Mwanza. Wafanyakazi jana walimsomea Rais Jakaya Kiwete madai 11
wanayomtaka awatimizie kabla ya kumaliza muda wake Oktoba, lakini mkuu
huyo wa nchi amesema ataishia pale atakapoweza na kumuachia mrithi wake
kazi ya kushughulikia mengine.
Kauli hiyo aliitoa
wakati akihutubia kwenye sherehe za Siku ya wafanyakazi Duniani
zilizofanyika kitaifa mkoani hapa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Rais
alikuwa akijibu hoja kadhaa zilizokuwapo kwenye risala ya Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi (Tucta)iliyosomwa na katibu wake mkuu, Nicholaus
Mgaya ambayo ilitaja madaio hayo, yakiwamo ya kuongeza kima cha chini
cha mshahara hadi kufikia Sh315,000, kupunguza kodi ya malipo kadri
unavyopata na kuundwa kwa Tume ya Usuluhishi.
“Tuna
madai 11 ambayo ni kima cha chini cha mishahara, maboresho ya pensheni,
makato ya kodi, Tume ya Usuluhishi ambayo bado ina changamoto kubwa
kwani sheria inasema suluhisho kati ya mwajiri na wafanyakazi linatakiwa
kufanyiwa kazi ndani ya siku 30, lakini kwa sasa inafikia mwaka mmoja,
na uhuru wa kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi na mengine ambayo ni
changamoto kwa wafanyakazi. Tunaomba utusaidie kuyatafutia ufumbuzi,”
alisema Mgaya katika risala hiyo.
Lakini, Rais Kikwete,
ambaye jana alizungumza akichanganya na utani, alisema changamoto za
wafanyakazi amezikuta na haziwezi kumalizika, hivyo anamwachia Rais
ajaye azishughulikie.
“(Rais wa Serikali ya Awamu ya
Kwanza) Mwalimu Julius Nyerere kwa miaka 27 alishindwa kuzimaliza
(changamoto za wafanyakazi). Rais wa awamu ya Pili, All Hassan Mwinyi
hakuzimaliza, Rais wa awamu tatu Benjamini Mkapa hakuzimaliza, na mimi
siwezi kuzimaliza. Hivyo zitakazobaki nikitoka madarakani, ninamwachia
Rais ajaye azishughulike,” alisema Kikwete.
Wakati wa
utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, wafanyakazi walikuwa
wakitarajia kusikia nyongeza ya mishahara kutoka kwa Rais kwenye sherehe
za Mei Mosi, lakini Mkapa akaondoa utamaduni huo baada ya kueleza
waziwazi kwenye moja ya sherehe hizo kuwa Serikali itaongeza mshahara
kama watu watachapa kazi.
Kikwete alitumia muda mwingi
wa hotuba yake kuaga na akaeleza kuwa hana mpango wa kuongeza muda kama
baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
“Nawashangaa wanaodai
kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza muda wa urais, kwani sina mpango wa
kufanya hivyo,” aliongeza Kikwete ambaye aliingia Ikulu mwaka 2010 kwa
ushindi wa zaidi ya asilimia 80. .
“Kwanza naomba
niwashukuru wafanyakazi wote kwa kukutana tena Mwanza. Wakati naanza
urais mwaka 2006 sherehe zangu za kwanza za Mei Mosi zilifanyika Mwanza,
na furaha kubwa sherehe za mwisho tena nafanyia Mwanza. Katika kipindi
changu cha uongozi nimefanya mambo mengi kushugulikia changamoto za
wafanyakazi.”
Bango la walimu lamkuna JK
Rais
pia hakusita kueleza jinsi alivyokunwa na ujumbe uliokuwa umeandikwa
kwenye mabango ya vikundi kadhaa vilivyopita mbele yake mwanzoni mwa
sherehe hizo, hasa bango la walimu lililokuwa na ujumbe usemao “shemeji
unatuachaje”.
“Nimesoma ujumbe wenu kupitia mabango.
Niwaambie kwamba ujumbe umefika na yote nitayafanyia kazi… hata ule wa
shemeji zangu pia,” alisema Rais Kikwete huku akicheka na kuingiza utani
akisema “kuoa mwalimu kazi”.
Akizungumzia suala la
kupunguza kodi kwa mishahara ya watumishi wa umma kutoka asilimia 12,
hadi tisa, Rais Kikwete alisema ataliangalia suala hilo hata kama
haitafikia asilimia hiyo mrithi wake anaweza kufikia huko.
Madai ya walimu
Akizunguzmia
madai ya walimu na wauguzi kuhusu malipo ya stahiki zao, Rais Kikwete
alisema Serikali imeanza kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu na
kwamba tayari kuna baadhi wameshanza kulipwa.
Kauli mbiu ya Mei Mosi
Kuhusu
kauli mbiu ya Mei Mosi mwaka huu, Rais Kikwete alisema kuwa kauli mbiu
hiyo ni sahii kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu na kwamba wafanyakazi
wajitokeze kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili waweze
kuchagua kiongozi wanaomtaka na kupata nafasi ya kuipigia kura Katiba
Inayopendekezwa.
“Mfanyakazi kajiandikishe, kura yako
ina thamani kwa maendeleo yetu. Hii ni kaulimbiu sahii kwa kipindi hiki.
Mkijiandikisha mtaweza kupiga kura na kuchagua madiwani, wabunge na
Rais ambaye atawatetea,” alisema.
“Mtambue kuwa
kitambulisho cha zamani hakitatumika tena kupigia kura, hivyo mjitokeze
kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura,” alisema Rais Kikwete.
Vibali vya ajira kwa wageni
Kuhusu
ongezeko la utoaji holela wa vibali vya kazi kwa wageni, Rais alimtaka
Waziri wa Kazi na Ajira kuandaa kanuni zitakazoratibu utekelezwaji wa
sheria mpya ya vibali vya ajira ili ianze kufanya kazi haraka
iwezekanavyo.
Alisema tayari Bunge limeshapitisha
sheria hiyo itakayoangalia kwa kina vibali vya ajira kwa raia wa kigeni
na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza utekelezaji.
“Kumekuwepo
na malalamiko kadhaa kuhusu wageni wanaokuja kufanya kazi katika sekta
mbalimbali nchini, hasa katika maeneo ambayo hata Watanzania wana ujuzi
nayo. Tumeliona hilo tayari limeshatungiwa sheria kinachosuburiwa kwa
sasa ni kanuni ili utekelezaji wake uanze mapema iwezekanavyo”alisema
Rais
pia alizungumzia changamoto ya mawakala wa ajira na kuwalezea kuwa
baadhi yao wamekuwa kiini cha kuwakandamiza wafanyakazi, hali
inayosababisha kukosa stahili zao za msingi.
Alisema
Serikali haitasita kuwachukulia hatua stahiki mawakala wa ajira
wanaokiuka sheria za kazi na ajira ikiwa ni pamoja na kujivika joho la
waajiri na kukodisha wafanyakazi kwenye makampuni.
Kikwete aibukia kwenye Bongo Fleva:
Rais
Kikwete pia hakusita kuburudisha wananchi waliohudhuria sherehe hizo
baada ya kujisifu kuwa ana kipaji cha uimbaji alichokionyesha kwa kuimba
sehemu ya wimbo wa bendi ya Orchestra Safari Sound wa “Mimi Msafiri”,
akisema kama asingekuwa Rais, angeweza kuwa msanii wa muziki wa kizazi
kipya.
Kama vile anaelezea maisha yake yataendelea hata
baada ya kuondoka Ikulu, Rais aliimba kipande cha wimbo huo kisemacho
“Mimi msafiri msafiri bado nipo njiani, sijui lini nitafika”.
“Nafikiri
nisingekuwa rais ningekuwa msanii wa bongo fleva kwani sauti yangu sio
mbaya sana japo siwezi kuwashinda wasanii kama Ali Kiba na
Diamond,”alisema Kikwete Wimbo huo ulitungwa na kuimbwa na mwimbaji
nguli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kikumbi Mwanza, maarufu
kwa jina la King Kiki, ambaye pia ametunga wimbo unaomsifu Kikwete.
Ujumbe wa Tucta
Akizungumza
kwenye sherehe hizo katibu mkuu wa Tucta alisema kuwa kabla Rais
hajamaliza muda wake, wanatarajia kuwa ataendelea kuwahimiza waajiri wa
sekta ya umma wawalipe wafanyakazi wao kima cha chini walichopendekeza
mwaka 2006 ambacho ni Sh315,000.
Pia alisema wanaomba
kodi wanayokatwa wafanyakazi ipunguzwe hadi kufikia asilimia tisa
pamoja na kuridhia mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO).
“Bado
kuna changamoto kubwa kwa wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi,
lakini tunatarajia kabla hujamaliza muda wako utatusaidia kupunguza kodi
hadi kufikia asilimia tisa, kuridhiwa kwa mikataba ya Hifadhi ya Uzazi
namba 183 na mkataba wa 155,” alisema Mgaya.
Hali ilivyokuwa
Baadhi
ya washiriki wa sherehe hizo za Mei Mosi zilizofanyika Uwanja wa CCM
Kirumba walizuiliwa kuingia uwanjani kutokana ujumbe wa mabango yao.
Washiriki
hao walisababisha mshangao kwa wananchi waliokuwa wamehudhuria sherehe
hizo kutokana na ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye mabango waliyobeba.
Baadhi
ya mabango hayo ni pamoja na ujumbe wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo
vya Elimu ya Juu, wamachinga yaliyokuwa na ujumbe unaosomeka “Katiba
Pendekezwa ni Haki ya Kila Mmoja , Isome na Uielewa na Uipigie Kura ya
Ndio, Akili za Kuambiwa Changanya na Zako”.
Dodoma
Mkoani Dodoma, Tucta iliishambulia Serikali kwa kitendo chake
cha kuwalipa mishahara midogo ambayo ni sawa na posho ya siku moja kwa
baadhi ya viongozi wa Serikali na taasisi zake.
Akisoma
risala ya mkoa katika maadhimisho yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri,
mratibu wa Tucta, Ramadhan Mwendwa alisema: “Kipato cha ujira wa
mishahara wa mwezi tunacholipwa wafanyakazi hakiridhishi kabisa kwa
sababu ujira huo ni sawa na posho ya siku moja ya kikao cha baadhi ya
viongozi wa serikali na taasisi zake.”
Huku
akishangiliwa na wafanyakazi, alisema malipo hayo kidogo athari yake ni
kukosekana kwa tija kazini kwani wafanyakazi hutumia muda wa kazi
kutafuta njia nyingine ya kujiongezea kipato.
Alisema wafanyakazi wengi hutumia mishahara yao kwa sijy saba tu.
“Wafanyakazi
tunaamini kuwa serikali ina uwezo wa kulipa kiwango hicho cha mishahara
tulichopendekeza cha Sh315,000 kutokana na rasilimali tulizonazo kama
kama ipo dhamira ya dhati,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Chiku Gallawa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wafanyakazi
kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake kufanya kazi kwa bidii, kuwa
wabunifu na waadilifu ili kuongeza tija.
Geita.
Mkoani
Geita, Tucta iliitaka serikali kutatua kero za wafanyakazi yakiwemo
madeni ya watumishi, kuimarishwa kwa vikao vya mabaraza ya wafanyakazi
na kudhibiti upandaji wa bei za bidhaa.
Akizungumza
kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kalangalala, mratibu wa shirikisho
hilo, James Kimola alisema endapo changamoto hizo hazitatatuliwa,
shirikisho litaishtaki mahakamani serikali ya mkoa.
Kimola
alisema moja ya maeneo yanayosumbua wafanyakazi ni mabaraza ya
wafanyakzi kuchukuliwa kama jambo la dharula na lisilokuwa na umuhimu
wowote, kutokana na mabaraza hayo kutoitishwa na wakurugenzi karibu
halmshauri zote, na yanapoitishwa wajumbe hawalipwi stahili za vikao
hivyo.
Alisema kutoitishwa kwa mabaraza hayo ambayo ni
chombo cha muhimu cha kumshauri mwajiri, kumesababisha wafanyakazi
kushindwa kujadili changamoto zinazowakabili.
“Wafanyakazi
kutolipwa fedha za uhamisho wanapopewa uhamisho, hususani walimu,
baadhi yao wanapodai gharama za uhamisho huambulia vitisho na hata
hufunguliwa mashtaka ya kusingiziwa. Hali hii haiwezi kuvumiliwa hata
kidogo. Tunaomba serikali ichukue hatua madhubuti kwa waajiri
wanaoendelea kuwahamisha watumishi huku wakijua hawana fedha,” alisema
Kimalo.
Ruvuma
Mkoani Ruvuma, mkuu wa
mkoa, Said Mwambungu amesema Serikali haitawafumbia macho waajiri
wanaowatoa vitisho, lugha chafu na masimango yasiyokuwa na ukomo kwa
watumishi wao kwa kuwa ni unyanyasaji.
Akizungumza
kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Mwambungu alisema waajiri na
waajiriwa wanapaswa kuheshimiana badala ya kutoleana vitisho ambavyo
havina tija.
Alisema, waajiri watambue na kukubali kuwa
ufanisi katika sehemu za kazi hutegemea uhusiano mzuri uliopo kati ya
mwajiri na mwajiriwa, hivyo lugha za mwajiri zinapaswa kuwa nzuri kwa
wafanyakazi wao.
Tanga
Wafanyakazi wa
Mkoani Tanga jana waliadhimisha siku ya Mei Mosi kwa kuiomba Serikali
kufanyia kazi ipasavyo changamoto iliyopo ya viwanda muhimu kufa au
kuhamishiwa nje ya nchi na mikoa mingine.
Mratibu wa
mkoa, Ahmed Ngereza alisema jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini hapa
kuwa kufa kwa viwanda muhimu vilivyokuwa vikitoa ajira kwa idadi kubwa
ya wakazi wa Tanga na vingine kuhamishiwa mikoa mingine kumeathiri
maisha ya wakazi.
Alisema licha ya kwamba jitihada
zimeanza kuchukuliwa kwa kuandaa maeneo na kulipa fidia kwa waliotakiwa
kupisha ujenzi wa Bandari ya tanga, bado kuna kusuasua.
Kilimanjaro
Mkoani
Kilimanjaro, Tucta imewataka waajiri kuboresha mazingira ya watumishi
ili waweze kuondokana na hali duni ya maisha inayosababisha kuwa
wajasiriamali na hivyo ufanisi kupungua.
Kaimu
Mwenyekiti wa Tucta mkoani Kilimanjaro, Alan Mbwambo alisema kwenye
sherehe za Mei Mosi zilizofanyika Uwanja vya Ushirika, kuwa mishahara
duni imesababisha wafanyakazi wengi kufanya shughuli za kujipatia fedha
tofauti na ajira zao.
“Kilio kikubwa kwa wafanyakazi ni
mishahara midogo ni vyema waajiri wangeongeza viwango vya mishahara kwa
wafanyakazi, ili waweze kuondokana na hali duni za maisha,” alisema
Mbwambo.
Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro amewataka Watanzania kuacha tabia ya kuukumbatia uduni na
ukabila kwani kufanya hivyo kutaliingiza Taifa katika vita isiyokuwa
na tija.
Akihutubia katika sherehe za Mei Mosi
zilizofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, alisema hivi sasa
kuna viashiria vya ukabila na udini, jambo ambalo alisema ni hatari kwa
mustakabali wa Taifa na kutaka kila mmoja kuheshimu dini na imani ya
mwenzake.
“Tuheshimiane, udini tusiukumbatie, ukabila
hauna nafasi katika dunia ya leo. Masuala ya ukabila yanahusiana na
matambiko tu lakini sio kuingiza katika jamii hivyo tusithubutu
kuligawana Taifa kwa misingi ya udini na ukabila kwani hivyo
vilishapitwa na wakati,” alisema Kandoro.
Awali, risala
ya Tucta iliyosomwa na katibu wa Tamico, Tabia Mwanjetile iliilaimikia
Serikali kwamba watumishi wamekuwa wakitozwa kodi kubwa katika
mishahara yao huku ikiwaachia wafanyabiashara ambao wamekuwa vinara wa
kukwepa kulipa kodi.
Dar es Salaam
Sherehe
za Mkoa wa Dar es Salaam zilizofanyika, Uwanja wa Uhuru, Mratibu wa Mei
Mosi, Mkoa wa Dar es Salaam, Charles Ngasha alitaja maombi yao kwa sasa
kuwa ni nyongeza ya kipato cha mshahara kutoka makadirio ya chini ya
Sh100,000-150,000 hadi Sh720,000 kutokana na mazingira ya hali ya uchumi
kwa sasa.
“Lakini pia, tunaomba Sheria ya Ajira
iwalazimishe waajiri kutambua vyama vya wafanyakazi katika ofisi za
mashirika na kampuni binafsi. Wafanyakazi wanaopandishwa vyeo
waharakishiwe kuongezwa mishahara, malipo ya madeni ya likizo, uhamisho
na changamoto za walimu zishughulikiwe,” alisema Ngasha.
Akijibu
madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alikiri
madai hayo kuwa ya msingi na kwamba atamfikia rais ambaye ni mkuu wa
nchi ili aweze kuyashughulikia.
Katika hatua nyingine,
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ameamua
kuichongea CCM kwa wafanyakazi, akidai kwamba chama hicho tawala
kinawakandamiza kwa kuwabebesha mzigo wa kodi na kwamba kinajali maslahi
ya wafanyabiashara wakubwa.
Alisema licha ya asili ya
CCM kuwa inatokana na harakati za wafanyakazi na wakulima wadogo kama
bendera yake inavyoonyesha nyundo na jembe, chama hicho kimewatelekeza.
“Hivyo
ni aibu kwa chama kilichoasisiwa na wafanyakazi leo kinaongoza kwa
kunyonya wafanyakazi kwa kodi kubwa kuliko nchi yoyote Afrika
Mashariki,” alisema.
Aliwashauri wafanyakazi waiombe
CCM iondoe alama ya nyundo kwenye bendera yake kwa kuwa ni kejeli
kwao,kwani chama hicho kwa sasa kipo kwa maslahi ya wafanyabishara
wakubwa.
“Hao ndio wanafaidi uchumi kwa misamaha ya
kodi na ukwepaji mkubwa. Ni maoni yangu kwamba kodi ya mshahara inapaswa
kushuka kwa 50, itoke asilimia 18 hadi 9% wastani wa kuanzia,” alisema
Kafilila.
Sharon Sauwa, Elizabeth EdwardSalum Maige,
Kelvin Matandiko, Joyce Joliga, Buruhan Yakub, Fina Lyimo, Albert Msole
Hadija Jumanne, Aidan Mhando Justa Mussa na Beatrice Mosses na Ngollo
John.
No comments:
Post a Comment