulisha wabunge waliohamia
Chadema kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge wa Kahama, James
Lembeli na mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mara, Ester Bulaya.
Mbowe alisema viongozi wanaounda Ukawa, wanaendelea kushirikiana
ingawa kuna changamoto kadhaa. Lakini, watatumia kila mbinu kuhakikisha
anapatikana mgombea mmoja kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Ukawa
katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
“Tunaendelea kushirikiana lakini kuna changamoto, kama viongozi
tutatumia kila mbinu tuwe na mgombea mmoja wa Ukawa na mazungumzo yoyote
yanahitaji uvumilivu, kuheshimiana na kushirikiana,” alisema Mbowe
ambaye ni mbunge wa Hai.
Hata hivyo, Mbowe alisema umoja huo hautatangaza mgombea wao kwa
haraka, kama ambavyo wananchi wanatarajia, kwa sababu tu CCM wamekwisha
kumtangaza wao, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
“Tutamtangaza mgombea wetu kwa muda muafaka na watanzania wote
watafurahi…hatuwezi kutangaza kwa sababu tu CCM wametangaza mgombea
wao,” alisema Mbowe.
No comments:
Post a Comment