Dar es Salaam.
Hatua ya Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, Augustino Ramadhani kujitosa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais imewavuruga wagombea wenzake wa urais na kuibua mjadala mzito katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua ya Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, Augustino Ramadhani kujitosa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais imewavuruga wagombea wenzake wa urais na kuibua mjadala mzito katika maeneo mbalimbali nchini.
Mitandao ya
kijamii ilijaa mijadala inayohusu kuingia kwake katika kinyang’anyiro
hicho, huku baadhi ya wapambe wa wagombea wakieleza wazi kukatishwa
tamaa na mgombea huyo ambaye wasifu wake unaonyesha ana sifa za ziada
zaidi ya baadhi ya wagombea.
Miongoni mwa hoja
zilizoibuliwa ni sifa ambazo CCM huzitumia bila kuzitaja, hasa kile
kinachoitwa zamu kati ya Bara na Zanzibar na nyinginezo, ikielezwa kuwa
akihitajika mgombea kutoka Zanzibar kumrithi Rais Jakaya Kikwete, Jaji
Ramadhani anaonekana kufaa zaidi.
Katika mijadala hiyo,
wapo waliohusisha hukumu alizowahi kuzitoa akiwa Jaji na baadaye Jaji
Mkuu kwamba zililenga kukibeba chama hicho tawala kwa sababu anaonekana
alikuwa na mapenzi nacho siku nyingi lakini wengine walieleza kuwa
hawaoni tatizo kwa jaji huyo ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya
Haki za Binadamu.
Jaji Ramadhani ajibu hoja
Wakati
maoni ya wananchi yakitofautiana juu ya hatua ya Brigedia Jenerali huyo
mstaafu kuchukua fomu, mwenyewe aliliambia gazeti hili jana kwamba kwa
sasa si jaji tena, hivyo ana haki ya kugombea urais na hakuna kanuni
wala sheria inayomzuia.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya
kuulizwa swali kuhusu Ibara ya 113A ya Katiba ya Tanzania inayotajwa
kumzuia, ikisema; “Itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani,
Jaji wa Mahakama Kuu, Hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote
cha siasa, isipokuwa tu kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa
katika ibara ya 5 ya Katiba.”
“Ukisoma Ibara hiyo
inasema kama mhusika ni jaji. Mimi huko nimeshaondoka sasa nitashindwa
kugombea kwa lipi? Wacha watu waibue mambo tu, lakini hata ukisoma
Katiba utaona mwenyewe wao wanazungumzia past tense (wakati uliopita),
sasa tunazungumzia present tense (wakati uliopo),” alisema.
Kuhusu
mapenzi kwa CCM yanayoweza kuathiri utendaji, Jaji Ramadhani alihoji,
“Hukumu gani niliipendelea? Hakuna kitu kama hicho. Kuanzia 1961
tulivyopata uhuru, majaji hawakuwa kwenye chama? Sasa kuna ajabu gani
mimi kuwa katika chama maana kipindi hicho kulikuwa na chama kimoja tu,
watu wote walikuwa katika chama si majaji tu.
“Zamani
(wakati wa chama kimoja), ulikuwa huwezi kupata kazi ya aina yoyote kama
wewe si mwanachama. Leo ajabu ni mimi tu. Hata wanahabari ilikuwa
lazima wawe wanachama.”
Jaji Ramadhani ambaye alikuwa
Makamu Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, juzi mchana
alichukua fomu kuwania nafasi hiyo ya kuongoza Serikali ya Awamu ya
Tano huku akisema; chema chajiuza, kibaya chajitembeza.
Katika
maelezo yake alisema alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu
tangu Agosti, 1969 wakati huo akiwa mwanafunzi wa Sheria katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema alipotuma maombi ya
kujiunga na jeshi alitakiwa kuwa mwanachama wa Tanu ndipo ajiunge na
jeshi na baada ya kufanikiwa kupata kadi ya Tanu aliendelea kuwa
mwanachama wa CCM hadi mwaka 1992.
Alisema wakati mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanza na
Katiba kukataza majaji kuwa wanachama wa vyama vya siasa, alijiondoa CCM
na alirejea alipostaafu ujaji mwaka 2011.
Wanasheria wampinga
Hata
hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema na mwanasheria nguli, Profesa
Abdallah Safari alisema: “Anajipa moyo tu. Nchi zilizopo katika Jumuiya
ya Madola, ikiwamo Tanzania, zinazuia majaji kujiingiza katika shughuli
za siasa, japo wanatakiwa kufanya shughuli nyingine, ikiwamo kufundisha.
“Haki
ili itendeke lazima ionekane. Inakuwaje Jaji anakaa mahakamani na
baadaye kuamua kujitosa katika siasa. Akifanya hivyo inatafsiriwa kwamba
akiwa jaji alikuwa akikilinda chama alichopo sasa.”
Profesa
Safari alitolea mfano hukumu ya Jaji Ramadhani na wenzake sita katika
kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila ya kutaka Mahakama
itambue mgombea binafsi na kusisitiza kuwa ilipingwa na wananchi,
akiwamo Jaji Mkuu aliyemtangulia, Barnabas Samatta.
“Jaji
Samatta aliiponda hukumu ile na kufanya Jaji Ramadhani na wenzake
waonekane hawakufanya kitu. Watu walihoji iweje majaji wote saba wawe na
mtazamo wa pamoja labda walikuwa wakiilinda CCM,” alisema Profesa
Safari na kusisitiza kuwa uamuzi wake wa sasa utawashangaza majaji wa
nchi za Jumuiya ya Madola.
Mhadhiri wa Shule Kuu ya
Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema:
“Uamuzi wake unaleta utata. Hakuna sheria inayombana ila inaonekana kama
aliendelea kubaki na kadi ya CCM au mapenzi na chama hicho kipindi
chote cha ujaji wake.” Alisema kwa sasa Jaji Ramadhani yupo Mahakama ya
Afrika na jambo hilo halileti picha nzuri kwa demokrasia nchini.
“Tunaonekana hatuheshimu misingi ya sheria. Hii inaweza kuleta picha
kwamba Serikali inatumia watendaji wake kwa masilahi ya chama.”
Jesse
alitolea mfano jinsi Rasimu ya Katiba ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ilivyopendekeza muda wa miaka mitano kwa watumishi wa Serikali
kujiingiza katika siasa lakini kipengele hicho kikaondolewa licha ya
kuwa na maana kubwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es
Salaam, Bashiru Ali alisema hakuna tatizo kwa Jaji Ramadhani kugombea
urais, akitolea mfano Jaji Mark Bomani kuwa aliwahi kujitosa kuwania
urais wakati amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
“Kwa
sasa Jaji Ramadhani si jaji tena, hivyo ana haki zote za kugombea
urais. Kama angekuwa jaji, polisi au mwanajeshi angejiuzulu na kuingia
katika siasa lakini kwa sasa hayupo tena huko,” alisema Bashiru.
Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei alisema, “Katiba inamruhusu kugombea ni haki yake.
Katiba ya CCM
Kwa
mujibu wa Katiba ya CCM Ibara ya 7, raia yeyote wa Tanzania mwenye umri
usiopungua miaka 18, anaweza kuwa mwanachama wa chama hicho iwapo
anakubali imani, malengo na madhumuni yake.
No comments:
Post a Comment