Pinda: Siku za uandikishaji zitaongezwa majimboni - LEKULE

Breaking

17 May 2015

Pinda: Siku za uandikishaji zitaongezwa majimboni


Dodoma. Serikali imeiagiza Tume ya Uchaguzi (NEC) kuongeza siku za uandikishaji kwenye majimbo iwapo kutakuwa na watu ambao hawajapata nafasi ya kusajiliwa kwenye Daftari la Wapigakura katika muda uliopangwa. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo jana wakati akihitimisha mjadala wa hotuba ya makadirio na matumizi ya ofisi yake bungeni mjini Dodoma jana. NEC imepanga kutumia siku saba kwa kila jimbo kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Wapigakura, ingawa katika baadhi ya maeneo kazi hiyo inayofanywa kwa mfumo wa kielektroniki unaotambua alama za mpigakura (Biometric Voters Registration), imechukua siku nyingi zaidi.
“Uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa kielektoniki unaendelea vizuri na vituo vya kupigia kura nchi nzima vitakuwa 36,000,” alisema Waziri Pinda.
“Tumeieleza Tume kwamba iwapo muda huo utakwisha na kubainika kuwa wapo ambao hawajaandikishwa, waongeze muda ili kuwamaliza wote.”
Kasi ndogo ya uandikishaji wapigakura kwa kutumia mashine za BVR imesababisha wapinzani kuingiwa na hofu kuwa Uchaguzi Mkuu unaweza usifanyike mwishoni mwa Oktoba kama Katiba inavyoelekeza baada ya tatizo hilo kusababisha Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30 kuahirishwa kwa muda usiojulikana.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alisema siku 60 zinatosha kukamilisha zoezi la uandikishaji wa watu wote wenye sifa kwenye Daftari la Wapigakura. NEC inatarajia kuandikisha wapigakura milioni 23.
Akijikita kwa muda mrefu kujibu hoja zilizotolewa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mhagama alisema mashine 4,850 za BVR zimeingia na zinafanya kazi katika mikoa mbalimbali.
Pia, alisema kabla ya mwishoni mwa mwezi huu zitaingia mashine nyingine 3,150 ili kukamilisha idadi ya mashine 8,000 zilizopangwa kuletwa kwa ajili ya kazi hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura.
Alisema kazi hiyo mkoani Njombe imekamilika huku akisisitiza kuwa BVR moja ina uwezo wa kuandikisha watu 100 na kwa hiyo siku moja wataandikisha watu 800,000.
“Ninawaombeni viongozi wa vyama vya siasa muwe makini uchaguzi ni suala nyeti. Jambo lolote linaweza kusababisha maafa yasiyokuwa na maana,” alisema.
“Uchaguzi mkuu uko palepale hakuna kitakachobadilika. Serikali ya CCM imetimiza wajibu wake haina cha kuhofia kuingia katika uchaguzi na mimi naamini itashinda.”
Aliwataka wananchi kujitokeza na kujiandikisha kwa wingi ili waweze kutumia haki yao ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Bajeti yapita
Jana, pamoja na kuelezewa kuwa inaonyesha jinsi Serikali ilivyochoka, bajeti hiyo ya Sh5.8 milioni ilipitishwa bila ya matatizo makubwa. Hata hivyo, Halima Mdee, ambaye ni mbunge wa Kawe (Chadema), Moses Machali (Kasulu Mjini, NCCR), Ester Bulaya (viti maalumu, CCM), Ezekiah Wenje (Nyamagana, Chadema) na Susan Lyimo (viti maalumu–Chadema) walisimama kuhoji matumizi ya fedha kwenye baadhi ya vipengele.
Machali alihoji kuongezeka kwa fedha za kununua magari mawili ya viongozi, katika maelezo ya Serikali iliweka kiwango cha Sh380 milioni bila kueleza inanunua magari ya aina gani. Lakini Naibu Waziri Tamisemi, Aggrey Mwanri alifafanua kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kukunua magari aina ya Toyota VX.
Kwa upande wake, Lyimo alihoji kuongezeka kwa fedha za ukarimu mpaka kufikia Sh105 milioni na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia alijibu kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaongoza kwa kutembelewa na wageni, wakiwamo wabunge, hivyo ni lazima iwepo bajeti ya kuwanunulia vitafunwa kama korosho kila wanapotembelea ofisi hiyo.
Dar yatengewa Sh9.5 bilioni
Mdee aliibana Serikali akitaka itoe maelezo kuhusu ukarabati wa miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam kutokana na kuharibiwa na mafuriko.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kuwa wametoa Sh9.5 bilioni kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu hiyo, kwamba wameiagiza Hazina kuanza kwa kutoa Sh3 bilioni hadi nne. Alisema ili kufanikisha kazi hiyo kwa haraka, ujenzi wa miundombinu utasimamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Serikali imeiagiza Hazina kutoa Sh3 bilioni hadi nne ili kazi hiyo iweze kuanza mara moja kunusuru hali mbaya ya barabara na madaraja inayolikabili Jiji la Dar es Salaam. Nakubaliana na ushauri wa Mkuu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni (Freeman) Mbowe kwamba Dar es Salaam inahitaji kupangwa vizuri,” alisema Pinda huku akiwataka wananchi waishio mabondeni kuhamia maeneo waliyopewa na serikali.
Utekelezaji wa bajeti ya Serikali
Kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Serikali, Pinda alikiri kuwapo kwa changamoto kubwa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kutokana na baadhi ya wahisani kutotimiza ahadi zao.
“Naomba nikiri kwamba bajeti ya Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu haikutekelezwa kwa kiwango cha asilimia 30, upungufu huo uliathiri kwa kiasi kikubwa bajeti yetu. Tumeamua mwaka huu katika bajeti yetu tumejielekeza kukusanya mapato ya ndani ili kuondoa utegemezi,” alisema Pinda.
“Taratibu zipo kwani kila ahadi inayotolewa na kiongozi zinawekwa katika kumbukumbu na wakuu wa mikoa na kwa kiasi kikubwa ahadi zimetekelezwa, zile ambazo hazijatekelezwa zitatekelezwa. Ahadi ni deni na Serikali itakayokuja itazitekeleza.” 
Kukua kwa uchumi
Akizungumza kukua kwa uchumi, Pinda alisema wataalamu wa Benki ya Duni (WB) walifanya utafiti mwaka 2012 wa nchi 29 zinazokuwa kiuchumi na Tanzania ilishika nafasi ya 15 duniani. Alisema mwaka jana Kampuni ya KPMG Afrika ilifanya utafiti wa nchi kumi zinazokuwa kwa haraka kiuchumi, Tanzania ilishika nafasi ya sita.
Elimu
Kuhusu elimu, Pinda alikiri kuwa sekta hiyo ina changamoto nyingi  na lazima Serikali ipambane nazo, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu, kujenga maabara na kuhakikisha kuwa kuna walimu wa kutosha.
 Majimbo ya Uchaguzi
Kuhusu kuongezwa kwa majimbo ya uchaguzi, alisema sababu kubwa iliyotumika ni kuangalia wastani wa watu katika eneo husika, mawasiliano, hali ya jiografia, hali ya uchumi, ukubwa wa jimbo, mipaka ya kiutawala, jiombo moja kutokuwa ndani ya halmashauri au wilaya na mpangilio wa mipaka.

No comments: