Ukawa, CCM wakabana koo bungeni - LEKULE

Breaking

14 May 2015

Ukawa, CCM wakabana koo bungeni


Dodoma. Mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2015/16 katika kikao cha pili cha mkutano wa 20 wa Bunge la 10, umetekwa na kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao, huku wabunge kutoka vyama vya upinzani wakihakikisha wanatumia neno “Serikali imechoka” kila wanaposimama kuchangia, huku wa CCM wakiitetea na kutamba kuibuka na ushindi wa kishindo.
Hotuba hiyo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda iliyozungumzia mafanikio katika kipindi cha miaka 10, ni ya kwanza kwa Bunge la Bajeti ambalo litahitimisha shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria cha Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya Uchaguzi Mkuu ambao kikatiba unatakiwa ufanyike wiki ya mwisho ya Oktoba.
Hali hiyo ya kumalizika kwa muda wa Serikali ya Awamu ya Nne ilijionyesha dhahiri kwenye michango ya wabunge, kiasi kwamba kila hoja ya kutetea au kubeza mafanikio ilichagizwa na maneno ya kuponda upinzani au kuiponda Serikali kuwa imechoka, neno lililotumiwa kwa mara ya kwanza juzi na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Katika kujadili hotuba hiyo jana, kati ya wabunge 22 waliochangia mjadala wa bajeti ya ofisi hiyo hadi jana mchana, 12 walijikita zaidi katika kujipigia kampeni wao na vyama vyao, hususan CCM na Ukawa, pamoja na kuwapiga vijembe wenzao kutoka vyama vingine.
Wengine 10 walichangia bajeti hiyo huku ‘wakichomeka’ masuala ya uchaguzi huo wa Oktoba na kutaka Serikali itekeleze ahadi ilizotoa katika majimbo yao.
“Bunge limeanza vibaya kutokana na wabunge kuanza kushambuliana,” alisema mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alipoulizwa kuhusu mwenendo huo wa mjadala.
“Wabunge warudi kwenye bajeti, waache kujadili watu na vyama,” alisema Nassari.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk Pudensiana Kikwembe alisema, “Wabunge wanataka kujihami na majimbo yao lakini watu watapima ni maendeleo gani yamefanyika katika kipindi cha uongozi wa wao.”
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses  Machali alikuwa na kauli kama hiyo alipofuatwa nje ya Bunge kuzungumzia mwenendo wa mmjadala.
“Sidhani kama ni sahihi (kujikita kwenye kampeni),” alisema Machali ambaye alikiri kuwa mabunge mengi hutawaliwa na hali kama hiyo wakati uchaguzi unapokaribia. “Tunachotakiwa kufanya ni kuzungumza mambo ambayo yanahusu bajeti hii ili kuweza kuishauri serikali mambo ya msingi ya kuzingatia.”
Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi alionya kuwa hali hiyo haiwezi kubadilisha kitu kwa kuwa uchaguzi lazima upo.
“Hakuna sababu ya kuendelea kupiga kelele kuhusu uchaguzi kwa sababu uko pale pale kwa mujibu wa Katiba,” alisema Arfi.
Mjadala huo ulitawaliwa na vijembe, mifano ya kuchekesha na hoja za nguvu zilizoishia kwa kupondana kisiasa na kushauri wananchi wasiipe tena fursa CCM kuongoza nchi, huku wabunge wa chama hicho tawala wakiponda kuwa wapinzani hawataambulia kitu.
Mjadala
Mjadala huo jana ulianza kwa mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba kuiponda Ukawa kuwa ndiyo dhaifu kwa sababu imeundwa na vyama vinne ili kuking’oa chama kimoja, jambo ambalo alisema haliwezi kufanikiwa.
“Huwezi kwenda Ikulu wakati hujashinda uchaguzi wa serikali za mitaa. CCM imeshinda kwa asilimia 70. Huwezi kupewa nchi wakati hujui maendeleo yaliyopatikana kwa miaka 50 tangu nchi ipate uhuru,” alisema Nkumba huku akiponda kuwa kauli za wapinzani kuwa Rais Jakaya Kikwete atajiongezea muda inaonyesha jinsi walivyo na hofu.

Paulina Gekul

Mbunge wa viti maalum (Chadema), Pauline Gekul alisema wapinzani wanavyosema serikali imechoka wana maana kuwa viongozi wa Serikali wamechoka kufikiri, hawawezi tena kuongoza na wanatakiwa kupumzika.

Gekul alitaja mambo saba ambayo CCM itakumbukwa kuwa ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na wakulima, wanakijiji na hifadhi za utalii; mauaji ya albino, unyanyasaji katika Operesheni Tokomeza, utengaji wa bajeti hewa za maendeleo, kushindwa kutengeneza fursa za ajira kwa vijana, kulimbikiza madeni ya wakulima na kutopima vijiji licha ya nchi kupata uhuru miaka 50 iliyopita.

“Msiibeze Ukawa, maana Watanzania wanajua wanachotaka. Tunaposema Serikali imechoka mnaruka tu katika viti. Tunamaanisha kuwa mmechoka kiakili, si kimwili,” alisema.

Mbunge huyo alisema kuwa kitendo cha Serikali kupeleka Tamisemi asilimia 17 ya fedha zilizotengwa kwa wizara hiyo, kinaonyesha ni kwa jinsi gani Serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake.

Mchungaji Msigwa

Mjadala huo ulifikia hatua ya uongozi wa Serikali kuelezewa kuwa ni dhaifu kiasi cha kuhatarisha hata usalama wa taifa.

“Heri mhalifu kuliko kiongozi dhaifu,” alisema mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Mbunge huyo alisema namba moja wa Usalama wa Taifa nchini ni Serikali ya CCM na ili Taifa liwe salama lazima kuing’oa madarakani. “Hii Serikali ya ajabu kabisa imechoka na tutaendelea kusema tu. Taifa hili ni kubwa kuliko kitu chochote, mnabadilisha mawaziri lakini kila siku mambo ni yaleyale ndio maana tunasema mmechoka.  Wananchi wajiandikishe katika Daftari la Wapigakura ili kukiondoa chama hiki,” alisema Msigwa.

 Mchungaji Msigwa alisema haiwezekani ndani ya mwaka mmoja Serikali ikataka kufanya mambo makubwa mengi wakati haina fedha, akitaja mambo hayo kuwa ni kusimamia Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitambulisho vya Taifa na kuendesha Kura ya Maoni.

Livingistone Lusinde

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliamua kujibu mapigo akitumia muda wake kumrushia madongo Msigwa na kuuponda Ukawa.

“Msigwa anashangaa Deni la Taifa kupaa sasa mbona wabunge hapa tunakopa, kipi cha ajabu. Uchaguzi Mkuu ukisogezwa mbele nchi haiwezi kulipuka kama wanavyosema Ukawa, mbona alivyokufa Rajab Jumbe (mgombea mwenza wa Chadema 2005) uchaguzi ulisogezwa mbele na nchi haikulipuka,” alisema Lusinde.

Assumpter Mshama

Mbunge wa Nkenge (CCM), Assumpter Mshama alijikita zaidi katika mifano ya mambo yaliyofanywa na serikali ya Awamu ya Nne huku akiwaponda wapinzani kuwa wanazungumza mambo wasiyoyajua.

Hamad Rashid Mohamed

Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alilitangazia Bunge kuwa hatagombea tena ubunge, badala yake atagombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ADC.

No comments: