TUIBEZE CHADEMA AU TUKUMBATIE MAFISADI? - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

TUIBEZE CHADEMA AU TUKUMBATIE MAFISADI?

MWAKA 2008 niliandika makala kuhusu hali halisi ya mwenendo wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bihalamulo. Makala hayo yalisababisha tafrani kati yangu na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).Uhusiano wangu na baadhi ya viongozi wa chama hicho, hasa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee uliyumba.

Uliyumba si kwa sababu nilichoandika hakikuwa sahihi bali ni kawaida ya wanasiasa kutopenda kuambiwa ukweli, pale wanapoona kuwa hoja inayozungumzwa inaweza kuwaporomosha kisiasa.
Sikustushwa na kuhamaki kwa mwanasiasa huyo hata kidogo! Niliamini kuwa hakupendezwa na habari hiyo.Nakumbuka mwanazuoni mmoja aliwahi kuandika kwamba habari nzuri ni taarifa ya kweli ambayo mtu fulani, mahali fulani, hataki ichapishwe au itangazwe, kinyume chake ni tangazo la biashara au waraka wa uhusiaono.

Katika makala hayo, nilionesha mpasuko uliokuwepo ndani ya Chadema wakati wa kampeni.Nilihusisha mpasuko huo na kushindwa kwa chama hicho katika uchaguzi huo, ambao Chadema ilikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi. Vyama vilivyokuwa na nguvu katika uchaguzi huo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema, ambapo mgombea kupitia CCM kwa wakati huo, Oscar Mukasa aliibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake, Anthony Mbasa (CHADEMA).

Nimeanza kwa utangulizi huo ili kuwaeleza wanasiasa kuwa kwenye mambo ya msingi huwa napenda kuzungumza ukweli bila kujali kuwa ninachoandika kinawafurahisha au kuwachukiza.
Nikirejea kwenye mfano wa jimbo hilo, nakumbuka nilizungumza na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na kumpa hali halisi ya mwenendo mzima wa kampeni katika uchaguzi huo na kumtahadharisha kuwa mambo fulani yalipaswa kufanyiwa kazi ili mgombea wake aibuke na ushindi. Alinisikiliza na kuahidi kuyafanyia kazi lakini sikupata muda wa kumuuliza kama alifanya hivyo au la kwa bahati mbaya Chadema ilianguka kwa tofauti  ndogo ya kura.
 Niliripoti tukio hilo kisha nikachambua sababu za chama hicho, walichukia sana kiasi cha kujadili makala yangu bungeni.
Kwa kipindi kirefu sasa nimekuwa nikifuatilia uwakilishi wa viongozi wa Chadema, na nikiri kuwa nimekuwa nikifurahishwa na utendaji kazi wao. Ilifikia wakati nikawa najiuliza iwapo wanasiasa hao hufanyiwa usahili kabla ya kuruhusiwa kuchukua fomu kugombea  ubunge  na ngazi nyingine za uongozi ndani ya chama hicho.

Tukichukulia mfano wa wabunge wa chama hicho, Freeman Mbowe (Hai), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Mnyika (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe), naweza kuwa mnafiki nisiposifia kazi zao nzuri wanazozifanya bungeni ya kutetea wananchi wa majimbo yao na masuala yanayohusu maslahi ya taifa.

Wamekuwa mstari wa mbele kufanya hivyo licha ya kwamba wakati mwingine wamekuwa wakikumbana na changamoto za utekelezaji wa miradi wanayopendekeza kutokana na kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa serikali iliyoko madarakani. Hilo ni kosa kubwa! Nitoe angalizo kwa serikali kuachana na siasa za namna hiyo.
Kwa kuwa wabunge wachapa kazi ndani ya chadema ni wengi, leo sitaweza kuwajadili wote katika safu hii, hivyo tuwaangalie akina Mnyika (Ubungo) na Halima Mdee( Kawe).

Wakati wabunge hawa wakiingia katika kinyang’anyiro cha kuwania  ubunge katika majimbo yao, mwaka 2010, kwa upande wa John Mnyika sikushangaa kushinda kwake  kutokana na ukweli kwamba harakati za mwanasiasa huyo kijana zilianza kupamba moto tangu mwaka 2005.

Alikuwa na hasimu mkubwa Charles Keenja na kwa jinsi upepo wa kisiasa ulivyokuwa ukivuma niliamini kuwa ipo siku Mnyika angeweza kumwangusha mwanasiasa huyo. Aliweza kujua udhaifu wake akautumia kujijenga kisiasa kuhakikisha anachukua jimbo hilo. Alifanikiwa, nilimpongeza. Wakazi wa jimbo la Ubungo wanakumbuka Keenja aliboronga nini katika kipindi cha utawala wake.

Kwa upande mwingine, sikuwa na imani sana na Halima kwa kuwa sikuwahi kumuona akiwa na  harakati nyingi katika siasa ukimlinganisha na John Mnyika. Mara ya kwanza kumjua mwanasiasa huyu nilidhani kuwa ni miongoni mwa wanasiasa wachache ambao huendesha siasa za chini kwa chini lakini zenye mafanikio makubwa. Nilipotoka! Halima ni mwanasiasa hodari jukwaani na hata katika kazi nyingine za kisiasa. Wanaofuatilia vikao vya Bunge mtakubaliana nami kuwa akisimama kuzungumza kitu  upende usipende utamsikiliza.Amekuwa akitoa hoja za msingi kwa ukali.

Wakati akigombea jimbo la Kawe, niliwahi kuhudhuria baadhi ya mikutano yake ya kampeni, na hapo ndipo nilibaini kuwa safari yake ya kisiasa ni  ndefu. Hiyo inatokana na ukweli kwamba, si mwanasiasa wa kukurupuka bali ni mtu anayependa kuzungumzia mambo ambayo yamefanyiwa utafiti.

 Tukiangalia jiografia ya majimbo hayo na umuhimu wake katika siasa za taifa letu, bila shaka mtakubaliana nami kuwa CCM haikuamini kuwa   kutokana na nguvu zake za kifedha na ushawishi hakuna ambaye aliamini kuwa majimbo hayo muhimu yangeongozwa na vijana wadogo kutoka chadema.

Niseme kwamba baada ya chadema kuchukua majimbo hayo,CCM imekuwa ikfanya mikakati kabambe kuhakikisha kwamba majimbo hayo yanarejea kwenye himaya yake lakini imekuwa ikishindikana kutokana na wananchi kuzinduka na kujua wanasiasa makini wa kuwasaidia. Akina Nape Nnauye na Shamsa Mwangunga wanakumbuka kisiki walichokumbana nacho wakati wakitaka kumng’oa Mnyika, uchaguzi wa mwaka 2010.

Huko Kawe, nakumbuka Halima alimwangusha Angela Kizigha ambaye alikuwa akigombea kupitia CCM katika jimbo hilo, na kuiacha CCM ikiwa imeduwaa. CCM ilifanya makosa kuteua mgombea asiyeuzika kwa wapigakura na ambaye hakuwa na ushawishi wa kisiasa ikilinganishwa na Halima.
Tukiwaangalia wanasiasa hawa tunaona kuwa wamejipanga vilivyo kupambana na miamba mikubwa ndani ya CCM.

 Hiyo inatokana na ukweli kwamba katika kipindi cha miaka mitano waliokaa bungeni hawakubweteka, badala yake wamefanya kazi kubwa inayoonekana.


Natambua kuwa wamekwamishwa katika utekelezaji wa baadhi ya ahadi zao lakini ukweli ni kwamba mchango wao katika bunge umekuwa wa manufaa makubwa.Hawa ni wa wanasiasa makini wa kupigiwa mfano! Mtaji wao kisiasa umewapa mafanikio angalizo langu ni kwamba kupanga ni kuchagua hivyo tuamue kuwachagua wachapakazi au mafisadi? Kazi kwenu wapiga kura.

No comments: