Ushirikiano wahitajika kudhibiti kipindupindu kwa Wakimbizi Wa Burundi - LEKULE

Breaking

1 Jun 2015

Ushirikiano wahitajika kudhibiti kipindupindu kwa Wakimbizi Wa Burundi


SERIKALI imewaomba wananchi kushirikiana na taasisi za Serikali pamoja na mashirika binafsi, kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ulioibuliwa na wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi.
 
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donald Mbando, wakati akifunga mkutano wa tatu wa sayansi ya afya ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
 
Alisema kutokana na wimbi la wakimbizi wa Burundi walioingia mikoa ya Kigoma na Kagera, kumesababisha magonjwa ya mlipuko yakiwamo kipindupindu ambao ni hatari iwapo hakutakuwapo na ushirikiano wa kutosha kudhibiti ugonjwa huo ambao mpaka sasa umesababisha vifo vya wakimbizi saba.
 
Aidha, aliwataka watafiti wa masuala ya afya nchini kuhakikisha kwamba wanaibua hoja mpya kuhusiana na masuala ya afya zitakazosaidia kuleta mabadiliko kwenye sera za taifa zinazohusu masuala ya afya.
 
“Kwa sasa taifa linashuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyo yakuambukizwa kama vile kisukari na shinikizo la damu. Kwa bahati mbaya vituo vyetu vingi vya afya havijaandaliwa vizuri kukabiliana na magonjwa haya kwa sababu sera zetu wakati zinaandaliwa hazikujikita zaidi kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio maana tunahitaji mabadiliko kwenye hili,” alisema Dk. Mbando.
 
Dk. Mbando alizataja sababu kubwa zinazochangia ongezeko la magonjwa hayo kuwa ni pamoja na matumizi ya pombe kupita kiasi, aina ya vyakula vinavyotumiwa na Watanzania hususani wale wanaoishi maeneo ya mijini, kutokufanya mazoezi pamoja na uvutaji wa sigara.
 
Aliongeza kuwa kwa sasa Serikali ipo kwenye mpango wa kuandaa mkakati wa nne wa huduma za afya hapa nchini utakaomwezesha kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.
 
“Kwa sasa ni asilimia 20 tu ya Watanzania ndio wanamiliki bima za afya zinazotolewa na Shirika la Bima ya Afya la Taifa na mashirika binafsi na hivyo kufanya asilimia 80 ya Watanzania kuishi bila kuwa na uhakika wa masuala ya tiba….hili tumelianza tayari,” alibainisha.
 
 Akizungumza kwenye mkutano huo, Makamu Mkuu wa Muhas, Prof. Ephata Kaaya, alisema kwa sasa taifa linahitaji zaidi tafiti za kiafya hususani kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ndio sababu mkutano huo ulijikita zaidi kujadili tatizo hilo.
 
Mkutano huo wa siku mbili ulihudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 wakiwemo madaktari, viongozi na wanafunzi wa udaktari kutoka Muhas na vyuo vingine vya afya.

No comments: