Dar/Mikoani.
Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield amemuuliza Rais Jakaya Kikwete iwapo ana mtu wake katika orodha ndefu ya makada waliojitokeza kuomba kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield amemuuliza Rais Jakaya Kikwete iwapo ana mtu wake katika orodha ndefu ya makada waliojitokeza kuomba kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Waziri huyo aliuliza swali hilo usiku wa
kuamkia Jumatatu (Juni 14, 2015) mjini Johannesburg, Afrika Kusini
wakati anazungumza na Rais Kikwete kutokana na wanachama wa CCM 35
kujitokeza kuchukua fomu za kuwania urais.
Viongozi hao
walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Umoja wa Afrika (AU)
uliofanyika, kwa siku mbili, kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton
Convention jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kumalizika jana.
Makada
hao wa CCM wameibua upinzani mkali kwenye mbio za urais na hadi sasa
hakuna dalili za mtu yeyote kuwa ana nafasi kubwa ya kupitishwa, hali
ambayo imesababisha vyombo vya habari kubashiri kuwa mteule wa CCM
anajulikana kwa viongozi wa juu wa chama hicho tawala.
Wakati
nchi ikijiandaa kupata kiongozi mpya atakayeongoza Serikali ya Awamu ya
Tano, mbio za urais ndani ya CCM zimevutia idadi kubwa ya wanachama
ambayo haijawahi kutokea kabla na baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama
vingi nchini mwaka 1992 baada ya watu 35 kuchukua fomu hadi sasa.
Mwaka
1995, wanaCCM waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Ali Hassan Mwinyi
walikuwa 15 na mwaka 2005 waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Benjamin
Mkapa walikuwa 11.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa mwanzoni tu mwa mazungumzo baina ya
viongozi hao, Linda alimuuliza Rais Kikwete, “Je, unaye mgombea yeyote
ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea”.
Baada
ya swali hilo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete alijibu,
“Sina mgombea ninayempendelea. Wagombea wote ni wa kwangu, ni wa chama
changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki
katika chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali”.
Kuhusu utiriri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM.
“Hiki
ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe
mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya
wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya
karibuni.
“Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha
mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu
wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”
Rais
Kikwete alisema hana tatizo na wingi wa wagombea kwa sababu haiwezekani
kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki yao.
Vile
vile, alisema wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na pia ni
ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka ndani ya chama na ni
uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa
wa mafanikio.
Uchaguzi mkuu wa Marekani utafanyika
mwakani na kwa mujibu wa taratibu zao, mchakato huanza mwaka mmoja kabla
na wagombea hupatikana Juni ya mwaka wa uchaguzi.
Hadi
sasa, makada wanne wa chama cha Democrats, ambacho kimeshika hatamu,
wamejitokeza kuwania urais, wakati katika chama cha Republican, ambacho
kina nafasi kubwa ya kushika madaraka mwakani baada ya kukaa nje kwa
miaka 10, kuna makada 12 waliojitokeza.
CCM iteue kwa staili ya Papa
Katika
hatua nyingine, mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina ameitaka
Kamati Kuu ya CCM kutumia mfumo wa Vatican wa kujifungia na kuomba siku
saba kabla ya kumpata Papa wakati itakapokutana kuteua mgombea urais wa
chama hicho baadaye mwezi huu.
Katika mchakato wa
kumchagua Papa, Makardinali kutoka sehemu mbalimbali duniani, hukutana
kwenye mji wa Vatican na kujifungia katika mkutano wao (Conclave)
wakiomba ili apatikane Papa na baada ya kukamilisha mchakato huo, moshi
mweupe huonekana juu ya jumba la mkutano kuashiria kukubalika kwake kwa
Mwenyezi Mungu.
“Mimi siwanii tena (ubunge), lakini
ninachosema, tuache ushabiki… ninaondoka, lakini nina ushauri kwa Kamati
Kuu na Halmashauri Kuu. Kwanza ninawapongeza waliojitokeza kuwania
urais lakini siyo yule msanii wa darasa la saba.
“Tuombe
Mungu atupe Rais mzuri, anayependa watu, anayependa maendeleo ya watu,
lakini na Kamati Kuu muanze kuomba Mungu kama anavyotafutwa Papa.
Makardinali wanajifungia siku saba, wanaomba, wanaomba na ninyi ombeni.
Sasa na sisi tusishabikie, tuache vikao vitaamua,” alisema Ntukamazina
wakati akichangia mjadala wa bajeti bungeni.
Membe aibukia kwa Msuya
Jana
wagombea wa CCM waliendelea na safari ya kutafuta wadhamini huku Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliibukia
kwa nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Cleopa Msuya.
Membe
alifika nyumbani kwa Msuya eneo la Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro na
kufanya naye mazungumzo akitokea mkoani Tanga ambako aliahidi kuwa
akibahatika kuingia Ikulu, kwanza atashughulika na bandari ya Tanga.
Katika
mazungumzo yao, Msuya alisema anamuunga mkono Membe katika harakati
zake za kugombea urais kwa kuwa anakidhi vigezo vilivyotajwa na Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Msuya alisema ana
matumaini CCM itamteua Membe kwa kuwa ni mgombea pekee ambaye hajawahi
kukumbwa na kashfa na amekidhi sifa zinazohitajika.
Msuya
alisema chama hicho hakipaswi kumchagua mgombea mwenye madoadoa ya
ufisadi na uchafu kwa kuwa mgombea wa aina hiyo hatawatendea haki
Watanzania.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi wa ngazi za madiwani, wabunge na rais, chama kinapaswa
kuwatanguliza watu wenye sifa na vigezo ili kupata viongozi bora
watakaowatumikia wananchi.
“Kama kweli Taifa
linawachukia mafisadi na wenye kila aina ya madoadoa, chama hakipaswi
kuwapitisha viongozi wa aina hiyo kwa kuwa
wataendeleza ufisadi huku Watanzania wakiendelea kuteseka,” alisema Msuya
“Kama
tunachukia ufisadi na matendo machafu haya yanayoendelea kufanywa na
baadhi ya watu katika Serikali yetu basi mgombea mwenye madoadoa
hataweza kuwatendea haki Watanzania kwani wananchi wanahitaji mtu safi
na asiyekuwa na aina yoyote ya uchafu,” alisema Msuya.
Pinda atikisa kwao
Mkoani
Katavi; Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameanza mbio za kusaka wadhamini
jimboni kwake Katavi ambako alipokewa kwa maandamano na kuchangiwa Sh1
milioni za kumsaidia kuzunguka katika mikoa mingine kutafuta wadhamini.
Pinda
maarufu kama “Mtoto wa Mkulima” alipokewa kwa mabango yaliyoandikwa
“Pinda siyo fisadi… ni mtoto wa mkulima… karibu nyumbani… wewe ndiye
rais ajaye”, na alisindikizwa kwa maandamano yaliyowafanya askari kuwa
na wakati mgumu kudhibiti ulinzi.
Baada ya kupata
wadhamini 9,141 katika tarafa mbalimbali za mkoa wa Katavi, Pinda
aliwashukuru na kueleza kuwa tukio hilo ni la kihistoria na kuwaomba
wananchi waendelee kumwombea ili aweze kupata ridhaa ya chama chake na
hatimaye kuwa rais.
Wasira na uchapakazi
Mkoani
Njombe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira amesema
uchapakazi na uaminifu wake ndio uliofanya kila Rais aliyepita ahitaji
kufanya naye kazi.
Wasira, ambaye pia ni mbunge wa
Bunda alisema hayo jana wakati akitafuta wadhamini katika mkoani Njombe.
Alisema asingekuwa mwaminifu, angekuwa ameshawekwa pembeni kama ambavyo
baadhi ya mawaziri wamefanywa.
“Nimekuwa sehemu ya
uongozi wa Taifa letu kwa miaka kadhaa, nimeanza na Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, akaja Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na
sasa Jakaya Kikwete, kwa hiyo ni walimu wangu wanne, uzoefu nilioupata
kutoka kwao ni shule tosha kwangu ya kuliongoza Taifa hili,” alisema
Wasira.
Bilohe na siri ya urais
Kada
wa CCM anayewania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais, Edephonce
Bilohe amesema hatishiki wala kuwaogopa wagombea wanaonunua watu kwa
nguvu ya fedha kwa kuwa uongozi ni tunu kutoka kwa Mungu.
“Natambua
kwamba nagombea nafasi hii kubwa zaidi nchini nikishindana na wasomi na
matajiri, lakini kamwe sitishwi na hawa wagombea wanaojidai kuhonga
viongozi na watu wengine ili wawaunge mkono,” alisema Bilohe.
“Tangu
nikiwa mdogo tulikuwa tunaambiwa kwamba CCM ni chama cha wakulima na
wafanyakazi, ndiyo maana mimi nikiwa mkulima katika Kijiji cha Muzye na
Mtala niliamua kwa moyo wangu wote kugombea urais ili niwawakilishe
maskini wenzangu ambao ndio wengi katika jamii na sina shaka wataniunga
mkono katika harakati zangu za kuingia Ikulu kuongoza Taifa,” alisema.
Kuhusu
migogoro ya wakulima na wafugaji, alisema: “Ni aibu nchi ya wastaarabu
kama Tanzania, inayoongozwa na viongozi wasomi bado tunashuhudia
mapigano ya wakulima na wafugaji wakigombea maeneo ya kulima na
kuchungia mifugo.
“Nchi yetu ina ardhi kubwa
isiyokaliwa na watu na haijawahi kutumika tangu dunia iumbwe, iweje sasa
watu wauane kwa ajili ya ardhi? Hili nitalikomesha.”
No comments:
Post a Comment