Dar es Salaam. Kiongozi mkuu wa chama chama
cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe jana alianika orodha ya majina ya watu
wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti zenye mabilioni ya fedha nje ya nchi,
lakini akasita kuyataja kutokana na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke,
Dar es Salaam, Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje
nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.”|
Alisema
Zitto alisema wamejaribu kuishinikiza Serikali ichukue hatua, lakini
inaonekana kutotaka kufanya hivyo na kwamba anaamini waandishi wa habari
kwa kutumia taaluma yao wataweza kuwaanika wahusika.
Wakati
maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina hayo, wananchi walionekana
kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi hiyo yenye majina 99 ya
wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya nchi, lakini kiongozi huyo
hakuwa tayari kuwapatia na badala yake akiwaambia wasome magazeti ya
kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya
raia hao wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki
kihalali lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua
leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa
ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa
habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia nakala yenye majina 99 ya
Watanzania au watu wenye uhusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya
Uswisi. Jumla ya akiba katika akaunti benki hii pekee ni Dola 114
milioni za Marekani,’’ alisema.
Wakati huohuo, Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ametawazwa kuwa chifu wa mkoa na wazee
wa Dar es Salaam na kuitaka serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi
chenji zinazotokana na ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond. Akizungumza
katika kongamano hilo la wazee la kutafakari uchaguzi wa mwaka 2015, Dk
Slaa alisema ingawa wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere
kupambana na maadui wa tatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini
kwa sasa ameongezeka adui wa nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga
alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka? Lakini ujinga, umaskini na
maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni ufisadi,” alisema.
Alisema
hakuna Mtanzania ambaye atakwenda dukani na Sh10,000 kununua chumvi na
kibiriti halafu akaacha chenji yake dukani kwa makusudi na hivyo
Watanzania bado wanadai fedha zao zilizopotea kutokana na ufisadi.
Kadhalika
Dk Slaa alisema kitendo cha wazee hao kukutana katika kongamano hilo
kinaashiria kuwa wana kiu, njaa na matumaini ya kutaka mabadiliko.
“Mwalimu
pia alipokewa na wazee wa Bagamoyo ambao walimuombea dua, akaenda
kwenye makaburi na waliunganisha nguvu kumng’oa Mwingereza na kupata
uhuru na mimi nawataka wazee wa Dar es Salaam kuongeza nguvu kuing’oa
CCM,” alisema Dk Slaa.
Alizungumzia pia uandikishaji wa
Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam
kuwa makini na kuhakikisha wanajiandikisha.
Awali,
katika kongamano hilo, Naibu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na
Shura za Maimamu nchini Sheikh Rajab Katimba aliizungumzia kauli ya
Katibu wa Itikadi na Uenezi, wa CCM Nape Nnauye ya kuwa CCM itashinda
kwenye Uchaguzi Mkuu ujao hata kwa bao la mkono na kusema ni ya
kichochezi.
“Wakati nchi inajitahidi kuwa na amani na
kuwa na uchaguzi wa haki na huru, kiongozi wa chama anazungumza
uchochezi mkubwa ambao kama viongozi wengine wangeusema sidhani kama
wangekuwa salama,” alisema.
Sheikh Katimba aliwaasa
Ukawa kuwa na umoja na kuwataka wawaite wazee ili wawape ushauri badala
ya kulumbana kwani huu si wakati mwafaka wa kuwa na migogoro.
No comments:
Post a Comment