MASHINE HATARI YATUA YANGA - LEKULE

Breaking

22 Jun 2015

MASHINE HATARI YATUA YANGA

KUMEKUCHA Jangwani! Huenda ukawa ni mwaka mwingine wa neema Yanga kutokana na kikosi hicho kusukwa vizuri kwa ajili ya mashindano. Kwa taarifa ni kwamba yule straika msumbufu kwa mabeki, Donald Ngoma, raia wa Zimbabwe, anatarajiwa kutua Yanga wakati wowote ndani ya wiki hii kwa ajili ya kumalizana na timu hiyo.
Hayo yote yamekuja baada ya TFF kupitisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni na Yanga inataka kuitumia nafasi hiyo kujiboresha kwa ajili ya michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Tayari Ngoma ameshatumiwa tiketi na sasa kinachosubiriwa ni kutua kwake tu. Inaelezwa kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, yupo tayari kumwaga fedha sasa kuhakikisha kikosi chake kinakuwa bora kimataifa.
Makubaliano ya awali ni kwamba Ngoma atapewa dola 250,000, zaidi ya Sh milioni 800, lakini Yanga wanasikilizia atue kwanza ili kuangalia uwezekano wa kupunguza kidogo.
 Kikizungumza na lekule blog chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimefunguka kuwa, tayari mazungumzo na mchezaji huyo yameshakamilika na alitumiwa tiketi wiki iliyopita na wakati wowote wiki hii atatua kwa ajili ya kuanza mazoezi pamoja na wenzake.
“Ngoma anatarajia kutua nchini siku yoyote kuanzia Jumatatu, tayari ameshatumiwa tiketi ya kuja nchini kuanza mazoezi na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.
“Wachezaji wengine wa kimataifa wanatarajia kuanza mazoezi Jumatatu katika Uwanja wa Karume ikiwa ni pamoja na wachezaji wengine waliosajiliwa hapa, hivyo kikosi kinatarajia kuwa kamili pamoja na wachezaji wa timu ya taifa,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro kuzungumzia suala hilo, alisema hawezi kulizungumzia mpaka wakati mwafaka utakapofika.

Aliyeiua Stars mikononi mwa Pluijm…

Si ulipata taarifa kwamba timu ya taifa, Taifa Stars juzi ilipigwa mabao 3-0 na Uganda? Sasa mfungaji wa mabao mawili ya Uganda siku hiyo, Erisa Sekisambu anatua nchini Alhamisi ya keshokutwa kuifuata Yanga SC. Sekisambu alileta ‘msiba’ mkubwa Tanzania juzi Jumamosi alipoifunga Stars mabao mawili ya kuongoza kwenye dakika 38 na 65 kabla ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Uganda 2014/15, Farouk Miya ambaye ni mchezaji wa mabingwa wa ligi hiyo, Vipers SC, kukandamiza bao la tatu kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 90.
Mchezo huo ulikuwa ni wa kuwania kufuzu Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Mchezo wa marudiano utapigwa baada ya wiki mbili nchini Uganda kwenye Uwanja wa Namboole na Stars itahitaji kushinda mabao 4-0 kusonga mbele.
Sekisambu ambaye ana faili kubwa la soka nchini Uganda kutokana na umahiri wake aliouonyesha msimu uliomalizika hivi karibuni, anatarajia kutua nchini na timu yake ya SC Villa ya Uganda kwa ajili ya kuumana na Yanga iliyo chini ya Mdachi, Hans van Der Pluijm kwenye mchezo wao wa kirafiki utakaopigwa Juni 27, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar.
Inaelezwa kuwa tayari Yanga wameshapata taarifa juu ya mshambuliaji huyo ambaye anatajwa na vyombo vya habari vya Uganda kuwa ni mmoja wa wachezaji wenye thamani kubwa nchini humo kwa sasa, hivyo juhudi za kupambana naye zimeshaanza kuelekezwa juu yake.

Mbali na hayo, Yanga pia ambayo bado ipo mawindoni katika kusajili vifaa vya uhakika kwa ajili ya msimu ujao, inaweza pia kumtolea jicho mshambuliaji huyo aliyeisaidia Villa kumaliza kwenye nafasi ya pili katika ligi na kutwaa ubingwa wa Kombe la Ligi Uganda 2015 huku yeye akiibuka mchezaji bora kwenye michuano hiyo.
Katika mchezo wa Stars juzi, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, aliomba karatasi ya majina ya wachezaji wa Uganda na akaonekana kuiangalia kwa makini kila wakati mechi ilipokuwa ikiendelea, hatua ambayo inaonyesha kuna kitu anakitafuta.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkurugenzi wa Nyumbani Kwanza Media Group, Mossi Magere, ambao ndiyo waratibu wa mechi hiyo, amesema kwamba kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa na Villa wataondoka kwao keshokutwa Jumatano na Alhamisi watakuwa Dar tayari kwa mchezo huo.
“Tayari kila kitu kimekamilika, tumeshaongea na Fufa (Shirikisho la Soka Uganda) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania TFF, kwa hiyo kila kitu kipo sawa na tumekubaliana na Villa kuwa wanakuja na kikosi chao kizima, hivyo yule mchezaji wao bora, Erisa pia atakuwepo,” alisema Magere.
Hata hivyo, taarifa nyingine pia inafafanua kwamba, benchi la ufundi la Yanga litautumia mchezo huo kumpa nafasi kiungo Msierra Leone, Lansana Kamara, kuonyesha uwezo wake kama anastahili kumwaga wino kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara 2014/15 au la.
Kwa sasa Kamara anaendelea kufanya majaribio katika kikosi hicho kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea katika Uwanja wa Karume jijini Dar.

 Beki noma Mganda atua kumrithi Sherman

Taarifa nyingine ambazo Championi Jumatatu limezipata jana jioni, zinasema Yanga inatarajiwa kuanza mazungumzo haraka na Klabu ya Express ya Uganda kwa ajili ya kumnasa beki mwenye uwezo mkubwa, Bakari Shafiq.
Pluijm alikuwa Zanzibar kuiangalia Taifa Stars ikicheza dhidi ya Uganda juzi lakini ‘tageti’ yake kubwa ilikuwa ni kuangalia beki wa kumsajili na amewataarifu viongozi wa Yanga kuwa amevutiwa na Shafiq mwenye uwezo wa kucheza beki ya kati na kulia.
Kama beki huyo akitua Yanga, mpango utakuwa ni kumtema Mliberia Kpah Sherman aliyefunga mabao manne msimu uliopita na Shafiq achukue nafasi yake.
Pluijm amekuwa hafurahishwi na Kelvin Yondani na anataka beki mwingine hatari wa kutengeneza kombinesheni na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

No comments: