Ikulu Yatengewa Sh bilioni 20 - LEKULE

Breaking

19 May 2015

Ikulu Yatengewa Sh bilioni 20

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, amewasilisha makadirio ya bajeti ya Sh bilioni 585 kwa ajili ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016. 
 
Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 20 zimetengwa kwa ajili ya Ofisi ya Rais (Ikulu), ikiwa ni matumizi ya kawaida kwa ajili ya ofisi hiyo na taasisi zake.
 
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jana, Kombani alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 Ikulu imepanga kutekeleza kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa huduma kwa rais na familia yake.
 
Kazi nyingine ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano Ikulu na kuanza maandalizi ya ujenzi wa jengo la mapokezi upande wa baharini. 
 
Nyingine ni ukarabati wa Ikulu ndogo mkoani Mbeya na maandalizi ya ujenzi wa Ikulu ndogo, Zanzibar. 
 
“Kutoa huduma za ushauri kwa rais katika maeneo ya uchumi, siasa, masuala ya jamii, sheria, mawasiliano, uhusiano wa kimataifa, mawasiliano na habari kwa umma.
 
“Kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership).
 
“Kuendelea kuratibu na kusimamia miradi ya maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea,” alisema.
 
Kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kombani alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 taasisi hiyo inakusudia kutekeleza kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchunguza tuhuma 2,776 zilizopo. 
 
Kazi nyingine ni kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa (Grand Corruption) kama ilivyopangwa katika mpango mkakati wa taasisi hiyo.
 
“Kufuatilia na kudhibiti vitendo vya rushwa katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
 
“Kuandaa mafunzo maalumu kwa waheshimiwa majaji na mahakimu kuhusu Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura 329 na Sheria namba 6 ya mwaka 2010 ya Gharama za Uchaguzi na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
 
“Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za rushwa katika uchaguz mkuu wa mwaka 2015. Pia kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya rushwa asasi za raia na waandishi wa habari,” alisema.
 
Bajeti hiyo inahusisha mafungu 10, ambako mbali ya fungu 20 linalohusu bajeti ya Ikulu, jingine ni fungu 30 linalohusu Ofisi Rais, Sekretariet ya Baraza la Mawaziri ambalo ni Sh bilioni 468.
 
Jingine ni fungu 32 Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Sh bilioni 46 na Ofisi ya Rais, Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyotengewa Sh bilioni 7.
 
Kombani alisema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma   na tasisi zake imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kuhakikisha utumishi wa umma unaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
 
Wabunge na rushwa
Nayo Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuimarisha mikakati ya kupambana na rushwa, huku ikitaka watoa rushwa wote wafungwe na wafilisiwe.
 
Akisoma taarifa hiyo jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rwekiza katika dunia ya sasa watoa rushwa wamekuwa wakitumia mbinu za kisasa kutekeleza kosa hilo.
 
Hata hivyo, Rwekiza alisema watoa rushwa na wapokeaji wanapaswa kushughulikiwa bila ajizi, kwa vile taifa linalonuka rushwa watu wake hasa wanyonge hawawezi kupata haki.
 
“Watoa rushwa inabidi washughulikiwe kwa ukamilifu. Watu hawa wachunguzwe, wahojiwe, wakamatwe, washitakiwe, wahukumiwe, wafungwe na wafilisiwe,” alisema Rwekiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini.
 
Aliitaka taasisi hiyo kuongeza nguvu kufanya uchunguzi maalumu wa tuhuma za rushwa katika vocha za pembejeo, maliasili   na kukamilisha uchunguzi kuhusu kashfa ya Tegeta Escrow na watuhumiwa wake wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo.

Mwisho

No comments: