Mwanadiplomasia Amina Salum Ali alitangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mei 21 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu nia yake hiyo, Balozi Amina
ambaye alikuwa Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) kwenye Umoja wa
Mataifa (UN) alisema wanawake wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za juu
za uongozi kwa kukosa fedha, lakini sasa ni wakati mwafaka kwao
kujiamini katika jamii wakiamini uongozi siyo fedha, bali ni uzalendo,
kujikubali na kujiamini.
“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza
kuifikisha nchi yangu katika uchumi mkubwa kwa kutumia rasilimali
zilizopo, zikiwamo gesi, mafuta, kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba
wakati wangu umefika kuwaongoza Watanzania kwa kushika nafasi za
juu,”alisema.
Balozi Amina ambaye aliwahi kushika nafasi za juu
za uongozi Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano, ukiwamo uwaziri wa
fedha, alisema Serikali inatambua mchango wa wanawake katika jamii,
hivyo kupewa nafasi kubwa kama vile ujaji na uhakimu ni kusaidia
kuongeza ufanisi wao kiutendaji.
“Wanawake wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia
kugombea nafasi za juu za uongozi kwamba kunahitaji fedha, hivyo
wanaishia kuwa wanyonge. Siyo kweli, wajitokeze kwa wingi ili watimize
ndoto za kuwajibika kwa Taifa lao,” alisema.
Alisema sheria hazitoshelezi kumlinda mwanamke,
lakini mfumo dume umepungua kwa kiasi kikubwa hata kama haijafikia
asilimia 50 kwa 50, jambo analosema lazima liangaliwe kwa mtazamo mpya.
Elimu yake
Balozi Amina alihitimu Chuo Kikuu cha New Delhi ,
India - Shahada ya Uchumi (B.A), mwaka 1979, pia alisomea masuala ya
utawala wa fedha na utafiti wa uendeshaji kwenye Taasisi ya Uongozi
(Institute of Management) Pune, India mwaka 1980, pia mwaka 1981
alihitimu Chuo Kikuu cha Pune, India - (Symbiosis College of Management)
-MBA in Marketing (Masoko) na mwaka 1983 Chuo Kikuu cha Helsinki,
Finland - Diploma ya utafiti wa masoko na uuzaji wa bidhaa nje (mafunzo
maalum ya PRODEC).
Nyadhifa alizoshika
Mwaka 1981 hadi 1982, Mchumi Mwandamizi -Tume ya
Mipango Zanzibar, mwaka 1982 hadi 1983, Mkurugenzi Biashara za Nje -
Wizara ya Biashara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mwaka 1983 hadi
984, Katibu Bodi ya Biashara Zanzibar- Wizara ya Biashara Zanzibar.
Nafasi nyingine ni, mwaka 1984 hadi 1985, Mchumi
Mwandamizi - Tume ya Mipango, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar,
mwaka 1985 hadi 1990- Mbunge Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,
mwaka 1985 hadi 1986- Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1986 hadi 1989- Waziri wa Nchi
,Wizara ya Mambo ya Nje.
Pia, mwaka 1989 hadi 1990- Waziri wa Fedha,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1990 hadi 2000 -
Mbunge Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar, mwaka 2001 hadi 2005- Waziri wa Fedha, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar , Mjumbe wa Tume ya Mipango, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, mwaka 2005 hadi 2006- Mjumbe Baraza la Wawakilishi
.Nyingine ni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, mwaka 2006 - Mwakilishi wa Kudumu wa AU kwenye Umoja
wa Mataifa.
Uzoefu ndani ya CCM
Uzoefu ndani ya CCM
Mwaka 1968 alijiunga na Umoja wa Vijana wa ASP (ASP Youth League) na kuendelea na uanachama hadi kuzaliwa kwa CCM, 1977.
Mwaka 1977 alijiunga na CCM baada ya kuunganishwa
kwa vyama vya ASP na TANU, mwaka 2006 alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa ya chama hicho hadi alipolazimika kujiuzulu kufuatia kuteuliwa
kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa
Mataifa.
Nafasi nyingine katika chama ni mjumbe wa kamati
mbalimbali zilizoundwa na CCM kwa kipindi chote alichokuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM na mlezi wa chama Mkoa wa Morogoro.
Pia, alikuwa mlezi wa Jumuia ya Vijana, Wilaya ya
Mjini Magharibi mwaka 1992 hadi 2006 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM hadi
alipoteuliwa AU.
Serikali yake
Atayakubali matokeo
Serikali yake
Akizungumzia aina ya serikali yake atakayoiongoza
baada ya kupewa ridhaa na Watanzania kupitia CCM, alisema kipaumbele
chake ni kufufua viwanda vya ndani ili kuongeza kipato cha Watanzania.
Pia, alisema rushwa, ubadhirifu, ufisadi, mikataba mibovu na kutojali wananchi ni mambo ambayo yameendelea kuwaumiza Watanzania.
Akizungumzia kuogopana kwa viongozi katika
kuwashughulikia mafisadi, Balozi Amina alisema utaratibu uliopo ufanyiwe
marekebisho ili wahusika washughulikiwe.
Alisema ni muhimu kuweka mahakama maalumu na mtuhumiwa kusimamishwa kwa muda.
“Kesi siyo isichukue miaka sita, pia uwajibikaji
siyo majadiliano, inapotokea lazima waziri awajibike mara moja,
unapokuwa rais na chama chako unapewa dhamana tu na inapotokea kosa
lazima uwajibike kisiasa,lakini naona imekuwa tatizo mpaka mtu aondolewe
na rais, hapana,” alisema na kuongeza:
“Kuhusu hali ya kujitokeza kwa wingi wagombea
urais, siyo tatizo, ila urais si jambo la majaribio, tuwaachie
Watanzania wachague mwenye sifa, aliyekuwa bora, mwenye uwezo na mimi
ninazo sifa zote na ninaamini kuwa bora zaidi kuliko wote.”
Atayakubali matokeo
Julai 7: Alizungumza na wanadishi wa habari
visiwani Zanzibar na kuwaeleza kuwa atakubaliana na matokeo
yatakayotolewa na chama chake wakati wa kumteua mgombea atakayepeperusha
bendera ya CCM katika uchaguzi.
Alisema atahakikisha anamuunga mkono mgombea
atakayeteuliwa na chama hicho, kufafanua kuwa hajakata tamaa na ana
imani kubwa kuwa huenda chama kikamteua yeye kwa sababu sifa na vigezo
vyote vinavyohitajika anavyo, hivyo ana kila sababu ya kuteuliwa.
Alisema endapo chama kitampitisha kugombea nafasi
hiyo na kushinda, ataunda timu ya watendaji imara kwa ajili ya kuleta
mabadiliko yenye wataalamu wa kila aina kutoka pande zote za Muungano
bila upendeleo.
No comments:
Post a Comment