MADEREVA wa bodaboda
ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja, wamenaswa wakizichapa
kavukavu baada ya mwenzao kuwazidi fedha za malipo yaliyotolewa na
abiria wao.
Tukio hilo la aina yake lilitokea
juzikati majira ya saa 7 mchana maeneo ya stendi wilayani Misungwi
mkoani Mwanza ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, bodaboda hao (wawili)
walidai mwenzao aliwazunguka kwa kuchukua pesa zaidi kutoka kwa abiria
waliokuwa wamewabeba na kuwapa pesa kidogo ambayo haikulingani na umbali
waliotembea kuwapeleka abiria hao.
Awali, bodaboda wote (watatu) walikuwa
katika harakati zao za kusaka abiria ambapo mmoja wao (anayedaiwa
kuwazunguka wenzake) alipata abiria watatu waliokuwa wakienda sehemu
moja ambao alielewana nao bei ya shilingi elfu mbili (2,000) kwa kila
mmoja wao kutoka eneo walipo mpaka eneo walilokuwa wakienda, bei ambayo
abiria hao waliiafiki na kumkabidhi pesa hizo ambazo jumla yake ilikuwa
shilingi elfu sita (6,000) kisha walimwambia atafute wenzake wawili,
akakubali na kufanya hivyo.
Baada ya kuwapata wenzake, bodaboda huyo
aliwaongopea kuwa wateja hao wametoa shilingi elfu moja (1,000) kila
mmoja hivyo amepokea jumla ya shilingi elfu tatu (3000) kwa madai
walikuwa hawaendi mbali.
“Wenzie walikubali lakini wakashangaa
safari ni ndefu tofauti na fedha waliyoitoa. Baada ya kuwashusha abiria,
walimbana mwenzao, akasema amepewa shilingi elfu moja kwa kila mtu.
“Jamaa hawakukubali, ikabidi wawafuate
wale abiria baada ya kuwauliza wakawaambia walimpa shilingi 6000 ndipo
walirudi kijiweni na kumkwida mwenzao ambapo naye hakukubali akaanza
kujibu mashambulizi hali iliyosababisha timbwili zito,” kilisema chanzo
chetu.
Hata hivyo, bodaboda wenye busara
waliingilia kati na kuwataka waache ugomvi, wakae chini kisha waelewane
kistaarabu ili wafikie mwafaka ambapo baada maneno hayo walimgeukia
bodaboda (anayedaiwa kuwazunguka wenzake) wakamtaka aache tamaa, awape
haki yao, ushauri ambao aliuafiki na kurudisha pesa hizo.
No comments:
Post a Comment