Watanzania
wengi na hata wagombea wa CCM walipigwa na butwaa kubwa baada ya kuona
Dk John Magufuli anachaguliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Ni watu
wachache walimshtukia Dk Magufuli tangu awali na kuona uwezekano wa
kiongozi huyo kufika happ alipo leo. Nataka tujadili mambo matano ambayo
nayaona kama sababu za CCM kumpa kijiti “Tingatinga” huyu.
1. Kura za kanda ya ziwa
Hili ni
jambo la kwanza ambalo liliwafanya wapanga mikakati wa CCM kumvusha
Magufuli. Ukiachilia mbali kufahamika kwake nchi nzima, lakini Magufuli
anatoka kanda ya ziwa ambako kuna wapigakura wengi lakini kukiwa na
‘hatihati’ ya majimbo mengi kuelekea upinzani. Kanda ya ziwa si salama
kwa CCM na lazima chama hicho kingehitaji mkakati wa kudhibiti
wapigakura kwa kuwaletea kitu kitakachowaamshia matumaini mapya.
Kanda ya
ziwa inaundwa na mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mwanza,
Geita na Mara na kuna jumla ya wakazi 11,832,857 kwa mujibu wa Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012. Nusu ya wapigakura walioko Kanda ya Ziwa,
yaani watu milioni tano wanaweza kuwa wapigakura, hiyo inamaanisha kuwa
hii ni idadi inayolingana na kura alizopata Rais Kikwete mwaka 2010.
Nataka
ifahamike kuwa kwa namna nchi yetu ilivyo, Kanda ya Ziwa ndiyo inaamua
nani aongoze Taifa hili na watu wa kanda hiyo wana tabia ya kujitokeza
kupiga kura. Kama tungekuwa tunafanya sensa za kiteknolojia na
zinazokusanya taarifa sahihi, naamini kanda ya ziwa ingeweza kujenga
zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa taifa hili na jambo hilo
linadhihirisha mantiki kuwa hii ni ngome ya ushindi kwa chama chochote
kile.
Hivi
karibuni, CCM imepoteza majimbo mengi kwenye kanda hii na kumtoa mgombea
urais eneo hili kuna maana nyingine ya kuwafanya wapigakura warudishe
imani kwa “mtu wa kanda yao” hata kama wasingependa kukichagua chama
chake. Mkakati wa namna hii unatumika duniani kote na umefaulu maeneo
mengi na ili uudhibiti, njia ya haraka huwa ni chama cha upinzani
kinachotaka dola nacho kutoa mgombea eneo hilohilo kama ilivyofanya NARC
mwaka 2002. Umoja huo wa Kenya ulimsimamisha Mwai Kibaki (Mkikuyu) ili
kuvunja nguvu ya chama tawala cha Kenya wakati huo (Kanu) ambacho
kilimsimamisha Uhuru Kenyatta (Mkikuyu) kwa lazima kikijua kuwa
kitapigiwa kura nyingi kutoka eneo hilo. Uwepo wa Mwai Kibaki kutoka
kabila moja na Kenyatta ulifanya Wakikuyu kugawanyika na Kibaki
akashinda kushika dola kutoka upinzani. Natumaini kwamba CCM inaijua
karata hii muhimu na imeamua kuitumia.
2. Kuvunja makundi CCM
Jambo la
pili lililofanya Dk Magufuli akapewa kijiti ndani ya CCM kwa ajili ya
uchaguzi huu ni kuwa mtu “asiye na upande”. Kiongozi huyu katika hatua
zote za utendaji wake alijiweka kando kutoonyesha kuwa ana nia ya urais
wa nchi. Alisimamia majukumu yake kiutendaji zaidi kuliko kisiasa na
hali hiyo ilimfanya akae mbali na mivutano ya kimakundi.
Hata
alipochukua fomu alikataa kuzungumza na vyombo vya habari juu ya
vipaumbele vyake, alipokuwa mikoani akikusanya sahihi za wadhamini
hakusikika, hakuwa na mabasi makubwa na hakutaka vyombo vya habari
vimfuatilie.
Kubwa
kuliko yote, hata mara moja hakuwahi kusikika akiwatishia wenzake au
kuwanyooshea vidole na kutoa misimamo. Hii ilimfanya aonekane yeye peke
yake ndiye anayeweza kukubalika na pande zote zinazovutana. Ukiachilia
mbali sifa nyingine, CCM ilihitaji kuwa na mgombea ambaye walau anaweza
kutopingwa sana na wenzake na katika hili naweza kusema kuwa
wamefanikiwa.
Nadhani
kimkakati ilikipasa chama hicho kumuondoa Lowassa na kumuacha Membe
kwenye tano bora ili wajumbe wanaomuunga mkono Lowassa (ambao naambiwa
ni nusu ya Halmashauri Kuu) wasisuse kuhudhuria vikao kwani wangekuwa na
kiu ya “kumshughulikia” Membe (hasimu mkuu wa Lowassa). Mkakati huu
ulifanikiwa vilivyo na kumbe aliposhughulikiwa Membe ndiyo mwanzo wa
kumpata Magufuli ambaye pande zote mbili (Membe na Lowassa) hazikuwa na
budi kumuunga mkono.3. Kufahamu utendaji ndani ya Serikali na
kutokukifahamu chama vizuri
Hili ni
jambo la tatu ambalo lilimvusha Dk Magufuli. Nadhani chama hicho
kilihitaji kuwa na mgombea ambaye anaitambua Serikali vizuri na anaweza
kuisimamia ipasavyo lakini akiepuka kuyumbishwa na mambo ya ndani ya
chama chake.
Dhana hii
nadhani inafanywa na CCM kama mbinu ya kuwaonyesha wapigakura kuwa
chama hicho kinatambua matatizo ya masilahi ya chama kuingizwa katika
uamuzi wa utendaji wa Serikali kila mara na njia pekee ya kulifanya
jambo hili ni kumpata mtu ambaye hajajishughulisha na masuala ya ndani
ya chama ili kama akija, aje na mipango mipya na labda awaweke katika
mstari, viongozi waandamizi ndani ya chama na wale watendaji wa kawaida.
Sijui CCM
itafanikiwa kiasi gani katika eneo hili lakini ninachotaka kusisitiza
hapa ni kwamba chama hicho kilihitaji mtu anayeweza utendaji na
usimamizi wa Serikali na ambaye huenda anaweza akahamishia kasumba hiyo
ndani ya chama. Kuwa na mantiki na mtizamo huu ni jambo moja na uwezo wa
kusimamia masuala haya yatendeke ni jambo jingine lakini yote haya
ndiyo yanayomkabili Dk Magufuli kwa sababu amechaguliwa na chama chake
kwa kulenga shabaha hiyo.
4. Uwepo wa Ukawa
CCM
inaweza kuwa imeshabadili mtizamo wake wa kufanya mzaha na upinzani hasa
baada ya Ukawa kuishi mwaka mzima na miezi kadhaa bila kuvunjika. Huko
nyuma “miungano ya vyama vya upinzani” ilionekana kama “safari ya
panya”, kwamba wakiparaganyishwa kila mtu anapita njia yake na
wanaachana. Kama kusingekuwa na Ukawa ni lazima CCM ingekuja na mkakati
wa kawaida na mgombea yeyote yule. Lakini uwepo wake, kuungwa mkono kwa
umoja huo na wananchi, vimeilazimisha CCM itafute mgombea mbadala ambaye
ataonekana “anathubutu” kama wanavyofanya viongozi wa Ukawa ili
kujaribu kuwajengea wananchi taswira kuwa “...mlitaka mtu ambaye
anasimamia mambo bila mchezo na bila woga, sasa tumewaletea mtu huyo”.
Sauti hii
ambayo CCM inajaribu kuipandikiza kwenye mioyo ya Watanzania hata
hivyo, inatofautiana kabisa na hali halisi ambayo inabaki kuwa umakini,
utendaji na usimamizi wa upinzani ungeweza kufanywa vizuri zaidi kwa
sababu ya kutokuwa na mibinyo kutoka ndani ya watu waliozoea mfumo wa
kukaa ndani ya Serikali. Hata hivyo, kwa kiasi fulani dhana hii ya CCM
itafanikiwa.
5. Kura za vijana, wanawake
Aina ya
watu ambao huvutia kura za wanawake na vijana huwa siyo lazima wawe
vijana au wanawake, hata wazee na watu wa makamo wenye mtizamo wa
kifikra na wanatenda mambo yao haraka kama vijana huchukuliwa kwenye
kundi hili.
Vijana
wengi wanaweza kuwa mashabiki wa “Magufuli” kutokana na tabia yake ya
kuwajibisha watendaji wake hadharani na papo kwa papo. Vijana wengi
huishi maisha ya kutegemea maisha ya “fasta fasta” yaani matokeo ya papo
kwa hapo. Vijana hutaka “mwizi akiiba auawe hapohapo”, hawataki
apelekwe mahakamani wala asikilizwe. Magufuli ana tabia za kufanya
maamuzi papo kwa hapo na haiba hii inaweza kuwavutia vijana maana
wanategemea kuwa na Rais ambaye anaweza kufika mahali akatoa maamuzi ya
papo kwa papo. Ila pia ana mtihani wa kuhakikisha kuwa analinda na
kuzingatia haki za binadamu.
Hitimisho
Mambo
haya matano yaliyompa Magufuli tiketi ya kugombea urais kupitia CCM
yanaweza kabisa kuzuiwa na uimara wa UKAWA. Umoja huo ukipata mgombea
thabiti na akajikita pia katika kudhibiti kura za kanda ya ziwa,
kuonyesha uthubutu na mipango inayotekelezeka na anayewavutia vijana na
wanawake lazima CCM itakuwa kwenye wakati mgumu kwenye uchaguzi wa mwaka
huu na Magufuli atakutana na vizingiti vinavyoweza kumkwamisha na hivyo
kuondoa kabisa matumaini ya CCM kuongoza dola.Kama UKAWA ikishindwa
kufanya kazi pamoja kwenye uchaguzi wa mwaka huu, wananchi hawatafikiria
mara mbili – watamchagua Magufuli kwa kishindo na hakutakuwa na mtu wa
kulaumu mwingine. UKAWA ndiyo ngao pekee ya kudhibiti uimara wa mgombea
wa CCM na kudhibiti imani ya wapigakura wa maeneo yenye watu wengi kama
kanda ya ziwa.


No comments:
Post a Comment