RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeibua ufisadi mkubwa katika mamlaka za Serikali za mitaa,mashirika ya umma na serikali kuu.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa ripoti ya ukaguzi mjini Dodoma jana,Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alisema ukaguzi huo umefanywa katika taasisi 176 za Serikali kuu, halmashauri 163 na mashirika ya umma 109.
Alisema usimamizi wa bajeti kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa ulibaini kuwapo upungufu wa fedha za maendeleo Sh bilioni 312. 04, Serikali kuu Sh bilioni 1.8, fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo hazikutumika lakini hazikutolewa ni Sh bilioni 417.
Fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo hazikutumika ni Sh 203.13, alisema.
Alisema ripoti hiyo imebaini ukiukwaji wa matumizi ya utoaji wa misamaha ya kodi, kuendelea kwa mishahara hewa, usimamizi mbovu wa mipango miji,madeni ya Serikali katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Kuhusu misamaha ya kodi, Profesa Assad alisema iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini imefikia Sh bilioni 22.33 kati ya yale yaliyotakiwa kutumiwa na makampuni ya Geita Gold Mine na Resolute Tanzania Ltd na yalipelekamafuta hayo kwa wakandarasi wasiostahili msamaha wa kodi.
“Matumizi ya misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yasiyokusudiwa na kusababisha upotevu wa Sh milioni 392.7, iliyosababishwa na Kampuni ya Kiliwarrior Expenditions Ltd. ya Arusha iliyokuwa imesamehewa kodi ya Sh milioni 465.2 kuingiza magari 28 ambako kati ya Sh milioni 465.23, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeambulia kukusanya Sh milioni 72.5.
“Misamaha ya kodi ya Sh milioni 53.4 ilitolewa kwa Kampuni ya Kilemakyao Mountain Lodge Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi wa hoteli katika Kijiji cha Changarawe wilayani Meatu. Kampuni hii iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha wa kodi wa gari moja ya Hyundai Santa.Magari mengine ni BMW X5 na Toyota Land Cruiser Prado hayakufahamika yalipo,” alisema.
Alisema amebaini kudorora kwa uwekezaji wa Serikali kwenye makampuni mbalimbali ambako Serikali ina hisa kutokana na kuchelewa kuongeza mtaji, wakati inapohitajika kufanya hivyo kama ambavyo inataka kutokea katika benki ya NBC Ltd.
Mashirika ambayo yamegubikwa na kusuasua kwa usimamizi wa uwekezaji wa Serikali ni pamoja na Shirika la Ndege Tanzania (ATC),Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambayo yote yanahitaji ruzuku kutoka serikalini.
Mashine za EFD’s
Katika ukaguzi wa malipo, CAG amebaini kampuni binafsi hazitumii mashine za elektroniki za kutolea stakabadhi na hivyo kusababisha Sh bilioni 4.4 kutokuwa na stakabadhi hizo wakati taasisi za Serikali zimefanya malipo yenye thamani ya Sh bilioni 4.6 bila kutumia mashine hizo, mbali na halmashauri 22.
“Katika suala hili, TRA ilitoza faini ya Sh milioni 440.8 kwa wafanyabiashara walioshindwa kutumia EFD’s ambako milioni Sh 72 zililipwa na hivyo kufanya bakaa ya Sh milioni 369 ambayo haikulipwa,” alisema Profesa Assad.
Mapato ya ndani
Ukaguzi wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 2014, ulibaini taasisi zilizo katika mpango wa kubakiza maduhuli na hazikurejeshwa zilikuwa Sh bilioni 32.74, hivyo kuathiri utekelezaji wa kazi zilizokuwa zimepangwa na taasisi husika.
Mishahara hewa
Ukaguzi wa CAG umebaini wafanyakazi walioacha kazi na kustaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao, licha ya Serikali kuwekeza katika mfumo wa Lawson kama njia ya kudhibiti hali hiyo.
Pia fedha za makato ya mishahara yao zimeendelea kupelekwa kwenye taasisi kama vile Bima ya Afya, TRA na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kutokana na hali hiyo mpaka sasa fedha zilizolipwa ni Sh milioni 141.4.
Alisema katika halmashauri 36, Sh bilioni 1.01 zililipwa kwa watumishi waliotoroka kazini.
Wizara ya ujenzi
Ripoti hiyo imeitaja Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na Waziri Dk.John Magufuli kuwa inaongoza kwa kudaiwa na wakandarasi.
Alisema mpaka anatoa ripoti hiyo wizara hiyo inadaiwa Sh bilioni 800.
Lakini jambo la kushangaza wizara hiyo pia imetumia Sh bilioni 250 nje ya bajeti husika.
UKAGUZI WA MIRADI
Alisema ukaguzi wa miradi ya maendeleo mwaka 2013/14 ulihusu miradi mikubwa mitano.
Miradi hiyo ni Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP), Mfuko wa Afya (HBF), Mfuko wa Barabara (RF), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na miradi mingine ambayo inatekelezwa wizara, idara na mashirika ya umma.
“Katika ukaguzi wa hesabu za halmashauri 162, tulibaini Sh 52.7 zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hakikutolewa hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa.
“Hii imechangia malipo yaliyocheleweshwa kulipwa mwaka wa fedha 2013/14,” alisema.
Alisema ukaguzi ulibainia fedha zilizotolewa na kutotumika ndani ya mwaka wa fedha 2013/14, ni Sh bilioni 495.9 ikiwa ni asilimia 25.45 ya fedha zote za miradi.
“Sababu kubwa ya bakaa hii ni pamoja na ucheleweshaji wa kutoa fedha kwa wadau wa maendeleo na mchango wa Serikali, mchakato mrefu wa taratibu za ununuzi, uwezo mdogo wa halmashauri wa kutumia fedha za miradi na wafanyakazi wachache wenye utaalamu katika kusimamia fedha za miradi.
Ocean Road
Alisema Taasisi ya Ocean Road inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wa kansa.
“Mahitaji halisi ni mashine 36, wakati zilizopo ni mashine 11 tu ambazo kati ya hizo, mashine tatu zimeshapitwa na wakati zinangoja kuondolewa na mashine nne zinahitaji kufanyiwa ukarabati.
“Hali hiyo inasababisha ucheleweshaji wa matibabu hususan mionzi kwa wagonjwa ambako humchukua mgonjwa zaidi ya miezi mitatu kutibiwa wakati viwango vinavyokubalika kimatibabu ni chini ya wiki mbili,” alisema.
Aliishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la vifaa katika taasisi hiyo.
Mipango Miji
Alisema ripoti yake imethibitisha halmashauri 148 ambazo ni asilimia 80 zinaendelezwa bila kuwa na mipango kabambe inayoweza kutoa miongozo wa shughuli zote za uendelezaji wa miji nchini.
“Halmashauri 96 au asilimia 65 kati ya halmashauri 148, hazijawahi kuandaa mipango kabambe tangu zianzishwe,” alisema.
Alisema maeneo mengi yanaendelezwa bila kufuata mipango kabambe iliyopo.
Usambazaji dawa
Alisema kwa mujibu wa ukaguzi, imebainika tathmini ya makadirio ya uhitaji wa dawa na vifaa tiba muhimu katika vituo vya afya haufanyiki kwa uhakika.
Alisema hali hiyo inatokana na asilimia 50 ya ripoti zinazohitajika za makisio ya dawa za vifaa tiba muhimu kutoka halmashauri za wilaya kutowasilishwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kama inavyotakiwa.
“Imebainika asilimia 54 ya oda zinazopokelewa na MSD kutoka bohari za kanda ni kuanzia muda wa siku 14 kulingana na muongozo wa MSD.
“Hii imesababisha kutetereka kwa mtaji kushuka kwa zaidi ya asilimia 69 kutoka Sh bilioni 81 mwaka 2008 hadi Sh bilioni 25 mwaka 2013.
“Hii imechangiwa na ongezeko la deni la Serikali ambalo limeongezeka zaidi ya mara nne kutoka Sh bilioni 14 mwaka 2008 hadi Sh bilioni 69 mwaka 2014,” alisema CAG.
Kutokana na hali hiyo, CAG alipendekeza uboreshaji wa upatikanaji wa dawa na vifaa muhimu katika vituo vya huduma ya afya.
“Ninapendekeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na MSD kutathimini hali ya mtaji wa uendeshaji wa mfumo mzima wa makisio na usambazaji wa dawa na vifaa tiba muhimu kwa lengo la kutatua tatizo la uhaba wa dawa,” alisema.
Wastaafu,watumishi
Kuhusu wastaafu, ripoti yake imegundua Sh milioni 5.43 zimelipwa kama posho na pango kwa watumishi walioko ubalozini nje ya nchi.
“Hii ni kinyume na kanuni za kudumu za utumishi, fedha hizo zinazoendelea kulipwa kwa wastaafu hao ambao hawafanyi kazi si zingeweza kulipwa kwa wafanyakazi?” alihoji Profesa Assad.
Majengo ya Serikali
Alisema ukaguzi huo umebaini majengo mengi yanayomilikiwa na Wakala wa Majengo yalijengwa kwa zaidi ya miaka 25 iliyopita, hali inayosababisha majengo hayo kuwa katika hali isiyoridhisha.
“Ilibainika hakuna utaratibu madhubuti wa usimamizi wa ukarabati wa majengo ya Serikali, hii ni kwa kuwa mikoa mingi haifuati taratibu zilizopo za ukarabati wa majengo ya Serikali.
“Kati ya mikoa sita iliyotembelewa hakukuwa na mkoa hata mmoja ulioweza kufanya marekebisho ya viwango vilivyowekwa vya ukarabati wa majengo ya Serikali.
“Pia hakukuwa na nyaraka kama vile vitabu vya rejista vya kuweka kumbukumbu ya hali ya ukarabati wa majengo katika ofisi zao na pale ukarabati unapotekelezwa, hutekelezwa bila kuwa na mpango kazi uliowekwa,” alisema.
CAG alipendekeza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Majengo kuweka sera ya ukarabati wa majengo yanayomilikiwa na Serikali na kufuatilia utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi ya majengo hyo.
Mifumo ya uhifadhi
Alisema katika ukaguzi uliofanyika ilibainika mipango ya usimamizi wa mazingira iliyoandaliwa na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), haitilii mkazo suala la viashiria hatarishi.
“Ilibainika NEMC halikutoa adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 kwa makampuni mbalimbali ya migodi inapokiuka sheria hiyo.
“Na hata pale adhabu zinapotolewa hakukuwa na ufuatiliaji mzuri kuweza kubaini kama adhabu husika imetekelezwa ipasavyo,” alisema.
Alisema pia halmashauri hazifanyi ufuatiliaji wa shughuli katika migodi hali inayosababisha NEMC kushindwa kuwa na picha halisi juu ya utunzaji mazingira katika migodi nchini.
“Vilevile imebainika kuwa hakuna utaratibu wa shughuli za usimamizi wa mazingira migodini, NEMC ilishindwa kuratibu kwa ufanisi ushirikiano wa wadau mbalimbali katika usimamizi wa mazingira migodini,” alisema.
CAG amependekeza NEMC kutathmini utekelezaji wa mfumo ulipo pamoja na kuanzisha uandaaji wa taarifa itakayoonyesha hali ya mazingira katika sekta madini na kutoa adhabu stahiki kuzuia uvunjaji wa sheria kutojirudia.
Huduma za ugani
Alisema katika uchunguzi huo, Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika hawajasambaza kwa ukamilifu miongozo inayohusiana na utoaji wa huduma za ugani kwa maofisa ugani.
“Pia hakuna vitabu vya rejista na ratiba zinazoonyesha utendaji kazi wa maofisa ugani hali inayosababisha utekelezaji usioridhisha wa mipango na miradi ya mendeleo ya kilimo,” alisema.
Alisema ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo teknolojia duni za shughuli za ilimo, ucheleweshaji wa fedha na kusababisha huduma duni za ugani na ufuatiliaji na tathimini za utoaji wa huduma za ugani kutofanyika ipasavyo.
“Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika zifanye tathmini ya huduma ya ugani na kuangalia na jinsi gani hizo zinaweza kuboreshwa katika maeneo ya uandaaji wa mipango, uratibu, uwezeshaji, ufuatiliaji na utoaji wa mrejesho ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo,” alisema.
Kauli ya PAC
Akizungumzia ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau alisema inaonyesha mapato ya serikali bado yanapotea na kulitaka Bunge lijalo lipambane na hali hiyo.
“Kwa ujumla hali ni mbaya, kwa mfano Wizara ya Ujenzi ililidanganya Bunge lililopita, angalia Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania), wanaongoza kwa madeni. Lakini pia Kitengo cha Maafa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu kimetumia fedha vibaya na hili lazima tulishughulikie haraka” alisema Mwidau.
No comments:
Post a Comment