Membe: Nikiwa Rais Nyerere atafurahi - LEKULE

Breaking

8 Jun 2015

Membe: Nikiwa Rais Nyerere atafurahi


Lindi/Dar. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ametangaza rasmi nia ya kuutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2015 akisema anatosha na kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko aliko atafurahi endapo atakuwa rais.

Membe aliyasema hayo jana kwenye Viwanja vya Ofisi ya CCM Mkoa wa Lindi katika hotuba yake ya saa moja kutangaza nia yake hiyo huku kwa kujiamini kabisa akisema kuwa yeye ndiye Rais wa Tanzania kwa miaka 10 ijayo.

Alisema katika urais wake, ataboresha elimu, ataweka msisitizo katika utawala bora, maendeleo ya jamii, uchumi na masuala mbalimbali ya kisiasa na kidiplomasia.

Huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliofika kumsikiliza, alisema amejipima na kuona anaweza.

“Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti…, nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.

“Sikukurupuka, zipo nafasi za kukurupuka na wapo wanaokurupuka, lakini si vyema kukurupuka kwa nafasi ya urais,” alisema.

Membe aliyesindikizwa na mkewe Dorcas, alisema Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu na kupiga goti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.

“Nilipiga goti nikamwambia Mwalimu, navitaka viatu vyako, alivivaa Mzee Mwinyi (Ali Hassan), Mzee Mkapa (Benjamin) na Kikwete (Jakaya), sasa nataka kuvaa mimi na nina hakika vinanitosha.

“Ninaamini vitanitosha. Nikamwambia chondechonde, kama havitanitosha, niambie… timu yangu ya mikoani ikawahi kuniambia unatosha,” alisema Membe.

Alisema alialikwa na Mzee Mwinyi katika ‘birthday’ yake ya miaka 91 na kati ya mambo aliyomwambia ni kwamba ameongoza nafasi mbalimbali, lakini hakuwahi kununua uongozi.

“Mzee Mwinyi aliniambia kuwa alipata vyeo bila kununua, alisema sikuwa na magunia ya pesa miee…, sikununua wajumbe. Sasa, utajisikiaje kununua vyeo? Utawaangalia kwa jicho gani wanapokosea na utachukua hatua gani kuwawajibisha? Kuna vitu vya kununua lakini si Ikulu. Ikulu hainunuliki.”

Utawala bora

Akizungumzia utawala bora, alisema kuwa hawezi kukaa kimya kuona rushwa, ubadhirifu, ufisadi vikichukua nafasi katika utawala wake.

“Ninawatumia salamu mapema, sitakuwa na kigugumizi kwa wanaotesa Watanzania. Nitahakikisha Watanzania wanachukia rushwa na kutakuwa na sheria kali dhidi ya mtoa na mpokeaji rushwa. Kama ni watumishi wa umma, watakwenda na maji... “Nitalinda mipaka yetu, polisi itakuwa ya kisasa na viongozi lazima wawe wanaosikiliza watu…”

Elimu na afya

Kuhusu elimu, Membe alisema ataweka mkazo mkubwa katika elimu ya ufundi na kazi itakayofuata ni kufufua vyuo vya ufundi ili wanafunzi wawe na uwezo wa kujiari au kuajiriwa kutokana na ufundi wao.

Katika sekta ya afya, alisema kuwa atahakikisha huduma za afya ya mama na mtoto zinamfuata mhusika na si kina mama kuwafuata watoa huduma.

Muungano

Alisema ataulinda Muungano kwa kuwa ni heshima ya Tanzania kimataifa kwani mpaka sasa ndiyo inayochukuliwa kama mfano kwa kuwa na Muungano imara... “Sitawavumilia watakaovuruga Muungano, nasikia kuna wanaoukebehi, nawaambia waache.”

Uchumi

Membe alisema atafanya kazi ya kuzishirikisha sekta binafsi na umma katika kuendesha uchumi na zaidi ni kuziwezesha sekta binafsi kupata mitaji mikubwa.

Alisema ana mpango ni kuwarudisha Watanzania katika uchumi wa viwanda kwa kufufua viwanda na kuboresha kilimo, ili mazao yanayozalishwa yanunuliwe hapahapa nchini na kusafirisha bidhaa.

“Hatutaki tena kusafirisha malighafi nje halafu tunaletewa bidhaa zilezile zilizosindikwa, haya mapinduzi ya viwanda ni lazima, mara tu nikiingia Ikulu Oktoba mwaka huu,” alisema.

Kadhalika, alisema kasi kubwa ya kufufua viwanda itashinikizwa na uwepo wa gesi asilia iliyovumbuliwa mikoa ya Kusini na itasaidia kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati ya umeme.

Vyombo vya habari

Membe alitaka vyombo vya habari kuvumbua uovu katika jamii kwa kuwa vinafika katika kila eneo na serikali yake itatumia taarifa hizo kufanyia kazi kikamilifu.

Alibeza muungano wa vyama vinne vya upinzani chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) akisema kuwa utaendelea kushindwa na hata mwaka huu, upinzani hauna nafasi na akaushangaa kwa tabia yao ya kudai wameibiwa kura mara zote wanaposhindwa.

Ilivyokuwa

Katika hafla hiyo, zaidi ya watu 3,000 kutoka wilaya za Lindi, Kilwa, Liwale na Nachingwea pamoja na mikoa ya Mtwara na Ruvuma, Pwani na Dar es Salaam, walisafiri kwa mabasi na magari binafsi kushuhudia uzinduzi huo na walianza kuingia uwanjani hapo saa 2.30 asubuhi kadri muda ulivyokuwa ukisonga, uwanja huo ulionekana mdogo.

Shamrashamra zilianza kuonekana mapema asubuhi kwani watu mbalimbali kwa makundi, katikati ya Mji wa Lindi walikuwa wamevalia mavazi ya njano na fulana zilizoandikwa “Twende na Membe 2015”.

Mabasi zaidi ya 50, mabasi madogo aina ya Coaster zaidi ya 20 na magari madogo mengi, ‘yaliipamba’ mitaa ya Lindi huku yakiwa yanapeperusha bendera za CCM na mabango ya kumtukuza Membe.

Ilipofika saa 5.52 asubuhi kundi la wanaCCM lilionekana likisukuma gari la Membe baada ya kuingia kwenye Viwanja vya CCM Mkoa wa Lindi na kupokewa kwa matarumbeta na shangwe kutoka kwa umati wa mashabiki wa mgombea huyo.

Kusindikizwa

Membe alisindikizwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa sambamba na wa kidini akiwamo mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani, George Kahama, Mwenyekiti wa Makanisa Lindi, Patrick Simunga, masheikh kutoka Mkoa wa Mtwara: Hassan Mpwangu, Kassim Kunengeneka, Mshamu Nanjopa, Ismail Iwalisi, Salum Malundapachi, Uwessu Mchoma, Saidi Litonele na Salum Namdidi.

Pia wabunge wa CCM; Faith Mitambo (Liwale), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini), Hasnein Murji (Mtwara Mjini), Lucy Mayenga (Viti Maalumu) na Mtutura Mtutura (Tunduru Kusini).

Wengine waliohudhuria ni wenyeviti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani pamoja na makatibu wa CCM mikoa ya Zanzibar na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mohamed Said Mohamed na Balozi mstaafu, Profesa Costa Mahalu.

Kahama

Akizungumza katika hafla hiyo, Kahama alisema, akiwa mmoja wa waasisi wa Taifa, nchi itakuwa salama kama Membe atakuwa rais wa Tanzania.

“Kama muasisi wa Tanzania nchi yetu itakuwa katika mikono salama kama Membe akipokea kijiti kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete,” alisema.

Alisema Membe ni mpenda amani, mchapakazi, mcha Mungu, muadilifu na mzoefu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa asiyekurupuka katika kuamua mambo.

Kahama ambaye amekuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi Awamu ya Tatu, alisema Membe ana elimu nzuri aliyoipata kwenye vyuo vinavyoheshimika duniani.

Alimsifia waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwamba ni shupavu na mtu makini mwenye uwezo mkubwa wa mambo ya usalama ambaye anaweza kuisadia Tanzania katika kipindi hiki ambacho kuna vitisho vya ugaidi.

Alisema ametembea katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza, Geita, Tabora na Lindi kwa lengo la kuangalia ni mwana CCM gani anayekubalika kushika nafasi ya urais.

“Ukiona mstaafu anasafiri sana mkoani mjue kuna jambo. Nilikuwa nazunguka kutafuta kiongozi bora wa kuongoza nchi hii katika awamu ya tano na nimemkuta hapa Lindi. Kiongozi huyu anayefaa kuwa rais ni Membe,” alisema na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Kahama alisema amemfahamu Membe tangu mwaka 1991 na kwamba utendaji wake ni mzuri na akawaomba wananchi wengine kumuunga mkono.

“Namuombea Membe katika safari yake hii yenye harufu ya uhakika,” alisema Kahama ambaye nafasi ya mwisho kuitumikia Serikali alikuwa Waziri wa Ushirika na Masoko.

Safari ya mafanikio

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Ali Mtopa alisema yupo na Membe katika safari yake ya mafanikio:

“Sote hapa tunasafiri na tuko kwenye gari la Membe, safari yetu si ya majaribio maana ukijaribu hufiki, hii ni safari ya mafanikio tunajua Membe atakuwa rais,” alisema.

Alisema Membe ndiye atakayemng’oa mgombea urais anayetokana na Ukawa kwa sababu ni kiongozi msafi.

Alisema safari ya Membe ni ya mafanikio na kwamba katika safari ya matumaini mtu anapotumaini vidonge, vinapoisha hufariki na kusema kuwa kamwe hawatabadili jina, chama kitabaki kuitwa CCM.

“Kuna safari ya matumaini, ukitumaini vidonge vikiisha unakufa,hii inaitwa safari ya mafanikio na unapofanya jambo unahitaji mafanikio,”alisema na kuamsha vicheko.

“Hatubadili jina, walibadili kuwa Ukawa lakini tumegundua ni ukiwa na kila mtu amwone Membe anafaa kuwa rais,” alisema Mtopa.

Wananchi

Katika safari hiyo, Membe pia alisindikizwa na wananchi wa chama hicho wakiwa na sare za chama huku wengine wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wenye kumuunga mkono,

Baadhi ya mabango hayo yalikuwa na maneno yaliyokuwa yakisomeka, Twende na Membe 2015, Membe ndiyo chaguo la Watanzania 2015, Membe kwanza ... wengine baadaye.

Baadhi ya wananchi akiwamo, Juma Nampachi alisema kuwa Membe ni kati ya watu waadilifu na hawana kashfa na anafaa kuwa Rais wa Tanzania.

Muuza maji aliyekuwa amevaa fulana ya Twende na Membe 2015 alisema: “Hakuna kama Membe.”

Mwendesha bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Said alisema kuwa Membe anafaa lakini asiwasahau akiingia madarakani.






No comments: