Sousse, Tunisia. Yanga imefanyiwa vurugu za kila namna baada ya kutua jijini Tunis na wapinzani wao, Etoile du Sahel juzi, lakini kocha Hans Pluijm amesema hakuna kipya katika vitimbi hivyo.
Pluijm, pia amewataka wachezaji wake kulipa masaibu hayo uwanjani leo kwa lengo la kuwafanya Waarabu hao wajutie vitendo vyao.
Yanga, iliyotumia saa 13 kusafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Sousse, mjini ulioko umbali wa kilomita 143 kutoka Tunis, utakapofanyika mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shiriksho la Soka Afrika (CAF).
Timu hiyo iliweka kambi yake kwenye hoteli ya kisasa ya El Mourad inayotumiwa na watalii wengi zaidi wakiwa kutoka Ulaya. Kikosi hicho kilionyesha ukakamavu, kupambana na Waarabu hao kijasiri katika mchezo wa awali, kinataka leo kuufanya mwiko ule wa kuwafunga Waarabu kuwa historia. Katika mchezo huo wa marudiano utakaofanyika, saa 3: 00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ukichezeshwa na waamuzi kutoka Uganda, Denis Bate akisaidiwa na Mark Ssonko, Balikoowa Musa Ngobi, Yanga italazimika kukomaa kwa visa ndani na nje ya uwanja.
Baridi yawatesa Yanga
Kikwazo kikubwa kwa wachezaji wa Yanga kilikuwa ni baridi kali iliyokuwa ikivuma sanjari na upepo mdogo ambao ulimlazimisha kocha Pluijm kuwa mkali katika mazoezi hayo ya juzi kwa kuwataka wachezaji wake kukimbia muda wote wa mazoezi hayo, lengo likiwa ni kuzoea hali hiyo.
“Hii ni baridi kali, kinachotakiwa hapa ni kuizoea kwa haraka, najua leo (juzi) itakuwa ngumu kwao, lakini kesho (jana) wakikimbia kidogo watafungua mapafu yao, tunatakiwa kuizoea kwa haraka hakuna njia ya mkato katika hilo,” alisema Pluijm. Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Pluijm alisema wanajua watakutana na wakati mgumu kufuatia Etoile kutaka matokeo mazuri wakiwa kwao, lakini wamejipanga kufanya kila kitu kushinda mechi ya leo.
Alisema kila kitu kinawezekana kwao kufuatia matokeo ya awali ya timu hizo kufungana bao 1-1 na sasa wanataka kufanya kama Etoile walichofanya Dar es Salaam kwa kutafuta bao la ugenini litakalowapa shida Waarabu.
Daktari adhibiti vyakula
Wakati Pluijm akizungumzia ufundi, daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani alikuwa na kazi ya kuangalia ofisi yake akilazimika kusimamia uandaliwaji wa vyakula akigomea baadhi ya vyakula.
Niyonzima, Cannavaro wabadili kikosi
Yanga itakayoshuka uwanja wa Olimpiki leo itakuwa na mabadiliko kidogo na ile iliyocheza mchezo wa awali ambayo yanatokana na mazoezi ya juzi kikosi hicho ni wazi kitakosa huduma ya Haruna Niyonzima aliyeachwa Dar es Salaam kufuatia kuugua malaria huku nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro akirudi.
Kuugua kwa Niyonzima ni wazi kutamrudisha kiungo Salum Telela aliyekosa mechi ya kwanza dhidi ya Etoile, akicheza mbele ya Said Makapu, Cannavaro aliyefunga bao la timu yake kabla ya kutolewa akiwa majeruhi akitarajiwa kuanza, akimrudisha Mbuyu Twite kulia, huku Juma Abdul akitarajiwa kuchezeshwa mbele yake, yaani kiungo wa pembeni kulia.
Manji atuma ujumbe mzito
Wakati kikosi cha Yanga kikipata kifungua kinywa jana asubuhi, walipokea ujumbe mzito kutoka kwa mwenyemkiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji akiwatakia kila la heri akitaka watambue kwamba Yanga inajivunia kuwa na wachezaji wa aina hiyo. Barua hiyo gazeti limepewa nakala yake.
No comments:
Post a Comment