Hoteli JB Belmont Yafungwa Mwanza kwa Kushindwa Kutimiza Masharti ya Mkataba. - LEKULE

Breaking

21 Jun 2015

Hoteli JB Belmont Yafungwa Mwanza kwa Kushindwa Kutimiza Masharti ya Mkataba.

HOTELI yenye hadhi ya nyota tano ya JB Belmont iliyoko jijini hapa, imefungwa kwa kile kilichoelezwa kuwa imeshindwa kutimiza masharti ya mkataba baina yake na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
 
JB Belmont ambayo inatumiwa zaidi na wageni wa kimataifa wakiwamo viongozi wa juu wa Serikali na wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa, ilifungwa jana asubuhi kwa tangazo linaloaminika kubandikwa na watumishi wa NSSF.
 
Baada ya kubandikwa kwa tangazo hilo, kuliwekwa kizuizi cha kamba kuwazuia watu kuingia hotelini jambo lililosababisha taharuki kwa baadhi ya wateja ambao walibaki wamepigwa butwaa pasipo kujua la  kufanya.
 
Hoteli hiyo inamilikiwa na familia ya marehemu Justus Buguma ambaye ni raia wa Uganda, na kabla yake ilikuwa chini ya umiliki wa aliyekuwa Mbunge wa Vunjo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aloyce Kimaro na ilikuwa ikifahamika kwa jina la Nyumbani Hotel.
 
Habari ambazo zimeifikia LEKULE  zinaeleza kuwa familia ya Bugumba nayo imeondolewa kwenye umiliki wa hoteli hiyo na NSSF baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango.
 
Alipoulizwa Meneja wa Kanda ya Ziwa wa NSSF, Hamis Fakhi kuhusu kufungwa kwa hoteli hiyo na wafanyakazi wa taasisi anayoiongoza, alisema jambo hilo ni kweli. Lakini alikataa kueleza sababu za kufikiwa uamuzi huo.
 

“Ni kweli tumefunga hoteli hiyo, lakini sina maelezo mengi ya hilo, nasema hivyo kwa sababu makubaliano ya mkataba kati ya mmiliki wa hoteli na NSSF yalifanyikia makao makuu,” alisema Fakhi.

No comments: