NAIBU
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema
kuwa akishindwa katika mchakato wa kura za maoni za kusaka urais ndani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), atarudi jimboni kuendelea kuwatumikia
wapiga kura wake.
Kutokana
na hali hiyo January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli, amewataka wananchi
wake kuwapuuza watu wanaopita na kudai kuwa wanataka ubunge kwa kuwa
yeye anatajwa katika kinyang’anyoro cha urais ndani ya CCM.
Kauli
hiyo aliitoa juzi jimboni kwake Bumbuli, wilayani Lushoto mkoani Tanga
katika mkutano wa hadhara ambapo alikuwa akizungumzia mafanikio na
changamoto za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi tangu alipochaguliwa
mwaka 2010.
January
alitumia mkutano huo kuwashukuru wapiga kura wake kwa kumchagua kuwa
mbunge mwaka 2010 huku akisema kuwa kama si wao asingeweza kutajwa
katika mbio za urais ndani ya CCM.
“Kutajwa si dhambi na kwa kuwa fomu za uchaguzi si sumu si dhambi kuchukua…. na kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
“Hivi kuna kiu kubwa ya uongozi wa aina mpya na kuna watu wamemwona mtu na kumtaja yeye jambo ambalo si baya.
"Wapuuzeni watu wanaopita na kusema mimi sitaki ubunge eti kwa sababu natajwa kwenye urais.
"Wapuuzeni watu wanaopita na kusema mimi sitaki ubunge eti kwa sababu natajwa kwenye urais.
“Hayo
ni maneno ya kilaghai na ya kukatisha tamaa na kichochezi msiyakubali.
Kinyang’anyiro ni kama mchezo wa mpira kuna kushinda na kushindwa.
“Tukishindwa
narudi hapa tuendeleze tuliyoyaanza, Rais Kikwete alijaribu mara ya
kwanza kura hazikutimia akarudi jimboni hata pia Kigoda (Dk. Abdallah)
naye alifanya hivyo ikashindikana akarudi kwenye ubunge,” alisema.
Akizungumzia
hatua ya kufufua uzalishaji wa Kiwanda cha Chai Mponde, January
alisema kuwa Serikali imeridhia kutoa Sh bilioni 4 ambazo ni gharama za
kulipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi.
Alisema
mbali na hilo madeni ya malipo ya wakulima, gharama za ukarabati na
mtaji wa kuanzia kuendesha shughuli za uzalishaji utaimarishwa.
January
ambaye yupo katika ziara ya siku tano ya kutembelea jimbo lake, alisema
Serikali ilituma wataalamu kufanya tathmini yenye lengo la kutambua
gharama za ufufuaji wa kiwanda hicho kilichokuwa kikiendeshwa na Chama
cha Wakulima wa Chai cha Usambara (Utega) na mwekezaji ambaye ni Lushoto
Tea Company katika miaka ya mwanzo ya 2000.
Alisema
kwa kuwa fedha hizo hazikuwa katika bajeti ya Serikali, ilibidi ofisi
ya waziri mkuu kuomba kibali kutoka kwa rais ili kutoa fedha hizo.
“Mambo
yote yako tayari. Kilichokuwa kinasubiriwa ni kibali ambacho kimekwisha
kutolewa na Rais Kikwete. Hivi sasa ni Hazina ndiyo inayosubiriwa itoe
fedha hizo kwa ajili ya kukarabati kiwanda na gharama nyingine,” alisema January.
Mgogoro
huo ambao umeleta maumivu makali ya kiuchumi na kijamii kwa wakulima
wapatao 4,000 walioko katika skimu tano za chai zilizopo katika eneo la
Halmashauri ya Bumbuli, ulitatuliwa na Serikali na maamuzi hayo
kutangazwa kwa wakulima na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdulrahman Kinana.
Baada
ya tamko hilo ambalo amelieleza kuwa la kihistoria la kuchukua kiwanda
kutoka kwa mwekezaji kukirejesha kwa wakulima, January alieleza kuwa
Serikali ilianza harakati za kufufua kiwanda kwa kutuma timu ya
wataalamu kufanya tathmini.
Wazee wambariki
Baada
ya kumalizika kwa mkutano huo, wazee wa Bumbuli, walimpa baraka huku
wakimuhakikishia kumwunga mkono katika harakati zake za kisiasa ndani ya
Chama Cha Mapinduzi.
Waliotoa
baraka hizo kwa niaba ya wazee ni Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili
na Kirutheli Tanzania (KKKT) Lushoto, Amasia Mweta na Sheikh Yahya
Mjata.
Ni
dhahiri mpambano wa kuwania urais ndani ya CCM unazidi kunoga, ikiwa
imebakia miezi michache kabla ya kupulizwa rasmi kipenga.
January
Makamba ni mmoja wa makada kutoka CCM waliotangaza nia ya kuwania urais
ndani ya CCM ambaye hivi karibuni aliandika kitabu kinachoeleza nia
yake hiyo.
Katika
kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza mikakati ya mwanasiasa
huyo kijana iwapo atapitishwa na chama chake ili kuwania na hatimaye
kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi kitaifa.
Katika
kitabu hicho chenye kurasa 196, January anasema rais ajaye lazima awe
na tafakuri pana na nia ya kuendeleza nchi na si kuwa na kaulimbiu
nyepesi za afya bure, elimu bure zisizo na ufafanuzi ili kuwahadaa
wananchi.
Kitabu
hicho kilichoandikwa na mchambuzi na mwandishi wa makala za siasa,
Padri Privatus Karugendo kimebeba sera na mikakati yake kiundani ya
kuiongoza nchi iwapo atapatiwa dhamana na CCM kugombea urais.
Katika kitabu hicho kinachoitwa, ‘Maswali na Majibu 40: Mazungumzo na January Makamba kuhusu Tanzania Mpya’,
mwanasiasa huyo anasema uongozi hauishii kwa kauli za juu juu za
kuongeza ajira, kuboresha elimu kwani kila mtu anaweza kuyasema hayo.
January,
anasema katika tafakuri zake anaona rais ajaye anatakiwa kuzitambua kwa
kina changamoto za nchi yake na kuwa na mikakati ya kuzitatua.
Kutokana
na changamoto hizo, Janury anasema ni za kiuongozi na utatuzi wake
unategemea kiongozi mwenyewe, hulka, mtazamo wake na usahihi wa uamuzi
anaoufanya.
“Kuomba
uongozi wa nchi si harakati binafsi na wafuasi wako kupata vyeo. Ni
dhamana kubwa ya kujenga mustakabali wa nchi na kuwaunganisha Watanzania
wote. Kwa hiyo, uamuzi wa kugombea lazima uupe heshima na nafasi
inayolingana na dhamana yenyewe,” anasema January katika kitabu hicho.
No comments:
Post a Comment