Kigoma.
Safari ya mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe kurejea bungeni imeanza rasmi baada ya kiongozi huyo wa chama kipya cha ACT-Wazalendo kuchukua fomu za kuwania kuongoza jimbo la Kigoma Mjini.
Safari ya mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe kurejea bungeni imeanza rasmi baada ya kiongozi huyo wa chama kipya cha ACT-Wazalendo kuchukua fomu za kuwania kuongoza jimbo la Kigoma Mjini.
Uamuzi
huo wa kulitaka jimbo hilo unathibitisha kauli zake ambazo amekuwa
akizitoa kwa muda mrefu kuwa hatarudi tena Kigoma Kaskazini kwa kuwa
alishawatimizia kila kitu na haoni sababu za kuwawakilisha tena wananchi
wa eneo hilo.
Kauli yake iliibua ubashiri kuwa Zitto
anataka kubadilishana jimbo na mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter
Serukamba, uvumi ambao aliukanusha akisema hadhani kama CCM inaweza
kupata jimbo Kigoma.
Zitto, ambaye alijiondoa Chadema
baada ya kukiuka katiba kwa kufungua mashtaka dhidi ya chama hicho,
hakufanya mbwembwe wakati akienda kuchukua fomu kwenye ofisi za ACT
Ujiji jana, badala yake aliita viongozi wa kata na matawi bila ya
kutaarifu vyombo vya habari.
“Nimeamua kugombea ubunge
wa Kigoma Mjini ili niwatumikie ndugu zangu ambao wamekuwa wakipata tabu
katika kupigania haki zao za msingi ambazo walistahili kuzipata kama
ilivyo katika mikoa mingine,” alisema Zitto alipoongea na mwandishi wa
Mwananchi kwa simu.
“Nitakapokuwa mbunge wa Kigoma
Mjini nitahakikisha barabara za mitaani zinapitika katika kipindi chote
cha mwaka, nitahakikisha watu wanaacha tabia ya kulima mashamba katikati
ya mitaa na makazi, lakini nitahakikisha kila mmoja anajiunga na mifuko
ya kijamii ili kujiwekea akiba ya uzeeni pamoja na kupata huduma ya
matibabu, elimu na nyinginezo zinazopatikana kwa kutumia mifuko hiyo.”
Mwenyekiti
huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema
bonde la Mto Luiche bado halijatumika ipasavyo kuzalisha chakula kwa
wingi.
“Nakusudia kuibana Serikali ijenge skimu ya
umwagiliaji maji ili wakulima walime kilimo cha mpunga kwa mwaka mzima
bila kupumzika, jambo ambalo litainua uchumi wa wakulima na kuongeza
chakula hapa Kigoma,” alisema.
Kuhusu umeme wa gridi
ya Taifa, Zitto alisema lazima upatikane ili kusaidia jitihada ya ujenzi
wa viwanda vya kusindika mazao ya uvuvi na kilimo kwa kuwa hivi sasa
mji wa Kigoma Ujiji unategemea umeme wa jenereta ambao hauwezi kuendesha
shughuli za viwanda, hali inayochangia mkoa kuendelea kuwa masikini
licha ya kuzungukwa na rasilimali nyingi.
Katibu wa ACT
wa Jimbo la Kigoma Mjini, Azizi Ally alisema Zitto alichukua fomu hiyo
jana kwa malipo ya Sh100,000 mbele ya viongozi 72 wa kata na matawi
kutoka jimboni humo.
“Kwa hali ya sasa Kigoma Mjini
inahitaji kupata mbunge anayeweza kufuatilia mambo kwa kina ili kuleta
maendeleo ya wananchi baadala ya yule anayekwenda bungeni kujifunza,”
alisema Ally.
“Watu wanakabiliwa na kero mbalimbali
kama ubovu wa barabara za mitaani, uhaba wa umeme wa uhakika unaoweza
kuendesha viwanda vikubwa na vidogo, pamoja na wengi kufanya kilimo cha
kujikimu zaidi.“
Zitto alitofautiana na uongozi wa juu
wa Chadema uliomtuhumu kuwa alikuwa amefanya uasi na kwamba
alishaanzisha chama kingine akiwa ndani ya chama hicho kikuu cha
upinzani na kusababisha avuliwe nyadhifa zote, ikiwamo ya unaibu katibu
mkuu.
Hata hivyo, wakati Chadema ikijiandaa kumjadili
na pengine kumvua uanachama, Zitto alifungua kesi akitaka mahakama
imuamuru katibu mkuu wa Chadema ampe nyaraka za mwenendo wa vikao
vilivyomvua madaraka na kuomba amri ya kuzuia vikao hivyo visimjadili.
Katika
hukumu ya kesi hiyo, mahakama ilitupilia mbali hoja zake, uamuzi
uliotafsiriwa kuwa umefungua njia ya kutimuliwa kwake kwa kitendo cha
kufungua kesi mahakamani kinyume cha katiba.
Mkazi wa
Gungu mjini Kigoma, Zuberi Mrisho alisema ujio za Zitto kugombea Ubunge
wa jimbo hilo utaamsha ari ya wananchi kujiandikisha kwa wingi katika
Daftari la Wapigakura na kujitokeza kupiga kura tofauti na chaguzi
zilizopita.
“Mwaka 2010 Vijana wengi hatukupiga kura
hapa kwa sababu tulikosa imani na baadhi ya wagombea wa nafasi
mbalimbali, lakini kwa ujio wa Zitto sasa nina hakika wengi tutajitokeza
kupiga kura ili tupate viongozi makini kwa maslahi ya mji wetu,’
alisema Mrisho.
No comments:
Post a Comment