JALADA LA LOWASA KUWEKWA HADHARANI - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

JALADA LA LOWASA KUWEKWA HADHARANI


DHORUBA ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, inazidi kutibua mawimbi kufuatia kunaswa kwa harakati za kuchafuana miongoni mwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali nchini, imebainika kuwa pamoja na watangaza nia wengine kuwindwa na mkakati huu, mlengwa mkuu ni waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa anayeonekana kuwa tishio kwa wagombea wenzake.

 HABARI KAMILI

Duru za kisiasa kutoka ndani na nje ya CCM zinaonesha kuwa mahasimu wakuu wa mgombea huyo mwenye mvi nyingi kichwani, wameandaa jalada la maisha ya kazi na ya kibinafsi na kwamba wamepanga kuliweka hadharani kwa lengo la kujaribu kumpunguza kasi ya kuelekea ikulu.

“Mimi huwa natumiwa na mtu (hamtaji) posti za kumchafua Lowassa ili niweke kwenye ‘blogu’ yangu marafiki zangu wasome,” alisema kijana mmoja mkazi wa Sinza jijini Dar, anayemiliki blogu inayosomwa na watu 9, 200 kwa siku ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Alipoulizwa kwa nini anatumiwa kumchafua mwanasiasa huyo anayeonekana kuwa na mvuto wa kisiasa, alisema: “Ukiniuliza kwa nini siwezi kukujibu, ila unajua kuwa hapa ni mjini hakuna kitu cha bure,” alisema, maelezo yanayoonesha kwamba huenda analipwa ili kufanya kazi hiyo.

 FAILI LA LOWASSA LIMEJAA NINI?

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, faili aliloandaliwa Mh. Lowassa na mahasimu wake limesheheni mambo binafsi, familia yake na utumishi wake kwa ujumla na kwamba limetengenezwa kwa mtazamo hasi kwa lengo la kumharibia taswira mbele ya jamii.

Mmoja wa wafuasi wa mtandao unaoratibu mpango huo wa kumchafua Mh. Lowassa (jina linahifadhiwa) alilieleza gazeti hili kwa siri kwamba baada ya kubainika kuwa tuhuma za ufisadi zilizokuwa zikitumiwa na maadui wa mwanasiasa huyo kugonga mwamba, umebuniwa mpango wa kumhusisha na watuhumiwa wengine kwa lengo la kuitia nguvu kashfa hiyo.

“Wewe ni rafiki yangu lazima nikueleze ukweli, baada ya skendo ya ufisadi kupitia Richmond (Kampuni ya kufua umeme iliyokumbwa na kashfa ya mkataba wenye utata mwaka 2008 na kusababisha Lowassa ajiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu) kuonekana kushindwa kumharibia sifa kwa wananchi, umebuniwa mkakati mpya wa kumhusisha na watuhumiwa wengine.

“Kelele za sasa hivi siyo ufisadi wake tu,  zinaunganishwa na urafiki wake na wanasiasa wengine wenye tuhuma mbalimbali, mfano Anna Tibaijuka, Andrew Chenge, Nazir Karamagi, Rostam Aziz (hawa wote waliwahi kutuhumiwa katika kashfa mbalimbali ambao kwa sasa wanatajwa kuwa marafiki zake), hawa waunganishwa naye ili jamii imuone kama anashirikiana na watu wabaya kwa hiyo na yeye ni mbaya.

Mbali na hilo, faili hilo limeingizwa pia maisha na mwenendo wa watoto wa mwanasiasa huyo, afya yake, harakati zake za kisiasa, huku hoja ya kujihusisha na vitendo vya utoaji rushwa kwa lengo la kujipalilia njia ya kisiasa ikipewa kipaumbele kwa lengo la kuwafanya wananchi waamini kwamba amekuwa akiwanunua watu ili wamuunge mkono katika safari yake ya kuelekea ikulu.

 NAMNA YA KUMMALIZA

Vyanzo vyetu vinaonesha kwamba mpango wa kummaliza mwanasiasa huyo umehusisha baadhi ya vyombo vya habari, wamiliki wa mitandao mbalimbali ya kijamii na watu maarufu ambapo kila mmoja kwa nafasi yake atakuwa na jukumu la kueneza habari mbaya zinazomhusu Mh. Lowassa.
Mbali na uenezaji wa habari za aina hiyo, vyanzo vinaonesha kwamba kuna baadhi ya wanasiasa maarufu wamepewa kazi ya kuhakikisha Lowassa hapenyi kwenye vikao vya maamuzi kwa madai kuwa ananuka ufisadi na rushwa.

Aidha, mkakati umewekwa kuwashambulia kwa lugha chafu wale wote wanaomuunga mkono kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vinavyoonekana kuandika habari zinazoonekana kumbeba ambapo siku za hivi karibuni, mmoja wa wamiliki wakuu wa vyombo vya habari vyenye nguvu (siyo Global) alitumiwa meseji za matusi na watu wasiojulikana kupitia simu za mikononi wakimtuhumu kuwa vyombo vyake vya habari vinampendelea Mh. Lowassa.

 KWA NINI LOWASSA ACHAFULIWE?

Pamoja na kuwa tishio miongoni mwa wagombea wengine wa nafasi ya urais ndani na nje ya chama chake, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa tangu Lowassa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, ajiuzulu uwaziri mkuu ameshindwa kuweka wazi vielelezo vinavyoonesha namna ambavyo hakuhusika katika kashfa hiyo.

“Amekuwa kimya mno, watu wanatumia mwanya huo kumwandama lakini amekuwa haoneshi kisayansi namna ambavyo hakuhusika, njia ziko nyingi, angeomba serikali iunde tume ya uchunguzi ili ije na ukweli kama alihusika au hakuhusika.

“Lingeshindikana hilo angekwenda mahakamani kuomba mahakama itamke kuwa hana hatia kwenye sakata hilo lakini maneno matupu wakati mwingine watu hawayaamini,” alisema Joseph Mwita, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

MAFURIKO YA LOWASSA

Tangu kipyenga cha mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM kipulizwe, mwanasiasa huyo amekuwa akiungwa mkono na maelfu ya watu ambao wamekuwa wakijitokeza katika mikutano yake mbalimbali ya kuomba udhamini na ule wa kutangaza nia alioufanya kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambako idadi ya watu waliohudhuria iliwashangaza wengi.

Uungwaji mkono huo wa watu wa kada mbalimbali, Lowassa aliufananisha na mafuriko ambayo mtu hawezi kuyazuia kwa mikono, falsafa ambayo wachambuzi wa mambo wanaielezea kuwa ni sawa na kusema kuwa nguvu yake ya kisiasa haizuiliki na kwamba njia ya kwenda ikulu iko wazi.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa chama chake na wananchi wanamuona kama kiongozi asiyekuwa na sifa thabiti za kuingia ikulu na hivyo kujitokeza kwa njia nyingine kuandaa mipango ikiwemo hiyo ya kumchafulia taswira yake ili tu asiweze kufikia ndoto zake na hivyo nafasi ya urais kumwangukia mgombea mwingine.

Wagombea ambao wanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya CCM ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalum, Mark Mwandosya na January Makamba ambao wote wanaendelea na harakati za kuomba wadhamini ndani ya chama chao.

No comments: