Vikwazo vipya safari ya matumaini - LEKULE

Breaking

31 Jul 2015

Vikwazo vipya safari ya matumaini

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa pili kushoto) akimkabidhi Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa fomu za kugombea urais kupitia chama hicho jana kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Regina ambaye ni mke wa Lowassa, na kulia ni Naibu Katibu MKuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Dar es Salaam.
Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alichukua fomu za kuomba ridhaa ya Chadema kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano, lakini anakabiliana na vikwazo vinne kabla hajafanikiwa kuongoza upinzani kutwaa madaraka kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.

Lowassa, mbunge wa Monduli na mwanasiasa aliyekulia ndani ya CCM, aliweka rekodi ya kuwa Waziri Mkuu wa Kwanza kukihama chama tawala alipotangaza kuhamia Chadema Jumanne wiki hii, akieleza kutoafikiana na mchakato wa kupata mgombea urais ndani ya CCM na sasa anataka kuwa kiongozi wa pili aliyeshika nafasi hiyo kuingia Ikulu baada ya Mwalimu Julius Nyerere.

Uamuzi wake wa kugombea urais kwa nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, unafanya upinzani kuwa na nguvu ya ziada kulinganisha na chaguzi zilizopita, kukabiliana na mgombea wa CCM, Dk John Magufuli na hivyo kuweka mazingira ya uwezekano wa kuchezeana rafu za kisheria.

Hadi sasa haijaelezwa sababu za kuenguliwa kwa Lowassa na makada wengine ndani ya CCM katika mbio za urais.

Hofu ya Lowassa kuwekewa pingamizi na vikwazo vingine vinavyoweza kumkabili, vimelifanya gazeti la Mwananchi kuongea na wadau mbalimbali kuhusu changamoto ambazo mbunge huyo wa Monduri anaweza kukabiliana nazo katika “safari ya matumaini” aliyoianzia CCM.

Tuhuma
Moja ya vikwazo vikubwa ambavyo Lowassa atakabiliana navyo ni tuhuma za ufisadi, na hasa sakata la mkataba wa ufuaji umeme wa dharura baina ya Serikali na kampuni ya Richmond DRC, ambalo lilimfanya awe Waziri Mkuu wa kwanza nchini kuwajibika kisiasa kutokana na kashfa.
Kabla ya kuhama CCM, viongozi wa Ukawa wamekuwa wakiishambulia CCM kwa ufisadi na hata kumtaja Lowassa.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alishawahi kumtaja Lowassa katika ‘orodha ya aibu’ ya watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, maarufu kama ‘list of shame’, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwembe Yanga Septemba 15, 2008.

Lakini juzi wakati wa mkutano na wanahabari, viongozi hao walianza kwa nguvu moja kumtetea Lowassa kuwa ni “mtu safi, mchapakazi na mfuatiliaji wa karibu wa majukumu anayokabidhiwa” na kwamba iwapo angekuwa fisadi angeshafikishwa mahakamani kujibu tuhuma, kwa mujibu wa mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.

Lowassa amekuwa akikabiliwa na swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu tuhuma za Richmond na amekuwa akieleza kuwa alijiuzulu kisiasa kwa niaba ya Serikali, akieleza kuwa alikuwa akifuata maelekezo.
Mbunge huyo wa Monduli amekwenda mbali zaidi na kusema ikiwa kuna mtu mwenye uthibitisho kuwa yeye ni fisadi, ajitokeze na kufungua kesi mahakamani.
Kama hiyo haitoshi, mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu jana alitumia muda mwingi kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo, akimtetea kwa kutumia vipengele vya Katiba.

“Mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama- katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali,” alisema Lissu akinukuu Ibara ya 39 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Kamati Kuu ya Chadema katika utafiti wake, imeangalia rekodi za mahakama karibu zote za Tanzania ili kujiridhisha kama Lowassa ana ‘criminal record (rekodi ya uhalifu)’ na kubaini kuwa hana.
“Hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yeyote ya Serikali. Mengine yasiyokuwa hayo ni porojo za wasioelewa.”

Pingamizi
Hofu ya pili kwa mwanachama huyo mpya wa Chadema ni uwezekano wa kuwekewa pingamizi kwa madai ya kuanza kampeni mapema na pia kukiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Mapema kabla ya mchakato wa uteuzi wa mgombea wa urais kuanza Julai 8, mwenyekiti wa cha DP, Christopher Mtikila alisema angefungua kesi dhidi ya CCM na makada wake sita, akiwamo Lowassa, kwa madai ya kuvunja sheria na kanuni za uchaguzi.

“Watu wameanza kampeni mapema na kwa mujibu wa sheria ya nchi, taratibu pamoja na kanuni za uchaguzi ni kwamba watu hao wamevunja sheria. Kwa hiyo tunapeleka kesi mahakamani kuwashtaki wao pamoja na chama chao,” alisema Mtikila.

Hoja kama hiyo aliitoa mwenyekiti wa CCK, Constatine Akitanda.
“Watu wameshindwa kujua kwanini hakuendelea kwenye mchakato wa urais yeye na wenzie watano. Kuna dalili waliokuwa wameanza kampeni mapema, walienguliwa na CCM kutokana na sababu ya kuvunja sheria hiyo,” alisema Akitanda.

“Kifungu cha 24 hadi 26 cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi kinakataza matumizi makubwa ya fedha. Sijui Chadema wamejipangaje kwa hilo siku zijazo, lakini nachotaka kuona ni jinsi watakavyotupa karata hiyo baada ya hapo tutajua la kufanya,” alisema Akitanda huku akieleza suala la mwanasiasa kuhama chama ni la kikatiba.

Wakati Akitanda akijiuliza jinsi Chadema walivyojipanga kukabiliana na kikwazo hicho, tayari Tundu Lissu jana alimtoa hofu Lowassa kwa kumueleza kuwa sheria haimbani hadi jina lake litakapopelekwa NEC.

Lissu alisema Lowassa ana haki ya kuzungumza jambo lolote na wala hatakuwa akifanya kampeni, huku akifafanua sheria ya gharama za uchaguzi.

“Sheria hii inatafsiri neno muda wa kampeni,” alisema Lissu.
“Inasema muda wa kampeni huanzia siku wagombea wanapopitishwa na NEC kuwa wagombea. Kwa hiyo kampeni za uchaguzi zinaanza siku ya uteuzi na hivyo kinachofanyika nje ya siku ya uteuzi, huwezi kukiita kampeni za uchaguzi.”
Alisema ushauri wake wa kisheria ni kwamba Lowassa ana haki ya kuzungumza na wananchi baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais kwa tiketi ya Chadema na kusafiri kila kona ya nchi kujitambulisha.
“Ukifanya hivyo wala hutavunja sheria yoyote bali utakuwa unafanya kile walichokianzisha. Sema wewe utakuwa unakifanya vizuri zaidi,” alisema.

Mashambulizi kutoka CCM
Iwapo Lowassa atavuka pingamizi hilo, atakumbana na kikwazo kingine cha kisiasa ambacho ni mashambulizi makali kutoka viongozi wa CCM.
Tayari viongozi hao wameanza kupangua hoja mbalimbali za baadhi ya makada, akiwamo Kingunge Ngombale Mwiru, waliotuhumu kuwapo kwa ukiukwaji wa Katiba na kanuni za chama hicho katika mchakato wa kupitisha majina ya wagombea urais kiasi cha kufanya jina la Lowassa likatwe.
Wiki iliyopita makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, Pius Msekwa aliandika maoni katika gazeti dada la The Citizen akieleza namna Kamati ya Maadili ilivyochuja wagombea wa urais kwa kuzingatia maadili ili kuondoa siasa zinazoendeshwa kwa kutumia ushawishi wa fedha.
“Kama vyama vingine vimejiandaa kupuuza maadili kwa kuwakaribisha watu wanaovunja kanuni ndani ya vyama vyao, ni bora waendelee na mambo yao,” aliandika Msekwa.
Hata hivyo, katika mchakato wa urais ndani ya CCM, kati ya makada sita waliofungiwa kwa makosa ya kuanza kampeni mapema kinyume na kanuni za chama hicho, majina ya makada wawili- Bernard Membe na January Makamba- yalipitishwa na Kamati Kuu na kuwa miongoni mwa wanachama watano ambao walipelekwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura kabla ya kupata majina matatu yaliyopelekwa Mkutano Mkuu.

Nguvu ya Dk Magufuli
Kuvuka kwa vikwazo hivyo kutakuwa kumetayarisha jukwaa la waziri huyo mkuu wa zamani kuanza kupambana jukwaani na Dk Magufuli, mgombea kutoka chama kikongwe ambacho kina mizizi kila kona ya nchi huku mbunge huyo wa Chato akionekana kuwa na nguvu ya ziada kutokana na uteuzi wake kuunganisha makundi yaliyokuwa yanapambana mwanzoni mwa mbio za urais ndani ya CCM.
Ukawa watatakiwa kumnadi Lowassa usiku na mchana kuvunja himaya ya Dk Magufuli ambayo ameanza kuijenga baada ya ziara ya mikoa mbalimbali iliyofanywa kwa kofia ya kutambulishwa kwa wanachama kuanzia Julai, 12.
Awali baada ya jina la Lowassa kukatwa Julai 10, CCM ilikumbwa na janga baada ya wajumbe watatu wa Kamati Kuu kujitokeza hadharani kupinga uamuzi huo, wakidai Katiba ya chama hicho ilikiukwa, jambo ambalo ni mara ya kwanza kutokea kwenye chama hicho. Pia wajumbe wa Halmashauri Kuu walimuimbia mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete wimbo wa kupinga uamuzi wa Kamati Kuu.
Ingawa baada ya Mkutano Mkuu kumteua Dk Magufuli kugombea urais wajumbe kadhaa walioonekana kuwa kambi ya Lowassa walitoa kauli za kumuunga mkono waziri huyo wa ujenzi, hali imeanza kuonekana si shwari baada ya wabunge, madiwani na wanachama kadhaa kuanza kutangaza kuihama CCM.

No comments: