MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imetoa hati ya kukamatwa kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena na mwenzake
kwa kuwa hawajafika mahakamani kusomewa mashitaka yanayowakabili.
Hakimu Mkazi Thomas Simba alitoa hati hiyo baada ya kukubali ombi
lililowasilishwa na upande wa Jamhuri wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Akiwasilisha ombi hilo, Wakili wa Serikali, Vitalis Peter alidai kesi
hiyo inawakabili washitakiwa watatu, lakini mshitakiwa Venance Matondo,
ambaye ni Mhasibu wa kampuni ya Simon Group ndiye aliyefika mahakamani
hapo.
Peter aliomba hati ya kukamatwa kwa Kisena ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Bodi ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) na Ofisa Msimamizi na
Mchunguzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Adam Yusuph, kwa
kuwa waliwapelekea hati za kuitwa mahakamani lakini hawajafika.
Aidha, Wakili wa Serikali Joseph Kiula alidai, Kisena alipelekewa
hati ya wito akasaini, na walipokuwa wanampigia simu alikuwa anasema
atakuja kesho, lakini hati ilimtaka afike mahakamani jana.
Yusuph alipelekewa hati na ilisainiwa na mke wake, lakini hakufika na simu yake haipatikani.
Awali, Kiula akimsomea mashitaka Matondo, alidai kuwa Oktoba 18,
2009, yeye na Kisena walighushi hati ya malipo kwa lengo la kuonesha
kuwa Chama cha Ushirika Shinyanga 84 Ltd kilisambaza tani 1000 za mbegu
za pamba zenye thamani ya Sh milioni 145, jambo ambalo si kweli.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya
kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh
milioni 10 kila mmoja. Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 28
mwaka huu kwaajili ya kutajwa.
Pia alitoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa hao kwa kuwa upande wa
Jamhuri, umethibitisha kuwa walipelekewa hati za wito, lakini hawajafika
mahakamani.



No comments:
Post a Comment