Giza nene zaidi makada urais CCM - LEKULE

Breaking

17 May 2015

Giza nene zaidi makada urais CCM


Dar es Salaam. Hali bado ni tete kwa makada sita waliofungiwa na CCM kujihusisha na masuala ya uchaguzi baada ya chama hicho tawala kueleza kuwa mchakato wa kuwachunguza haujakamilika na adhabu yao inaweza kuendelea hata baada ya vikao vya juu vitakavyofanyika mwishoni mwa wiki.
CCM pia imebadili tarehe za vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ambavyo awali vilipangwa kufanyika Mei 20, 21 na 22 na badala yake sasa vitafanyika Mei 22,23 na 24.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za chama hicho jijini, Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hafahamu lini adhabu ya viongozi hao itakwisha kwani bado mchakato wa kuwachunguza haujafika mwisho.
“Nilisema mchakato unaweza kuchukua miezi mitano, wiki mbili, mwaka, au miaka na kama mchakato haujaisha bado wataendelea na adhabu yao,” alisema Nape. Nape alisema hata kikao cha mwishoni mwa wiki cha Kamati Kuu kinaweza kujadili au kutojadili, akifafanua kuwa madhumuni ya mkutano huo siyo kufunga wala kufungua kada yeyote kutoka katika kifungo chake bali ni kwa ajili ya mambo ya chama na Uchaguzi Mkuu. Nape alisema chama kinafuata kanuni ambazo zinasema mtu akiwa kwenye kifungo, haruhusiwi kugombea nafasi yoyote.
“Hiyo kanuni ipo na imetungwa hata kabla sijazaliwa hivyo nasisitiza ni kanuni na wala si mimi, nasisitiza pia kuwa sijazuia watu kuchukua fomu bali chama kinafuata kanuni,” alisema.
Alisema kada yeyote wa CCM akiamua kufanya kampeni kabla ya muda ataadhibiwa, lakini akisubiri hana hatia kwani kinachogomba ni kanuni.
Februari mwaka jana, Kamati Kuu ya CCM iliwafungia kwa miezi 12 vigogo wa chama hicho kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na kukiuka maadili ya chama.
Waliokumbwa na adhabu hiyo iliyotolewa Februari 12 mwaka jana baada ya kubainika kuanza kampeni mapema ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa Kilimo na Chakula), January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia) na William Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema.
Kati yao, tayari Wasira ameshatangaza nia yake ya kugombea urais wakati Lowassa amepanga kutangaza kuanza ‘safari ya matumaini’ mwishoni mwa wiki mjini Arusha.
“Chama hakiwezi kuacha watu watangaze kiholela… wengine kuzimu, wengine mbinguni. Namna hii tutakiharibu chama,” alisema. Alisema kutangaza kama unagombea si vibaya, lakini matendo yanayoambatana na kauli yako ndiyo ambayo chama hakiyataki.
Alisema mchakato wa makada hao sita upo chini ya kamati ya nidhamu na huenda kikao cha Kamati Kuu ya CCM kikayazungumza mambo ya vigogo hao.
Kubadilika kwa ratiba ya NEC
Katika mkutano huo, Nape alieleza mabadiliko ya ratiba ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM na Kamati Kuu ambao utafanyika Mei 22, 23 na 24 badala ya Mei 20, 21 na 22 kama ilivyopangwa awali.
Nape alisema mabadiliko hayo yanatokana na mwingiliano wa ratiba ya Baraza la Wawakilishi na hiyo ndiyo sababu ya kusogezwa mbele kwa mikutano hiyo.
“Vikao vya maandalizi ya awali kwa ajili mkutano wa NEC na Kamati Kuu, vitaanza tarehe 18 hadi 21 na hivi vinafanya kazi ya kuandaa na kuthibitisha ajenda za vikao vikuu,” alisema.
Alisema ajenda muhimu katika mikutano hiyo ni pamoja na hali ya kisiasa nchini, maandalizi ya uchaguzi mkuu, mchakato wa namna ya kuwapata wagombea wa CCM na ratiba ya uchaguzi.
“CCM pia imekuwa na vikao vya maandalizi ya ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2015/2020 na vikao vinavyoendelea vitapewa taarifa ya tulipofikia. Wajumbe watapewa ruhusa ya kutoa maoni yao kwenye mapendekezo ya ilani hiyo,” alisema.
Nani mgombea wa CCM?
Akizungumzia kuhusu mchakato wa kumpata mgombea wa CCM, Nape alisema kuwa vikao vinavyoendelea vitatoa ratiba ya mwenendo wa atayewania nafasi hiyo ya urais.
Alisema vikao hivyo vitapanga tarehe ya kuchukua fomu, kuzunguka kutafuta wadhamini, kutengeneza kanuni za kuwapata wagombea na mambo mengine yanayohusu wagombea.
“Mengi yatazungumzwa katika vikao vile, tulikuwa pia na mazungumzo ya namna ya kuboresha kura za maoni na kanuni za kuwapata wagombea hao,” alisema.
Nape alisema utaratibu wa wagombea kupata wadhamini na idadi yao utajadiliwa kwenye kikao hicho.
Mbwembwe marufuku siku ya kuchukua fomu
Pamoja na vikao hivyo, Nape alisema wanaoutaka urais hawataruhusiwa kuwa na mashamsham ya aina yoyote bila kujali wadhifa na nafasi ya mtu serikalini.
Alisema upo utaratibu ambao umewekwa na chama wa kuwabana watu wenye nyadhifa kama waziri mkuu kusindikizwa na ving’ora au misafara ya magari ya Serikali wakati wakienda kuchukua fomu.
“Kuna utaratibu wa kuchukua fomu, hili jambo liliwahi kujadiliwa sana na likaleta mjadala ndiyo maana tukasema hata kama mgombea ni waziri, basi siku ya kuchukua fomu asifuate protokali za kiserikali kutokana na wadhifa wake,” alisema.
Alisema hata waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Cleopa Msuya, hawakusindikizwa na msafara wa magari ya Serikali wakati walipokwenda kuchukua fomu.
“Hatuwezi kufuata itifaki za kiserikali wakati wa kuchukua fomu. Vitu vingi tulivizuia,” alisema. Alisema chama kitaeleza kanuni nyingine kuhusu mchakato huo kwa mfano iwapo mgombea atakuja na waandishi wake siku ya kutangaza nia au waandishi watawekwa na chama.
Nape aijibu ‘safari ya matumaini’ ya Lowassa
Kuhusu taarifa ya Lowassa ya kutoa neno Mei 24 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kuzungumzia ‘safari ya matumaini’, Nape alisema:
“Lowassa ni mtu mzima, ana akili timamu na anafahamu sheria na kanuni, lakini mimi na yeye tutakutana kwenye Kamati Kuu.”
Juzi, mbunge huyo wa Monduli akiwa kwenye shughuli ya harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Patandi, Arusha alisema atatoa neno Mei 24.

No comments: