Jeshi la Polisi limekanusha madai ya polisi wa wilaya ya Bunda, wanaodai kulazimishwa kuchangia fedha kwa ajili ya mafuta ya kusafirisha mwili wa mwenzao aliyefariki dunia katika Hospitali ya rufaa Bugando kwenda nyumbani kwao katika wilaya ya Mahenge mkoani Morogoro.
Jeshi limetoa kauli hiyo baada ya kuwapo malalamiko katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bunda, ambako kulikuwa na umati mkubwa wa askari Polisi waliokuwa wamekusanyika, wakidai kupinga amri ya kulazimisha kuchanga fedha kwa ajili ya kusafirisha mwili wa mwenzao.
Baada ya mwandishi kusikiliza malalamiko ya polisi hao, alizungumza na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya (OCD), Gwisael, ambaye alikanusha kuhusu madai ya askari hao.
Alisema, mchango wanaotoa ni wa Sh 5,000 kama ilivyo kawaida na siyo za mafuta Sh 10,000, kama inavyodaiwa na baadhi ya askari.
Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Philipo Kalangi, alimwambia mwandishi kwamba, imetolewa gari na mafuta lita 220 kwa ajili ya kusafirisha mwili wa askari huyo, Koplo Mahamudu Magasa.
Kamanda Kalangi alisema ni marufuku kwa askari yeyote kuchangishwa mchango wa mafuta.
“Tayari nimeshatoa gari na mafuta lita 220 kwa ajili ya kusafirisha mwili wa askari huyo, na pia tunatoa na posho ya kujikimu kwa askari watakaosafirisha mwili wa marehemu, sasa ni nani kawaambia wachangie tena…sisi tuna utaratibu wetu wa serikali siyo kuchangisha askari fedha za mafuta,” alisema.
Hata hivyo, jana saa 7:52 mchana, mwandishi alishuhudia gari la Polisi lililotumwa na Kamanda wa Mkoa kutoka mjini Musoma, lenye namba za usajili DFP 1822 likiwa tayari liko kituoni hapo kusubiri kusafirisha kwa mwili wa marehemu.
Askari huyo, Mahamudu aliugua juzi na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza ambako alifariki dunia. Awali, askari waliokutwa kituo cha Polisi wakilalamikia kuchangishwa, walisema kitendo hicho ni sawa na kwamba serikali haithamini utumishi wao.
Walidai watumishi wa idara nyingine wanapofariki fedha hutolewa na serikali kwa ajili ya kusafirisha miili yao. “Iweje sisi tulazimishwe kuchangia,” alihoji mmoja wa askari.
Walisema kuwa wao siku zote wamekuwa wamejiwekea utaratibu, kwamba mwenzao anapofariki wanachangia mchango wa Sh 5,000 kila mmoja, zisaidie familia ya marehemu na siyo kuchangia mafuta ya kusafirisha mwili wa marehemu.
Hata hivyo, wakati polisi hao wakiwa wamekusanyika nje ya kituo hicho wakipinga hatua hiyo, maofisa wa jeshi hilo wilayani hapa wakiongozwa na Mkuu wa Polisi katika wilaya ya Bunda, walikuwa kwenye kikao cha pamoja.
No comments:
Post a Comment