Jaji Warioba: Sitaongea Chochote Kuhusu Uongozi kuelekea Uchaguzi - LEKULE

Breaking

21 Jun 2015

Jaji Warioba: Sitaongea Chochote Kuhusu Uongozi kuelekea Uchaguzi

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba amesema hatoongea chochote kinachohusu masuala ya uongozi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika Oktoba.
 
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa kampeni ya Vuguvugu la Uhuishaji Maadili inayofanywa na chama cha wataalam Mbalimbali wa wakristo(CPT)alipotakiwa kutoa maoni kuhusu mchakato wa uchukuaji fomu za kugombe urais unaoendelea katika Chama Cha Mapinduzi(CCM).
 
 Alisema katika kipindi hiki  cha mchakato wa kuelekea katika uchaguzi mkuu sio raisi  mtu akaongea jambo la msingi likaeleweka katika jamii.
 
Nilisema kwa kipindi hiki nitakaa kimya sitoongea,kwa sababu muda huu ukisema chochote kinahusishwa na uchaguzi mkuu  jambo ambalo sitaki linitokee,hata hapa nimekubali mwaliko huu kwa sababu ya ushawishi  ha heshima ya rafiki yangu (Profesa Kanywanyi)”alisema  Jaji Warioba.
 
Alisema  hakubaliani na baadhi ya watangaza nia wanaojiita waadilifu  kwakuwa kuna baadhi yao wanatoa rushwa na wengine wanafuata taratibu za kawaida katika mchakato huo.
 
Alisema  kulingana na misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kila mtanzania anapaswa kuwa mzalendo na mwajibikaji.
 
Alisema mgongano wa maslahi katika baadhi ya maeneo ni chanzo cha ufisadi kuporomoka kwa maadili mambo ambayo yanaweza kuhatarisha amani ya nchi.
 
“Viongozi na jamii kwa ujumla wanapaswa waichunge amani iliyopo nchini kwakuwa ikipotea itakuwa aibu kwa Taifa,”alisema Warioba.
 
Alisema kwa sasa kuna dalili ya ukabila,udini  na ubaguzi wa rangi,kikanda  na wakichama unaanza kurudi jambo ambalo linachangia kuhatarisha amani na uporomoshaji wa maadili.
 
Alisema   nchi haiwezi kuwa na viongozi wenye maadili endapo jamii inayowazunguka haina maadili.
 
“Jamii haionyeshi kama inataka viongozi wenye maadili kwakuwa inachangia kuporomosha maadili,hakuna mtu ambaye anaweza akamrekebisha mwenzake katika hili,”alisema Jaji Warioba.
 
Awali akitoa mada kuhusu suala la uhuishaji  maadili Mwnyekiti wa CPT,Profesa Beda Mutagahwya alisema  kwa sasa Taifa limekuwa na kashfa mbalimbali zinazohusisha watumishi wa umma na watawala ambao wengi wao hawajachukuliwa hatua zozote za kinidhamu na kisheria.
 
“Kumekuwa na wimbi la rushwa,uvunjaji wa haki za binadamu  bila kuchukuliwa hatua,uvunjaji wa haki za binadamu bila kuchukuliwa yote haya yanaamsha hasira za umma na kutufanya tusema sasa yatosha,”alisema  Profesa Mutagahwya.
 
Alisema kitendo cha kutafsiri  kama bahati mbaya ama ajali kazini kwa matukio ya dhuluma na maovu  ni kudalilisha Taifa kwakuonekana limekosa umakini.
 
Alisema kuna umuhimu wa kujenga upya maadili ya Taifa ambayo kwa sasa yameporomoka na kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.
 

Alisisitiza wahusika wanapaswa kutunga miundo mipya ya utawala,sheria mpya,kuimarisha vyombo vya usalama  pamoja na kuunda tume za maadili na taasisi za kuzuia rushwa.

No comments: