January: Nitateua mawaziri 18 tu - LEKULE

Breaking

8 Jun 2015

January: Nitateua mawaziri 18 tu


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba jana alitangaza nia kwa mara nyingine ya kuwania urais akiahidi serikali yake kuunda baraza la mawaziri wasiozidi 18 wasiotiliwa shaka na wananchi juu ya uwezo na uadilifu wao.

Makamba ambaye alishatangaza nia hiyo mwaka jana akiwa London, Uingereza alisema ametafakari kwa kina kuhusu changamoto zinazoikabili nchi na aina mpya ya uongozi inayohitajika na kuamua kuomba ridhaa ya urais ili azitatue.

Mwanasiasa huyo aliwaambia wananchi waliojitokeza kumsikiliza kuwa kesho atakwenda Dodoma kuchukua fomu ya kuomba ridhaa hiyo na kuongeza kuwa; “sijagombea kugombana na watu, nimegombea kupambana na changamoto za watu. Naiomba nafasi huku nikielewa kiu ya Watanzania kupata aina mpya ya uongozi wa zama za sasa utakaotoa matumaini mapya yatakayozaa Tanzania mpya. Naelewa misingi iliyojenga nchi yetu ya haki, umoja, amani na upendo na mshikamano… inayotakiwa kulindwa kwa gharama zote.”

Alisema aina ya uongozi wa utakaochaguliwa Oktoba ndiyo utakaoamua mustakabali wa nchi na majawabu mapya yatakayomtofautisha yeye na wengine.

Makamba ambaye aliyohutubia kwa takribani saa 1.17, alisema atainadi ilani ya CCM kwa nguvu zote na serikali atakayounda itaongozwa na falsafa ya uwezeshaji mpana kwa wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Sitaunda serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu… nitaunda serikali ya mawaziri 18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo wake,” alisema Makamba huku akishangiliwa.

Alisema serikali yake itakuja na vipaumbele vitano vya kukuza vipato vya watu kwa shughuli zote, huduma bora na za uhakika za kijamii; utawala bora, haki, utawala wa sheria, usimamizi wa uchumi na kulinda amani, umoja na usalama wa nchi.

Makamba (41) alieleza namna atakavyotekeleza vipaumbele vyake kama alivyokwisha eleza katika mahojiano yake yaliyomo katika kitabu cha Padri Privatus Karugendo kiitwacho Maswali na Majibu 40 juu ya Tanzania Mpya.

Kuhusu ukuzaji wa uchumi, mbunge huyo wa Bumbuli alisema ataunda baraza la uchumi litakalojumuisha wataalamu kutoka taasisi za umma, magwiji wa uchumi na wawakilishi wa sekta binafsi, litakalohakikisha uchumi unawekewa mipango ya muda mfupi na mrefu kutatua changamoto zinazoikabili nchi.

Alisema pia ataziboresha taasisi za kifedha, tume ya mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kudhibiti matatizo yanayoikabili nchi ukiwamo mfumo wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi.

Katika mipango yake ya kulinda amani na umoja alisema ataanzisha jukwaa maalumu litakalojumuisha Baraza za Maaskofu Tanzania (TEC) Jumuiya Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) litakalokuwa linakutana na rais kila baada ya miezi miwili kujadili namna ya kuimarisha umoja, amani na upendo nchini.

Alitaja mambo mengine atakayoyatekeleza kwa kuyaita majawabu mapya kuwa ni kutatua tatizo la ajira, rushwa, miundombinu, elimu, maji na umeme.

Katika mapambano dhidi ya rushwa, alisema atafanya mabadiliko ya kisheria, kimfumo, kitaasisi na kijamii yakiwamo kuipa meno Takukuru kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani, kuanzisha mahakama maalumu ya uhujumu uchumi na kuanzisha kurugenzi ya uchunguzi na mashtaka ya uhujumu uchumi.

“Katika uchaguzi huu, tunayo fursa ya kuanza safari ya kumaliza tatizo hili. Rekodi ya uadilifu sio sifa pekee ya uongozi. Lakini pia siyo jambo la kupuuzwa hata kidogo. Namna viongozi wanavyotafuta uongozi ndivyo watakavyotawala. Tunayo fursa ya kuchagua viongozi ambao hawatapata kigugumizi kupambana na rushwa. Tunayo fursa ya kuchagua viongozi ambao hawatakuwa na madeni ya kulipa. Sina shaka kabisa kwamba mimi ni kiongozi wa aina hiyo,” alisema.

Alisema serikali yake itapata fedha kutoka vyanzo mbalimbali na kutaja kiwango cha mapato kwa kuhusisha zaidi sekta binafsi, kupunguza misamaha ya kodi kutoka asilimia tatu hadi asilimia moja, kuiongezea TRA ufanisi, kukamilisha miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma na kukuza sekta ya utalii.

Ndengo aahidi kuanzia Azimio la Arusha

Musoma. Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Entrepreneurship Limited, Boniphace Ndengo amejiunga na watangazania wa urais kupitia CCM, huku akijigamba kuwa ni gia mpya itakayoanzia lilipoishia Azimio la Arusha.

Akitangazania kwenye ukumbi wa MCC mjini Musoma kwenye hafla iliyohudhuriwa na watu wachache jana, Ndengo alisema akipewa fursa ataendeleza harakati zilizoanza wakati wa muhula wa kwanza chini ya Azimio la Arusha za kujenga Taifa la watu wanaojitegemea kifikra na uchumi.

“Nimepima mahitaji ya Watanzania ya wakati huu, chama changu, majukumu ya Ofisi ya Rais kama kiongozi wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, nimejipima katika vigezo vya kitaaluma, kiuongozi na utawala. Nimeridhika pasi na shaka kwamba ninao uwezo wa kuvaa viatu hivi… ahadi yangu ni sitawaangusha na hakuna atakayejuta.”

Ndengo alisema alianza na mghahawa mdogo Mtaa wa Uhuru mjini Musoma, lakini hivi sasa anaitwa mwekezaji hivyo kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo nchini, anakusudia kujenga Tanzania kuwa kituo bora cha kimataifa cha utalii na kuifanya kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Mpango mkubwa zaidi

Ndengo alisema jambo moja linalopungua ni mpango utakaohimiza uwajibikaji na uwekezaji wenye tija, ambao utaongeza kasi ya ukuaji uchumi wa nchi na mtu mmojammoja.

“Hatuna sababu ya kumlaumu mtu yeyote, isipokuwa baada ya hapa tutakuwa na sababu ya kumlaumu ambaye atatulazimisha kuendelea kubaki katika hali hii,” alisema.

Alisema iwapo atafanikiwa kupata ridhaa ya chama chake, Serikali yake itatangaza uhuru kwa walimu, wafanyakazi, wakulima na wajasiriamali wadogo ambao wamekuwa wafungwa na watumwa wa mikopo isiyo na tija.

Alisema elimu ni nyenzo bora ambayo aliahidi kumpa kila mtoto nchini bila kujali jinsi, rangi, kabila na awe amezaliwa mjini au kijijini. Alisema tathmini ya sasa inaonyesha kuwa zipo kasoro ambazo lazima zirekebishwe ili mfumo wa elimu wa nchi uwe nyenzo muhimu kwa vijana, kutoa mchango wao kulijenga taifa.

Ndengo alisema rasilimali bora kwa Watanzania ni ardhi, hivyo ataitumia kuondoa umaskini kwa kuhakikisha wanapata haki ya kumiliki na kuitumia.

“Tusipoweka sera madhubuti za umiliki na matumizi ya ardhi, sera zitakazojali masilahi ya watu maskini, tutajikuta sehemu kubwa ya ardhi katika taifa hili inamilikiwa na watu wachache na hao wengine wakibaki kuwa maskini hohehahe,” alisema.

Alisema maadui wakuu wa taifa hivi sasa ni rushwa na ujinga ambao huzaa ufisadi hatimaye umaskini na akipata ridhaa ya wanaCCM na Watanzania, amekusudia kupambana na kutokomeza hayo ndani ya mwaka mmoja.



No comments: