Wasomi na wachambuzi wa siasa wamesema Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete ameona mbali kuwataka viongozi wa chama hicho kuteua
mgombea wa urais anayekubalika ndani na nje ya chama wakisema bila
kufanya hivyo wataangushwa na mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
Akizungumza jana, Profesa wa Chuo Kikuu cha
Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema mwaka huu CCM itakuwa na
ushindani mkali kuliko ilivyowahi kutokea kwenye uchaguzi wowote wa
nyuma.
Alisema ushindani huo unatokana na kuwapo kwa mgombea urais wa Ukawa unaoundwa na vyama Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
“Vyama
hivyo vimeamua kushirikiana kusimamisha mgombea mmoja kwenye nafasi ya
urais, ubunge na udiwani, ushirikiano huo utatoa upinzani mkali kwa
CCM,” alisema Mpangala.
Alisema CCM wameliona hilo na
ndiyo maana Rais Kikwete ameona ni muhimu awaeleze wana CCM kwamba
wanatakiwa kuchagua viongozi wanaokubalika na wananchi walio wengi,
vinginevyo watashindwa.
“Yale mambo ya zamani ya kila
kundi kuwa na mgombea wake yakirudiwa hivi sasa yatakigharimu chama
hicho, wanatakiwa kuungana na kuweka mtu anayekubalika bila kujali
makundi,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo pia alisema
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa na tofauti kubwa na chaguzi
zilizopita, hivyo lazima wapate mgombea maarufu.
Akitoa
mfano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 alisema: “Katika kipindi hicho
Mkapa (Benjamin) hakuwa akifahamika sana ukilinganisha na wana-CCM
wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo lakini alishinda na kuwa rais.
Mwaka huu wakijaribu kufanya hivyo wataanguka vibaya, hali ya kisiasa
imebadilika,” alisema.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka
huu, viashiria vinaonyesha kuwa vyama vya upinzani vinazidi kuwa na
nguvu mwaka hadi mwaka, akitaja Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita
kama mfano... “Hata mgombea wa urais wa CCM, 2010 alipata kura chache
ikilinganishwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Hii ina maana vyama vya
upinzani vinakua kwa kasi,” alisema.
Alisema kukithiri
kwa rushwa na umaskini katika jamii kumewakatisha tamaa wananchi hivyo
watahitaji kiongozi mwenye uwezo kupunguza matatizo hayo.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema Rais Kikwete
anafahamu kuwa chama hicho kisipoweka wagombea wanaokubalika kitaanguka
kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Kikwete ameliona hilo na
wanachama wenzake wafahamu kuwa huu si wakati wa kuweka mtu wao, bali
mtu anayekubalika na wananchi walio wengi,” alisema.
Alisema
ukiacha kwenye nafasi ya urais, CCM wana mifano mingi ambayo waliweka
watu wao lakini wananchi walipiga kura za hasira kuvichagua vyama vya
upinzani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Benson Bana alisema kauli ya Rais Kikwete imelenga kukinusuru chama
hicho kutokana na nguvu kubwa ya vyama vya upinzani.
Alisema
CCM ina wanachama wengi wanaokubalika ndani na nje ya chama hicho ambao
mmoja wao akichaguliwa kugombea urais anaweza kukisaidia.
“Hotuba
ya Kikwete inawakumbusha wanachama kuchagua watu wanaokubalika kwa
sababu wapo, suala hapa anawakumbusha kuchagua mtu sahihi,” alisema.
Kuepuka makundi
Katika
hatua nyingine, Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru
(pichani) amesema haiwezekani kuepuka makundi ya urais katika kipindi
cha uchaguzi ndani ya CCM, lakini mwisho wa siku, chama hicho kitamteua
mtu anayekubalika ndani na nje ya chama.
“Hatuwezi
kwenda kwenye uchaguzi wa kidemokrasia bila ya kuwa na makundi,” alisema
Kingunge wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Uzalendo kilichorushwa na
Kituo cha ITV juzi.
“Mwaka 1995 kila mgombea alikuwa na kundi lake na mwaka 2005 tulikuwa na makundi hata mwaka huu yapo,” alisema.
No comments:
Post a Comment