Kama alivyowashangaza wengi pale alipojitokeza kuchukua fomu za
kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais Mei 29 mwaka huu, ndivyo Dk John
Magufuli alivyowashangaza tena jana kufikia hatua hii ya tano bora.
Bila makeke, majivuno wala majigambo, Magufuli
ambaye ni waziri wa ujenzi alipochukua fomu alisema tu kuwa kipaumbelea
chake ni kutekeleza ilani ya uchagzi ya CCM.
Hata katika safari yake ya kusaka wadhamini
mikoani, mbunge huyo wa Chato alikwenda kimya kimya, bila mbwembwe,
ahadi wala kukusanya mashabiki.
Bila shaka hiyo ndiyo siri yake ya ushindi, alihofia kukatwa mapema kwa kukiuka masharti ya chama, kama ilivyowatokea wengine.
Hata kabla hajachukua fomu, Dk Magufuli hakuwahi
kutangaza nia yake ya kuwania urais, hadi alipoibuka ghafla na papo hapo
akapenya hadi hatua hii muhimu.
“Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote
nimekataa kulijibu kwa sababu katika chama chetu (CCM) kuna utaratibu
wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma,
vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania
nafasi mbalimbali kujitokeza. Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali
lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’.
“Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za
kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote
inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,”
alisema Dk Magufuli.
Pamoja na kutokuwa na papara za kutangaza nia wala
kuanza kupitapita kwa wanachama kutafuta kuungwa mkono, Dk Magufuli
alikuwa vinywani mwa watu wengi, ndani na nje ya CCM, wakisema
akiteuliwa anaweza kuleta ushindani dhidi ya upinzani.
Waziri huyo wa muda mrefu na maarufu kwa
kumbukumbu na kukariri takwimu mbalimbali, kila wizara anayokwenda
inageuka maarufu na kuanza kusikika, lakini kazi kubwa inayomweka kwenye
mwanga wa kisiasa napengine hata kumfikisha katika hatua hii ni wizara
ya Ujenzi na hasa usimamizi wa ujenzi wa miundombinu.
Dk Magufuli alizaliwa katika Kijiji cha
Rubambangwe kilichopo Wilaya ya Chato mkoani Geita, ndipo unapoweza
kukutana na wananchi ambao wanafahamu maisha yake ya ujana na hatua
alizopita hadi hadi hatua ya leo.
Kuna simulizi za kusisimua kuhusu maisha ya
Magufuli ambaye wananchi wengi wa jimbo lake wanamtumia kama alama ya
ushindi, akihusishwa na mafanikio ya kujitenga kutoka Wilaya ya
Biharamulo hadi wakapata jimbo na hatimaye Wilaya.
Alivyoachishwa kazi
Wakazi wa
Chato wanaamini kuwa Dk Magufuli hakuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa
mpaka aliposhawishiwa na wazee kugombea ubunge baada ya kuona wamekuwa
wanyonge kwa muda mrefu.
Mzee Emmanuel Francis anayakumbuka maisha ya ujana
ya Magufuli, ‘’Wazee tulikaa na kumuona huyu ndiye msomi wa kiwango cha
juu anayeweza kutukomboa tulikuwa tunamfuatilia tangu akiwa mwalimu
shule ya sekondari Sengerema hata alipokuwa mkemia kwenye shirika la
pamba,” alibainisha Francis.
Anasema Magufuli hakuwakatisha tama, alikubali
kujitosa kugombea ubunge akipambana na Phares Kabuye (sasa marehemu)
ingawa matokeo hayakukidhi kiu yao, japokuwa mgombea mwenyewe
aliyakubali.
Tukio la Magufuli kumshika na kumpongeza mshindani wake liliwashangaza na kumuona kama kijana asiye na kinyongo.
KIlichomponza hata hakina maana, wanasema hata
uvaaji wake wa miwani ulimpunguzia kiasi fulani cha kura baada ya baadhi
yao kuamini kuwa miwani ni kielelezo cha usomi na hivyo asingekuwa
kiongozi wa kukimbiliwa.
‘’Wasukuma tuna kasumba ya kupigiwa magoti, baadhi
ya wananchi walipomuona ni kijana anayependa kuvaa miwani walisema huyu
ndiye atatusahau kabisa,” anabainisha Francis.
Alipojaribu mara ya pili baada ya jimbo kutengwa
na kuanzishwa Chato akaibuka mshindi, sasa wanajivunia kuwa na shule
nyingi za sekondari zikiwamo wa Muungano, Meghji na Chato na nyingine
zikiwa na kidato cha tano na sita, suala ambalo Francis anasema
lisingewezekana bila Dk Magufuli.
Tetesi za urais
Wanakijiji wenzake wanakiri kuvuma kwa jina la mbunge wao na kutajwa miongoni mwa waliokuwa wanataka kuwania urais katika.
Francis anasema hana wasiwasi na kutajwa kwa jina
la mbunge wake miongoni mwa wanataka uongozi wa nchi kwa kuwa amepata
uzoefu mkubwa kupitia wizara alizoongoza katika awamu tofauti.
“Amepita katika wizara nyingi bila kuwa na tuhuma
za ubadhilifu kama ilivyotokea kwa mawaziri wengine, alionyesha uadilifu
na kila wizara aliyoongoza ilionekana kuwa imara na yenye mafanikio,”
alisema Francis.
Tangu awali, mzee huyo na wenzake walibainisha kuwa wanatamani
mbunge huyo achukue fomu ya kugombea nafasi ya urais, huku akiamini kuwa
anaweza kuungwa mkono na wananchi wengi kutokana na historia yake ya
kuwatumikia kwa uadilifu.
Hata hivyo, wasiwasi wa wengi ni kuwa waadilifu wa
aina yake ni vigumu kupata nafasi hadi kufikia kiwango cha kupendekezwa
kuwania uongozi wa nchi kwa kuwa kuna makundi hayawapendi.
Mchunga ng’ombe
Familia ya Magufuli ambaye ni baba yake na John
ilikuwa ya wafugaji, hivyo watoto waliozaliwa katika kaya hiyo kwa
vyovyote vile wasingeweza kulikwepa jukumu la kuchunga ng’ombe.
Hata wakati wa likizo wananchi walizoea kumuona
John akifanya kazi za kawaida za nyumbani ikiwa ni pamoja na kuchunga
ng’ombe na kukamua maziwa wakati wa likizo.
“Baba yake alikuwa na mifugo mingi na hakuwa mtu
wa kujikweza, wakati wa likizo tulizoea kumuona John akifanya kazi za
nyumbani hata kwenda shambani kulima na kukamua maziwa,” alisema mkazi
wa kijiji hicho.
Mkazi mwingine, Maritha Rufunga ana kumbukumbu
tofauti kuhusu maisha ya ujana wa mbunge huyo na hata hajasahau wakati
mbunge huyo kwa sasa alipoanza safari yake kielimu kwa kujikwaa.
“Hakuwa na majivuno na hata alipomaliza shule na
kushindwa kuchaguliwa baba yake alikuwa amekataa asiendelee na masomo,
lakini kuna mwalimu wake alikwenda kumtetea kwa baba yake ili akarudie
shule,” alisema Maritha Rufunga.
No comments:
Post a Comment