Dar es Salaam.
Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza kuhama CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema pande hizo mbili zimefanya uamuzi mgumu ambao utanufaisha kila upande.
Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza kuhama CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema pande hizo mbili zimefanya uamuzi mgumu ambao utanufaisha kila upande.
Profesa
wa Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema uamuzi huo wa
Lowassa ambaye alitangaza kujiunga na Chadema na kufafanua kuwa
amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani kutekeleza azma yake ya
kuwakomboa Watanzania na kuendeleza safari ya matumaini ni uamuzi mgumu.
Alisema: “Lowassa amefanya uamuzi mgumu kutoka CCM lakini hata wapinzani wamefanya uamuzi mgumu kumpokea.”
Alisema
sababu kubwa ya Chadema kukubali kumpokea Lowassa ambaye leo
anatarajiwa kuchukua fomu kuwania urais, wakati ilikuwa inamtuhumu kwa
ufisadi inatokana na mwanasiasa huyo kuwa na watu wengi wanaomuunga
mkono, hali ambayo itaibua ushindani mpya katika siasa nchini.
Ni faida zaidi
Profesa
Mpangala alisema pamoja na Lowassa kutuhumiwa na viongozi wa vyama
vinavyounda Ukawa kwa ufisadi, uwepo wake ndani ya umoja una faida zaidi
kuliko hasara.
“Faida ya Lowassa kwenda Ukawa ni kubwa
zaidi kuliko hasara ya kuendelea kumpinga na kumtuhumu kwa ufisadi.
Ukawa wanatambua kuwa uwepo wa Lowassa utawapa kura nyingi katika
uchaguzi ujao,” alisema.
Profesa huyo alisema si jambo
la ajabu kwa mwanasiasa kuhama chama, huku akitolea mfano mwaka 1995
jinsi Augustine Mrema alivyohama CCM kwenda NCCR kuwa,
“Kama si nguvu ya Mwalimu Julius Nyerere pengine angekuwa rais,” alisema.
Mhadhiri
wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Malya
alisema katika siasa kinachotazamwa zaidi ni nafasi, na kwamba katika
siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu.
“Ila ujio wa
Lowassa Chadema lazima utazamwe, ni lazima chama hiki (Chadema)
kimtazame kiongozi huyo anakuja na kitu gani? Pia, CCM nao hata kama
hawatasema wazi, lakini kuondoka kwa Lowassa kutawatikisa kidogo,”
alisema.
Dk Malya alisema Lowassa alikuwa kiongozi
katika Serikali iliyoundwa na CCM, hivyo ni lazima aeleze kilichomshinda
kukifanya wakati huo na sababu za kutaka kuyafanya yaliyomshinda akiwa
ndani ya Ukawa.
Mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema: “Ukitazama kwa
makini utagundua kila mmoja anambeba mwenzake, yaani Lowassa anaibeba
Chadema na Ukawa na wao pia wanambeba yeye.”
Alisema
kama waziri mkuu huyo wa zamani atagombea urais kwa tiketi ya Chadema ni
wazi kuwa mpambano utakuwa mkali kati yake na mgombea urais wa CCM, Dk
John Magufuli kwa maelezo kuwa kuna baadhi ya mambo wanaendana.
“Mtaji
wa chama cha siasa ni watu na lengo kuu ni kuongoza nchi. Hakuna adui
wa kudumu katika siasa. Kilichotokea ni jambo la kawaida tu ila tu watu
wamestushwa maana hawakutegemea Lowassa kuwa atakihama CCM,” alisema.\
Lissu: Kwanini tumemkubali
Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ametaja sababu mbili za Ukawa kumkaribisha
Lowassa kuwa mgombea urais wakati chama hicho kilimtaja katika orodha
ya mafisadi mwaka 2007.
“Edward Lowassa ni mwanasiasa
asiyeeleweka na aliyewagawa watu zaidi kwa sasa katika siasa nchini na
amekuwa hivyo kwa muda mrefu. Sisi Chadema tulimweka kwenye orodha ya
mafisadi kutokana na kuhusika kwake na kashfa ya Richmond mwaka 2007.
Kwa hiyo swali halali kabisa ambalo lazima tulijibu kwa ufasaha ni hili:
‘Kwa nini tumemkubali, siyo tu kumpokea kama mwanachama, bali kumpa
heshima ya kuwa mgombea wetu wa urais? Na kwa nini washirika wetu wa
Ukawa nao wamemkubali kuwa mgombea wao wa urais?
“Jibu
ni kwamba tupo katika kipindi na mazingira ya kipekee ya kisiasa katika
nchi yetu. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu kama Taifa, tunaona
mfumo tawala ukipasuka vipandevipande. Kwa mara ya kwanza tunaona CCM
ikipasuka katikati, na mtu aliyeipasua CCM na mfumo tawala ni Edward
Lowassa.
“Sisi Chadema tumefanya kazi kubwa ya kujenga
chama tangu 2010. Tuna wagombea wengi na bora katika majimbo mengi ya
uchaguzi na ngazi ya madiwani kuliko ambavyo tumewahi kuwa nao kwa miaka
yote ya nyuma.
“Hata hivyo, ni ukweli pia kwamba kuna
maeneo mengi ya nchi ambako tuko dhaifu sana. Kwa kuingia kwake Chadema
na Ukawa, Lowassa anayaingiza maeneo hayo kwenye ulingo wa kisiasa na
sisi kuyafikia.
“Na Lowassa ataiporomosha CCM kwa
sababu ana nguvu kubwa ndani ya chama hicho kuliko mwanasiasa mwingine
yeyote. Katika mazingira ya sasa ya kipekee, tunahitaji kuamua nani ni
adui mkubwa zaidi wa nchi yetu na ustawi wake; Edward Lowassa mtuhumiwa
wa ufisadi au CCM na mfumo tawala ambao unajenga mazingira
yanayostawisha na kulinda ufisadi?
“Sisi Chadema na Ukawa tumeamua kuwa adui yetu mkubwa wa sasa na siku zote ni CCM na mfumo tawala.
Tumemkaribisha
Edward Lowassa kwa sababu kuwapo kwake kutaharakisha kuiangamiza CCM na
mfumo tawala. Tunaomba wananchi mtuelewe na kutuunga mkono?
Kwa nini Dk Slaa hakuonekana
Katika
mkutano wa kumtambulisha Lowassa, baadhi ya viongozi waandamizi wa
Chadema hawakuhudhuria, kitendo kilichofafanuliwa jana kuwa walikuwa na
majukumu mengine kichama.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
(Zanzibar), Salum Mwalimu alisema taarifa zinazosambazwa katika mitandao
ya kijamii kwamba viongozi hao wamechukizwa na uamuzi wa chama hicho
kumkubali Lowassa ajiunge Chadema, si za kweli.
Viongozi
ambao hawakuonekana katika mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya
Ledger Bahari Beach ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Naibu
wake (Bara), John Mnyika na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu
Lissu.
“Kama mnavyojua kwa sasa kuna mambo mengi
yanaendelea nchini likiwamo suala la uandikishaji wa wananchi katika
daftari la wapigakura,” alisema Mwalimu huku akifafanua kuwa mchakato
huo ni moja ya mambo yanayofuatiliwa kwa ukaribu na viongozi wa Chadema.
“Mbona
suala hili mnataka kulikuza sana. Ni kitu cha kawaida Chadema ni chama
kikubwa na viongozi wake wana shughuli nyingi za kufanya,” alisisitiza.
“Jana,
(juzi) Dk Slaa hakuwapo wala Lissu, lakini katika mkutano wa leo (jana)
Lissu kaja Dk Slaa hajaja. Na hata leo (jana) Mbowe ambaye tulikuwa
naye jana leo hayupo. Kwa hiyo ni suala la utaratibu tu na si kila tukio
lazima tuwe wote,” alisema.
Kuchukua fomu
Katika
hatua nyingine, Mwalimu alisema leo Lowassa atachukua fomu za kuomba
ridhaa ya kuwania urais kupitia Chadema katika ofisi za makao makuu ya
chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam.
“Atachukua fomu kesho (leo) na kutakuwa na shamrashamra za aina yake,” alisema.
Kingunge, Sophia wajitenga
Mwanasiasa
mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru na Waziri wa Maendeleo ya
Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba wametoa kauli zinazoashiria
kujitenga na uamuzi wa Lowassa kuondoka CCM.
Simba,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), alisema bado
ni mwanachama wa CCM na kuwa uamuzi wa Lowassa ni wa mtu binafsi.
“Mimi haunihusu, bado ni mwanachama wa CCM, tafadhali msinisumbue,” alisema.
Simba,
pamoja na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu ya CCM; Mbunge wa Songea Mjini
(CCM), Dk Emmanuel Nchimbi na Adam Kimbisa waliitisha mkutano wa
waandishi wa habari kuipinga kamati hiyo kwa kulikata jina la Lowassa
katika mchakato wa kumpata mgombea wa urais.
Aidha,
Kingunge ambaye wakati wa kusaka wadhamini katika mchakato wa awali wa
urais ndani ya CCM alijitokeza hadharani kumuunga mkono Lowassa alisema
hatua yake ya Mbunge huyo wa Monduli kuhamia Chadema ni uamuzi binafsi
hivyo hawezi kuutolea maoni yoyote.
“Kama ameondoka, basi anatakiwa aulizwe yeye na wala si mimi kwa sababu kila mtu ana maamuzi yake binafsi,” alisema.
No comments:
Post a Comment