Mbunge wa Viti Maalum alihama juzi CCM na kujiunga Chadema, Ester
Bulaya amesema licha ya kuahidiwa vyeo vingi ukiwamo uwaziri na ukuu wa
wilaya ili asihame CCM, aliamua kuviacha ili aweze kuwasaidia Watanzania
wa chini ambao wameonewa na serikali ya chama hicho kwa miaka 50
iliyopita.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyikia katika Viwanja vya
Stendi ya zamani mjini Bunda jana, Bulaya alisema wakati chama chake cha
zamani kilipogundua mikakati yake ya kuhamia Chadema, makada wake
walimwendea wakimsihi asitoke, bali abakie ili apatiwe ukuu wa wilaya au
uwaziri.
Bulaya aliyeambatana na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambaye pia
alijiunga na Chadema juzi, alisema baada ya kutafakari kwa muda mrefu
uhalisia wa maisha ya Watanzania hasa wa vijijini na jinsi ambavyo
Serikali ya CCM imekuwa ikiwatendea, aliamua kuachana na ahadi hizo na
kujiunga na Chadema kwa kuwa inalenga kuwakomboa Watanzania. “Ngojeni
niwaambie, niliahidiwa ukuu wa wilaya na uwaziri ilimradi tu nisihame
CCM. Lakini nikaona yote hayo ni upuuzi, bali cha muhimu ni kuwakomboa
Watanzania, nikaachana nayo yote nikaja Chadema,” alisema.
Bulaya aliyejigamba kukulia na kufanya kazi ndani ya CCM, alisema
chama hicho hakina sera zozote za kuwakomboa Watanzania badala yake kuna
za kuwanufaisha wachache, jambo ambali yeye na Lembeli hawakulitaka.
Bulaya alitangaza azma yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda
Mjini, akisema tayari ameshajaza fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho
kugombea nafasi hiyo.
“Niwaambie tu kwamba nimeshajaza fomu na kuirejesha na kesho (leo)
nitashiriki kura za maoni. Inshallaah Mungu akinisimamisha nitagombea
nafasi hiyo na nina uhakika wa kushinda,” alisema Bulaya.
Akihutubia mkutano huo, Lembeli aliwataka wakazi wa jimbo hilo
kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, badala yake waichague
Chadema kwa nafasi zote bila kumsahau Bulaya kwa ubunge kwa kuwa ni mtu
mwadilifu.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee akihutubia mkutano huo aliwataka
Watanzania wakubali kula fedha wanazogawa na makada wa CCM ili
wachaguliwe kwa nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani lakini
kura zote waipatie Chadema.
No comments:
Post a Comment