Dhana ya kulitizama Taifa
Kwa hali ilivyo
sasa ninaona jotoridi ikizidi kupanda katika vyama vya siasa hasa ukizingatia
michakato ya ndani ya vyama ya kuteua watakaopewa dhamana ya kugombea nafasi za
udiwani, ubunge na Urais. Kwa kiasi kikubwa kabisa, naona Wananchi wakigubikwa
na mjadala wa nani ni nani na huenda nani atapata nini. Mjadala huu licha ya
kwamba ni mzuri sana hasa katika jamii ya kiraia lakini huenda usiwe na tija sasa
kwa raia, ushauri wangu kwa raia wenzangu ni kuanza kutizama hali halisi ya
nchi yetu, tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi?
Tukijua tumetoka
wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi, itakuwa rahisi sana kujua haiba na
wajihi wa mtu ambaye tunamtaka kwa nafasi ya udiwani, ubunge na Urais na
hatutajikita katika kujadili watu na kujifunga na ushabiki wa kambi moja dhidi
ya nyingine au chama kimoja dhidi ya kingine.
Ifike pahala
mjadala wetu kuelekea uchaguzi ili uwe na tija tuutizame kwa msingi kwamba,
licha ya kwamba nchi yetu ina changamoto nyingi lakini tuna matarajio fulani
kama raia, tuna ndoto za nchi na Taifa tunalolitaka. Tukitizama amani katika
Taifa letu, amani ya mtu mmoja mmoja, amani katika jamii zetu, usalama wetu,
tukilitizama hili tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Tukiutizama Umoja wa Taifa
letu, tumekuwa tukijinasib na kauli kama Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,
je tukiutizama kwa jicho la karibu Umoja wa Taifa letu ukoje? Umoja kati ya
Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, lakini hata Zanzibar, tutizame Umoja kati
ya Unguja na Pemba, tuangalie Umoja katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa
inayomaliza muda wake hivi karibuni.
Huku Bara tutizame
Umoja kati ya dini mbalimbali lakini pia tutizame Umoja wetu kisiasa, tuna
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Vyama vya Siasa, niwaulize
tija ya kuwa na Taasisi hizi muhimu katika kujenga mustakabali wa siasa zetu
sasa na baadaye iko wapi? Juzi tu hapa mchakato wa Katiba umekwamishwa kwa
makusudi na sikuona Umoja wa kisiasa wa vyama vyote au wanasiasa wote wenye
mapenzi mema waliosimamia kweli ili kuokoa mchakato huu wa kihistoria.
Nimeangazia Amani
na Umoja wa Taifa, nikijua misingi ya uwepo wake ni Haki na Usawa, je haki za
watu na raia wa taifa letu zinalindwa, zinatunzwa, zinahifadhiwa na kutolewa
kikamilifu? Bila unafiki na kwa jibu lolote lile unaloona jema, je, haki hizi
zinapatikana kwa usawa? Usawa kati ya wasio nacho na walio nacho, usawa kati ya
masikini na matajiri, usawa kati ya wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara
wadogo-wadogo. Usawa kati ya maeneo ya mijini na maeneo ya pembezoni.
Tunaweza
tukajadili usawa wa haki lakini pia usawa wa fursa, hivi ni nani katika Taifa
letu ambao wananufaika na mikopo ya mabenki, hivi ni nani katika Taifa letu
ambao wananufaika kwa haraka na fursa za ajira. Utasema labda tuangalie tu
miongoni mwa vijana upatikanaji wa fursa za ajira ukoje, lakini juzi hapa
natizama taarifa ya Habari nasikia katika jiji la Mwanza kuna ongezeko kubwa la
wazee wasio na ajira, hii tafsiri yake nini? Tunatoka wapi, tuko wapi na
tunataka kuelekea wapi? Tukijikita katika mjadala huuu na kulitizama Taifa
hatutakuwa na muda wa kuzongwa na mbwembwe za watangaza nia ambao nia yao na
nikiwasikiliza wengi ni kufika ikulu wakati sisi tunataka tufike kule katika
nchi ya ahadi ambayo Wananchi, watu na raia wa Taifa letu wanastahili kuwepo.
Kiongozi anayeweza
kusimamia Amani na Umoja unaojengwa katika misingi ya Haki na Usawa, ni yule
mwenye uthubutu, ni yule asiyeona haya kusimama na watanzania, mwenye hekima,
mpole, baba wa wote, ishara ya Umoja wetu, jamii inamuamini na sisi tunajua kwa
hakika anajua matatizo yetu na tukimuona tunajua ana dhamira ya kweli
kutufikisha katika Tanzania tunayoitaka, kwanza kwa kuijengea misingi imara na
pili kutuleta kama Taifa pamoja.
Elimu ya kuhamasisha uandikishaji
Nina uhakika
kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura amejiandikisha, ama yuko
anajiandikisha au ameshajiandaa tayari kuandikishwa pindi Tume ya Taifa ya
Uchaguzi itakapofika katika eneo lake. Na kwa wale ambao kwa namna moja au
nyingine, kwa makusudi au kwa bahati mbaya wameikosa haki yao ya kikatiba ya
kuandikishwa kwenye daftari la wapiga kura, naomba mjitokeze mara moja sasa ili
Tume ya Uchaguzi itimize ile ahadi yake kwamba hakuna raia mwenye sifa ya
kuandikishwa atakayeachwa kuandikishwa.
Nitoe rai kwa
Wananchi wenzangu hasa wale wenye sifa ya kuandikishwa na hawajaandikishwa bado
wajitokeze, ili sote tusaidie kuikumbusha Tume ili iwaandikishe wakati muda ungalipo.
Kuhusu
uandikishwaji wa wanafunzi walioko shuleni na vyuoni, nimefuatilia hoja za
wanafunzi na hoja za Tume ya Uchaguzi, wanafunzi wana hofu juu ya watakapojiandikisha
na uhalisia wa watakapopigia kura ifikapo Oktoba 25, hapa kuna hoja. Kama zoezi
linavyoendelea kutoka mwanzoni mwa mwaka huu ni hakika kuna wanafunzi wengi
watakuwa wameandikishwa wakiwa mashuleni na vyuoni kwao na wakati wa kupiga
kura ama watakuwa shuleni na vyuoni au watakuwa likizo.
Kwa mujibu wa Tume
ya Uchaguzi, kutakuwa na fursa ya kubadili eneo la kupigia kura, ambapo mpiga
kura kule ambako anajua atakuwepo mwezi Oktoba basi atakwenda na kuboresha
taarifa zake na hapo ndipo Tume itahamisha taarifa zake za ukaazi wa awali
kwenda eneo jipya atakalopigia kura. Fursa hii ya kubadili taarifa za ukaazi
kutoka eneo moja kwenda lingine itakuwepo kati ya tarehe 11 hadi 18 Agosti
2015. Rai yangu, wanafunzi wote zingatieni fursa hii.
Wakati nikiwasihi
wanafunzi kuzingatia fursa hii, napenda nieleze pia changamoto zinazoambatana
na fursa ya kubadili eneo la kupigia kura. Wanafunzi hawa mwezi wa Agosti ama watakuwa
likizo au watakuwa shuleni na watakuwa wameandikishwa katika eneo tofauti na kwao
au shule, na tuzingatie Oktoba 25 wanafunzi hawa watakuwa wapi kwao au shule? Kama
Tume ya Uchaguzi ikijipanga vizuri mwezi Agosti na iwe zaidi ya wiki moja kama
ambavyo wao wamejipangia, basi zoezi la kuboresha taarifa kwa wale watakaotaka
kubadili maeneo ya upigaji kura litawezekana.
Bila kusahau
kwamba inawezekana kabisa baadhi ya wanafunzi watakuwa shuleni mwezi Agosti na
huenda mwezi wa Oktoba wataruhusiwa kwenda kupiga kura makwao, wanafunzi hawa
watakuwa wamenyimwa haki ya kupiga kura katika maeneo yao, Tume na Wizara ya
Elimu zingatieni hili mapema ili lisituletee lawama baadaye.
Kuhusu watangaza nia wa CCM
Nimeamua kuujadili
mchakato wa CCM kwasababu bado ni chama Kiongozi, bado nasisitiza, kila
nikipita huku na huko naona mnasemana na kunyoosheana vidole. Nawakumbusha
kwamba mbinu za ujanja haziwezi kuwaondoa wajanja. Vitabu vya dini vimeandika,
je ufalme mmoja waweza kusimama juu ya ufalme uleule? La hasha, bali ufalme
mmoja waweza kuinuka juu ya ufalme mwingine. Najaribu kusema ubaya hauwezi
kuushinda ubaya bali ni wema pekee huweza kuushinda ubaya.
Natizama siasa
zinavyoendelea nasema, siasa na mikakati ya hila kamwe haiwezi kuwa suluhisho
la kuondokana na ubaya kuelekea uteuzi, uchaguzi mkuu na hata serikali
itakapopatikana. Wagombea wabaya na ambao wamejivisha ngozi ya kondoo ni wabaya
zaidi kuliko wagombea ambao tayari mnaonekana kuwajua kama sio kuwafahamu
kwamba wao ni mbwamwitu. Mtaingia katika dhambi kubwa itakayokigharimu Chama
cha Mapinduzi kama kwa hekima ya kiMungu mtashindwa kupambanua nani ni
mbwamwitu aliyejivisha ngozi ya kondoo na mkaacha kumhukumu anavyostahili na
kukimbilia kumhukumu mbwamwitu mnayemjua, hamtakuwa mmetenda haki na kitendo
hicho kitawatafuna.
Rai yangu kwa
wazee wa CCM, baadhi yenu mnanihuzunisha sana, mimi ni kijana mdogo tu, napenda
kujifunza kwenu, lakini matendo ya baadhi yenu yananifanya nijiambie kama Mungu
akinipa uhai, aslani sitapenda kuenenda katika njia yenu, mnanichanganya kwa
hakika. Hekima yenu iko wapi? Inamaana hamuoni, inamaana na ninyi mmeingia
katika mkumbo wa kutokuona na kujitoa ufahamu, je furaha yenu ni kuona nchi ina
sintofahamu, nchi iko njiapanda na Chama cha Mapinduzi halkadharika?
Mwalimu Nyerere
hakusubiri kualikwa kutoa maoni yake, pale ilipobidi alitoa maoni yake
hadharani na Taifa likaponywa. Ninyi nasikia mnasema chinichini eti hamjaalikwa,
eti hamshirikishwi, kweli? Ama mnasubiri ratiba au mnasubiri vikao, kweli? Hivi
kusema kama mzee ni kusubiri vikao pekee? Au niseme mababa na mababu zangu na
ninyi mmeingia katika ule ugonjwa wa Taifa, ule ugonjwa wa kuogopana. Ugonjwa
mbaya kabisa, ninyi mnajua wengi wetu na kwa ubinadamu wetu usiofaa hata Mungu
hatumwogopi, je leo hii, binadamu wenzetu ni zaidi sana kuliko Mungu? Najua
wengine mko madarakani, wengine mmestaafu, lakini mimi mtoto na mjukuu wenu
nawaambia kwa hakika msipochukua hatua sasa na hatua ya hekima, mtakuwa na hoja
ya kujibu hapa duniani lakini pia mbele ya haki.
Utete wa suala la Zanzibar
Hili la Zanzibar
nimelifuatilia kwa ukaribu, ninavyoona ni kama mnalichukulia kama kitu cha
mzaha. Naona hatujifunzi kutokana na makosa, naona tunapenda sana utimilifu wa
methali kama ile ya asiyesikia la mkuu, huvunjika guu. Eti viongozi wangu, hasa
wale mlioko madarakani kwa hamuoni ya Zanzibar na namna ambavyo viashiria vya kuteteresha
amani vinavyojidhihirisha? Je mnachukua hatua gani? Je mnataka kutatua tatizo
lililoko Zanzibar kwa mbinu za hila au kwa muafaka na kuheshimiana na kulinda
maslahi ya watanzania wakaazi wa Zanzibar?
Naona kila mtu
yuko kimya, ni kana kwamba kila kitu kiko kawaida, sawa, na najua huwa ni
kawaida yenu hasa ndugu zangu wa damu kutoka Zanzibar kujitoa ufahamu kwamba
kila kitu kiko sawa. Au na ninyi mnataka mpate utimilifu wa methali za wahenga
hasa ile ya mficha maradhi kifo humuumbua? Sasa ukishakufa hata ukiumbuka
haitokuwa na mantiki lakini shida ni kwa wale ambao mnatuachia matatizo. Rai
yangu tena kwa wazee wa Bara na wa Zanzibar, tizameni matatizo ya Zanzibar na
kwa muafaka yatatueni. Na mkumbuke Mgombea Urais wa Muungano, ukomavu, hekima,
busara na uelewa wake wa hali tete ya Zanzibar utatusaidia kuishi na matokeo ya
baada ya Oktoba katika pande zote za Muungano na kuwa kiungo muhimu cha
kuuimarisha Muungano wetu.
IMEANDIKWA NA KUANDALIWA NA HUMPHREY POLEPOLE.
IMEANDIKWA NA KUANDALIWA NA HUMPHREY POLEPOLE.
No comments:
Post a Comment