UTANGULIZI:
Ndugu zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,
Hii
ni siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita ili
kuwatangazia rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka kuomba
ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze kuteuliwa kuwa
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nasema
hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini historia yangu itainakili
kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha yangu nimejitokeza
kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama chetu. Mara ya kwanza ilikuwa
ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hapa nchini
nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete; wakati ule sote
tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda pamoja kuchukua fomu ndani ya
Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari.
Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa
Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati ya wawili sisi
basi mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.
Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kabisa kumuunga mkono moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete.
Nikiwa
Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa
wa mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia 80
wa Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.
Nitaeleza
kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na kwa nini naamini mimi
ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. Mpaka hapa itoshe tu
kuwaeleza ni kwa kwa nini naamini leo ni siku muhimu kwangu.
Lakini
nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema hivyokwa sababu naamini
inajibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu wa kumpata
kiongozi imara atakayewaongoza Watanzania kujenga taifa imara. Na hili
pia nitalieleza kwa kina.
Hali ya Nchi na Matarajio ya Watu:
Miaka
48 iliyopita katika jiji hili la Arusha, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage alianzisha mchakato wa kujenga taifa huru kiuchumi na kupiga
vita maadui umaskini, ujinga na maradhi kwakutumia silaha ya
kujitegemea.
Leo
hii, wakati taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao, hatuna budi
kutafakari tulikotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ili tuweze kubuni
upya mikakati ya kuhitimisha azma aliyo kuwa nayo Mwalimu, ili tujenge
taifa huru, lenye utulivu, mshikamano, amani na maendeleo.
Nchi
yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha mpito katika maeneo
yote makuu ya maisha yetu – katika siasa, katika uchumi na katika maisha
ya kijamii.
Kisiasa,
tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa vyama vingi ambapo
ushindani kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali na kwa bahati mbaya
kufikia sura ya kuonekana kama vile ni mapambano ya watu binafsi badala
ya mapambano ya sera na dira ya kuongoza nchi.
Tunashuhudia
kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani ya chama kimoja
kimoja na pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya kingine. Kadiri
siku zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa kuendelea nchi
yetu inaweza kujikuta mahali pabaya.
Kukua
kwa ushindani ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha demokrasia yetu
na tukiwa na ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya kuleta
mabadiliko mema kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kasi ya
maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Kinyume
chake ushindani unaochukua sura ya chuki binafsi au kukomoana na hata
kulipizana visasi si ushindani wenye tija na tunapaswa kuutafutia tiba.
Tunahitaji
uongozi imara kusimamia kipindi cha mpito kutoka siasa muflisi za aina
hii na kuelekea kwenye siasa mpya zinazoimarisha ushindani wenye tija
unaojikita katika kushindana katika kuwapatia huduma bora Watanzania.
Kiuchumi,
tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali
na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi.
Kwa
upande mwengine, Serikali ya Rais BenjaminiMkapa na Rais Jakaya Kikwete
imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi
asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa.
Tanzania
sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika
sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha
ya Watanzania.
Hata
hivyo, kipindi hiki cha mpito kuelekea ujenzi wa uchumi wa kisasa
kimeshuhudia kuongezeka kwa hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi
kwamba hawatonufaika naukuaji huu wa uchumi na ugunduzi wa utajiri
mkubwa wa gesi asilia.
Kwa
upande mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa
utajiri huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili
waweze kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Niliwahi kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi imara ni bomu linalosubiri kulipuka.
Vijana
wasio na ajira hupoteza matumaini na ni rahisi kughilibiwa kuingiza
nchi katika machafuko.Tunahitaji uongozi imara kuweza kuikabili hali
hiyo na kuitafutia suluhisho maridhawa.
Kijamii,
kipindi cha karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya tabia miongoni
mwa raia katika hali ambayo haijawahi kuwa sehemu ya utamaduni wa
Watanzania.
Kumekuwa
na ongezeko la kutisha la matukio ya uhalifu linalokwenda sambamba na
wananchi kuonyesha wanapoteza imani na taasisi zinazosimamia sheria na
usalama na kuamua kujichukulia sheria mikononi mwao.
Kumeripotiwa
matukio mengi yakiwemo ya kuvamiwa vituo vya polisi, askari kupigwa na
kuporwa silaha, matumizi makubwa ya nguvu katika utatuzi wa migogoro
mbalimbali hasa ile ya kijamii, mathalani migogoro ya wakulima na
wafugaji, mivutano ya kidini na pia mivutano baina ya viongozi wa dini
wenyewe kwa wenyewe na baina ya viongozi wa dini na wale wa Serikali.
Matokeo
yakemshikamano wa taifa nao unaingia majaribuni. Mara nyingine wananchi
wanatuuliza viongozi iwapo hii ndiyo nchi tuliyoachiwa na waasisi wetu.
Tunahitaji uongozi imara wa kukabiliana na changamoto hizi na kurudisha
mshikamano wa taifa letu na watu wake.
Watanzania Wanataka Mabadiliko;
Ndugu
zangu, mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote hayo na yana
mahusiano gani na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka kuiongoza
nchi yetu kupitia CCM?
Nimeyaeleza haya kwa sababu haya na matukio mengine yanayoendelea nchini yamepelekea Watanzania kutaka mabadiliko.
Watanzania
wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kuzishinda changamoto hizi na
kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake anaishi akiwa
na uhakika wa mahitaji yake muhimu na papo hapo akijiridhisha kwamba leo
yake ni bora kuliko jana yake, na kesho yake itakuwa bora zaidi kuliko
leo yake.
Kwa
maneno mengine, Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi
imara unaoweza kuwaongoza kujenga taifaimara. Hii ndio Safari ya
Matumaini.
Chama
chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na watangulizi wake, TANU na ASP,
kimepata bahati ya kuungwa mkono na Watanzania tokea enzi za kupigania
uhuru, wakati wa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, na pia
miaka yote tokea Uhuru, Mapinduzi na hatimaye Muungano wetu. Watanzania
hawajawahi kushuhudia chama kingine kikiongoza Serikali zetu zaidi ya
CCM. Wamekiamini na wanaendelea kukiamini.
Hata
katika yale majimbo machache ya nchi yetu ambayo hatukufanya vizuri
katika uchaguzi, ukiangalia kwa undani utaona si kwamba watu wa maeneo
hayo wana matatizo na CCM kama Chama bali wana matatizo na baadhi ya
viongozi ambao walishindwa kukiwakilisha vyema Chama na kutambua matakwa
ya wananchi hao.
Mimi
naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania wanaonekana
kutaka mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba watayapata mabadiliko
hayo ndani ya CCM.
Lakini
kama alivyotupa wasia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995
wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa
nchini, Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM
watayatafuta nje ya CCM.
Mimi
naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko
wanayoyataka. Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na ya ukweli
kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa ajili ya
kujenga taifa imara.
Vyama
vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu. Moja ya hulka ya
binadamu ni kubadilika kulingana na mahitaji ya mazingira anayoishi.
Kwa maneno mengine, binadamu ni ‘dynamic’. Kwa sababu hiyo basi, hata vyama vya siasa vinapaswa kuwa ‘dynamic’.
CCM
haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya ‘dynamism’. Kwa zaidi ya miongo
mitano sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza kubadili dira na
mwelekeo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania ya wakati
husika.
Ndiyo maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi zilizotukabili.
Tanzania
imeendelea kuwa nchi ya amani licha ya kubadili mfumo wetu wa siasa
kutoka ule wa chama kimoja kuja vyama vingi; licha ya kubadili mwelekeo
wa uchumi wetu kutoka ule wa dola kumiliki njia zote kuu za uchumi kuja
katika uchumi wa soko unaozingatia ushiriki mpana wa Watanzania wa
matabaka yote; na hata karibuni kabisa katika mchakato wa kuipatia nchi
yetu Katiba mpya.
Tanzania
tumeweza kufanya mabadiliko ya uongozi mara nne katika hali ya amani na
maelewano, jambo ambalo nchi nyingi za Afrika zimeshindwa.
Ni imani yangu kwamba tukijikubalisha tunaweza tena kuwapa Watanzania wanachokitaka katika zama hizi za sasa.
Lakini
ni lazima tuoneshe dhamira hiyo kwa dhati ili, kama alivyotuasa Mwalimu
Nyerere, Watanzania wasiyatafute mabadiliko hayo nje ya CCM.
Nasisitiza
tena kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko
wanayoyataka, lakini pia wananchi wana hiali kuchagua mabadiliko
wanayoyataka.
Uongozi unaohitajika kuleta mabadiliko yanayotakiwa:
Rais
Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi chake na kama ambavyo
amekuwa akisisitiza mara kwa mara katika hotuba zake za karibuni ni
kwamba yeye ametekeleza wajibu wake kwa kuweka misingi imara ya ujenzi
wa Taifa la kisasa lenye uchumi madhubuti na unaoweza kukua kwa kasi.
Amesema anamwachia atakayemkabidhi uongozi wa nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda wake kuendeleza pale atakapoachia.
Kwa maoni yangu ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:
- Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya kufanya maamuzi magumu;
- Uongozi thabiti na usioyumba;
- Uongozi makini na mahiri;
- Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;
- Uongozi utakaozikabili changamoto kifua mbele na siyo kuzikimbia;
- Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;
- Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo:
- Aweze kuwaunganisha Watanzania (kukabiliana na viashiria vya migawanyiko ya aina mbali mbali inayoinyemelea Tanzania);
-
Aweze kuja na sera na mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza
pato la Mtanzania;ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato kati ya
aliyekuwanacho na wasiokuwanacho;
- Aweze kuja na sera na mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;
- Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;
- Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;
- Asimamie nidhamu ya matumizi ndani ya Serikali;
- Aweze kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali;
- Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara
Uongozi Imara,Taifa Imara
Naamini
kwamba uongozi wa juu wa nchi katika nafasi ya Urais si kazi ya
lelemama na unahitaji utashi. Kabla hata ya kutakiwa na wenzako ni
lazima kwanza wewe mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio kwamba unao
uwezo wa kuwaongoza wananchi wenzako. Na katika hilo, rekodi yako ni
lazima izungumze na kulithibitisha hilo.
Binafsi
nina hazina ya uzoefu na rekodi njema ya matokeo ya kazi nilizozifanya
katika uongozi na utumishi wa umma ndani ya CCM na ndani ya Serikali.
Nilianza kazi nikiwa Katibu Msaidizi wa CCM katika mikoa ya Shinyanga,
Arusha na Moshi.
Nimekuwa
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya CCM. Niliingia
Bungeni mwaka 1985 na baadae mzee wangu, Rais Ali Hassan Mwinyi,
akaniamini kwa kuniteua kuwa Waziri.
Nimekuwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Makaazi na
Maendeleo ya Miji, Waziri wa Mazingira, Waziri wa Maji na hatimaye
Waziri Mkuu.
Miongoni mwa mafanikio ninayojivunia katika uongozi na utumishi wangu, na ambayo Watanzania wanayatambua na naamini wanayathamini, ni pamoja na:
-
Nikiwa Waziri wa Maji chini ya uongozi mahiri wa Rais Mkapa,tulithubutu
kushawishi na kuongoza hatua za kukataa kufungika na makubaliano
yaliyowekwa na wakoloni ambayo yalikuwa yanazizuia nchi zilizopakana na
Ziwa Victoria zisiweze kufaidika ipasavyo na maji ya Ziwa hilo. Leo hii
ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa wanafaidika na ujasiri wetu katika
kukabiliana na suala hilo zito.
-
Nikiwa Waziri wa Mazingira, tulipanda miti mingi zaidi kuliko wakati
mwingine wowote tokea Uhuru na pia kuwakabili kikamilifu na kuwachukulia
hatua waliochafua na kuharibu mazingira.
-
Nikiwa Waziri Mkuu, tulisimamia agizo la Rais Kikwete na kufanikisha
utekelezaji wake ndani ya miaka miwili kwa kujenga shule nyingi za
sekondari kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru.
-
Kipindi hicho hicho, tulisimamia agizo la Rais Kikwete la kuanzisha
Chuo Kikuu cha Dodoma na kuhakikisha kinakamilishwa kwa wakati. Leo hii
Chuo Kikuu hicho ni fahari ya Tanzania.
Tunapomtafuta
Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu
ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
katika nchi yetu. Na kwa Chama Cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye
atakuwa pia Mwenyekiti wa Chama chetu.
Naamini
kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika
mambo ambayo najivunia na sitoyasahau katika historia yangu ni kushiriki
kwangu kuilinda nchi yangu pale ilipohitajika.
Nilishiriki
kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni askari wa mstari wa
mbele wa mapambano. Nikiwa Mbunge nilipata heshima ya kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naamini Watanzania hawatakuwa na wasiwasi
wa usalama wao nikiwa Amiri Jeshi Mkuu.
Nimeeleza
uzoefu wangu kwenye Chama na huo hauhitaji maelezo zaidi. Ninakijua
vyema Chama Cha Mapinduzi kiasi cha kutosha kabisa kukiongoza kama
Mwenyekiti wake pale wakati utakapofika.
Wana-CCM wanajua nikikabidhiwa uongozi, Chama chetu kitakuwa chini ya nahodha madhubuti, mzoefu na asiyeyumba.
Kutokana
na rekodi yangu hii, naamini ninazo sifa za kuwaongoza Watanzania
wenzangu katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la kisasa lenye watu
wazalendo walioshikamana na lenye uchumi imara unaomnufaisha kila
Mtanzania. Naamini ninao uwezo wa kuwapa Watanzania Uongozi imara kwa
ajili ya ujenzi wa Taifa Imara.
Dira yangu na Matarajio ya Watanzania
Mfumo
tuliojiwekea hapa nchini unaelekeza kila chama cha siasa
kinachosimamisha mgombea Urais na kinachowania kuongoza nchi yetu kuja
na Ilani ya Uchaguzi ambayo ndiyo inayoweka misingi ya sera
zitakazofuatwa na Serikali itakayoongozwa na chama hicho pale kinapopewa
ridhaa ya kuongoza nchi.
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa ni cha kupigiwa mfano katika kutayarisha
Ilani bora na ndiyo maana mara zote kimepewa ridhaa ya kuongoza nchi
yetu. Tumefanya hivyo tokea enzi za mfumo wa chama kimoja na tumeendelea
kufanya vizuri katika mfumo wa kushindanisha sera kupitia vyama vingi.
Najua
kwamba Ilani ya CCM ya mwaka 2015 imo katika hatua za mwisho za
kukamilishwa na itakapopata baraka za vikao vya Chama itakuwa ndiyo
msingi wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba
mwaka huu.
Hata
hivyo, naamini pia kwamba mgombea mwenyewe anayetaka ridhaa ya Chama na
ya Watanzania kuongoza nchi naye anapaswa kueleza dira yake.
Mimi, baada ya kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo na matarajio na matumaini waliyo nayo Watanzania, naamini kwamba Uongozi imara unaolenga kujenga Taifa imara unapaswa kuwa na dira yenye malengo yafuatayo:
-
Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia yanayotutenganisha na
kuyafanyia kazi ili yasivuruge yale yanayotuunganisha ambayo ni mengi
zaidi na makubwa zaidi.
-
Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila kwa
kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na zenye kutuelekeza kwenye
Utanzania wetu.
-
Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni shirikishi unaomnufaisha
kila Mtanzania aliyeko mjini au kijijini. Tunapaswa kubadili hali
tuliyo nayo sasa ambapo Kilimo kinaonekana kama kimesahauliwa na
wakulima wetu wanaonekana wanakata tamaa.
Wafugaji
na wavuvi nao wanahisi sekta zao hazijapewa umuhimu unaostahiki.
Tunahitaji kuondokana na hali iliyopo sasa ya kuwa Taifa linalouza
malighafi na badala yake kuwa Taifa linalosindika na kusarifu mazao na
kutengeneza wenyewe bidhaa zitokanazo na malighafi yake.
Ndani
ya miaka mitano ijayo tutahakikishatunaiondolea Tanzania sifa ya
kusafirisha malighafi na badala yake kusindika mazao yanayozalishwa hapa
nchini kama pamba, kahawa, chai na korosho na kuyaongezea thamani
(value addition).Mkakati huu utazalisha ajira nyingi na kuongeza mapato
ya fedha za kigeni nchini.
Tunahitaji
kujielekeza kwenye kujenga viwanda na kuleta ajira. Tuna vivutio vingi
sana vya utalii lakini bado Tanzania inapitwa na nchi kama Afrika Kusini
katika kuingiza idadi kubwa ya watalii.
Kwa
nini nchi kama Dubai iweze kuvutia watalii kwa mamilioni na Tanzania
tushindwe? Tunapaswa kukabiliana kikamilifu na hisia zilizopo miongoni
mwa wananchi kwamba Tanzania hainufaiki ipasavyo na utajiri wa
rasilimali zake nyingi ilizo nazo.
Tutajipanga zaidi kuhakikisha tunanufaika kama nchi na rasilimali zetu kama madini na gesi asilia. Hii ndio Safari ya Matumaini
-
Kukuza kipato cha wananchi na kunyanyua hali za maisha ya watu wetu.
Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha
Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa
matabaka yote zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa
ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia.
-
Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa wingi wa
rasilimali tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari
Tanzania tuna kila sababu ya kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na badala
yake kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika.We can transform our nation
from being the begging bowl to become the bread basket of Africa.
-
Kujenga mfumo mpya wa elimu unaojielekeza kuwatayarisha vijana wetu
waweze kuajirika, kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.
Tumepiga
hatua kadhaa katika elimu lakini kiwango cha elimu bado ni hafifu.
Pamoja na kuwa na shahada (degrees), bado wahitimu wetu hawawezi
kushindana kwenye soko la ajira.
Wakati
tunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki,hatuna
budi kujikita kubadili mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo
ya ufundi na stadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu na wenye
kujiamini katika kukabiliana na changamoto za maendeleo duniani.
-
Kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na kulipunguza kwa kiasi kikubwa
kama si kulimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.
Ni jambo la kusikitisha kwamba tumezungukwa na mito na maziwa lakini
bado watu wetu hawana maji ya kunywa hata ndani ya Dar es Salaam.
-
Kujenga na kusimamia mfumo imara wa kutekeleza sera na sheria
tunazozitunga na kuzipitisha kwa lengo la kumtumikia Mtanzania na
kumjengea uwezo wa kubadili maisha yake ili tuweze kwenda sambamba na
viwango vya kimataifa. Tanzania imepata sera na sheria nzuri sana lakini
utekelezaji wake umekuwa hafifu.
Tumekuwa
wepesi wa kutunga sera na sheria lakini wazito mno wa kuzitekeleza na
kuzisimamia. Uongozi imara wenye kulenga ujenzi wa Taifa imara
utahakikisha tunakuwa mfano wa utekelezaji wa sera na sheria tulizo nazo
na mpya zitakazotungwa kukabiliana na malengo tuliyojiwekea.
Mambo
haya niliyoyaeleza hapa ndiyo yatakayokuwa msingi mkuu wa utendaji wa
Serikali nitakayoiongoza pale nitakapopewa ridhaa ya kubeba bendera ya
CCM katika nafasi ya Urais na pia nitakapopewa ridhaa ya kuliongoza
Taifa letu kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ramani ya Uongozi Imara Ninaouamini 9 Leadership Roadmap)
Kama
nilivyotangulia kusema, kazi ya kuongoza nchi si lelemama na hasa
unapoongozwa na dhamira ya dhati na msukumo wa ndani ya nafsi
unaojielekeza kubadilisha maisha ya wananchi wenzako waliokuamini
uwaongoze. Kwa vyovyote vile, hiyo haiwezi kuwa kazi ya mtu mmoja. Ni
kazi ya pamoja.
Lakini
ili muweze kufanya kazi kama timu moja iliyojipanga kisawasawa kuleta
mabadiliko yanayohitajika na ili muweze kweli kutoa Uongozi imara
unaojikita kujenga Taifa imara hapana budi kiongozi mkuu anayeongoza
timu hiyo aweke ramani anayokusudia kuifuata katika kutoa uongoziimara
anaoukusudia yaani ‘Leadership Roadmap’.
Pamoja
na kuwa sehemu ya uongozi huko nyuma, kutakuwa na maamuzi na matumaini
mapya. Ramani ya uongozi imaraninayokusudia kuutoa kwa wenzangu na
ambayo nitaitumia kuiongoza timu yangu katika kuwatumikia Watanzania wenzangu itajikita katika maeneo yafuatayo:
1.
Kurejea kwenye Katiba katika kuainisha nia, dhamira na malengo yetu ya
kujenga jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu na amani.
Muhimu katika hili ni kukemea tabia mbaya zinazochochea mfarakano katika
jamii kama vile matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila.
Aidha
moja ya misingi muhimu ya Katiba ni Muungano wetu. Itakuwa dhamira
yangu kuimarisha misingi ya Muungano pamoja na udugu wa damu nahistoria
ya ushirikiano iliyojengwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amri Abeid Karume na kuyaenzi
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
2.
Kujenga fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua azma ya
kujitegemea kama Taifa. Ni dhahiri kuwa pamoja na rasilimali zetu, bado
Tanzania ni taifa tegemezi. Bado tunajidanganya kuwa wafadhili
watatujengea nchi. Tukumbuke, nchi zinajengwa nawananchi wake.
Nasi
pia lazima tujikomboe kifkra na tuondokane na utamaduni wa kuwa
tegemezi. Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza
kujitegemea na kuijenga Tanzania sisi wenyewe.Kujiamini na kujitegemea
ndio uhuru wa kweli.
3.
Kujenga uzalendo, uadilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwazi katika
shughuli zote za serikali na kupambana na rushwa.Watanzania tumepoteza
uzalendo kwa kiasi kikubwa. Kuna vitendo vinavyoashiria kuwa hatuipendi
tena nchi yetu.
Tunashabikia
wizi na rushwa. Inabidi turejee kwenye misingi ya taifa letu misingi ya
uadilifu na uzalendo. Tukumbuke kuwa hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa
kama tutaruhusu rushwa ishamiri.
Wawekezaji
hawataleta mitaji yao kwa wingi kama rushwa itaendelea kutawala katika
huduma serikali na wananchi hawawezi kupata huduma bora kama rushwa
itaendelea kutawala. Ni lazima tuipinge rushwa kwa vitendo sio maneno.
4.
Kujenga Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu inayoendeshwa kwa
misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji.Maendeleo ya watu hayawezekani
bila serikali kusimamiautekelezaji sera na miradi na kuleta ufanisi
katika kutoa huduma na kusimamia maendeleo. Tumekuwa wepesi wa kutunga
sera lakini wazito wa kuzitekeleza na kuzisimamia.
5.
Kuleta msukumo mpya wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi
katika ujenzi wa uchumi wa kisasa na unaojitegemea. Sekta binafsi ndiyo
nyenzo ya uchumi imara. Inazalisha mali, ajira na kuchangia kwa kiasi
kikubwa katika pato la taifa kwa kulipa kodi.
Ilisekta
hii itoe mchango unaotakiwa katika maendeleo ni lazima ifanye kazi na
serikali kwa karibu. Tukumbuke, bila uchumi imarahakuna huduma bora!
6.
Uwekezaji katika huduma za jamii. Elimu na afya bora, mazingira, makazi
safi na maji salama ndiyo mihimili ya maendeleo ya watu.
Hii
inawezekana tu iwapo serikali itakuwa na sera na utashi wa kuutambua
uboreshaji wa huduma za jamii kama ndiyo lengo kuu la maendeleo ya nchi.
Serikali nitayoiongoza itahakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu
bora na inayogharamiwa na serikali kama mimi na wenzangu tulivyopata.
Wakatitunazungumzia
kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki, hatuna budi
kurekebisha mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi
na ustadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu, wenye kujiamini,
wenye uwezo kushindana katika soko la ajira na wa kujiajiri. Napenda
kusisitiza kuwa elimu ndiyo muhimili wa maendeleo, ndiyo mkombozi wa
kweli wa binadamu. Mimi ni mfano hai wa ukombozi wa elimu.
Elimu
ndiyoimenivusha kutoka kijijini kwetu Ngarash na kunipa upeo wa
kitaifa. Mama akiwa na elimu atajua umuhimu wa kumpeleka mwanae shule,
anapata lishe bora na chanjo stahili na kuwa anaishi katika mazingira
safi. Elimu ndilo jibu la umaskini, maradhi na ujinga.Taifa lililo
elimika ni taifa lenye maendeleo.
7.
Kujenga uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini.Mkakati wa kuondoa
umaskini Tanzania lazima ujikite kwenye nguzo za ushiriki wa kila
Mtanzania katika uchumi wa taifa.
Kwa
misingi hii, tukiweza kupunguza umaskini, tutaweza pia kupunguzatofauti
za kipato ambazo tukiziacha ziendelee kukua kwa kiasi cha sasa,
zinaweza kuhatarisha utulivu na amani katika jamii yetu.Uchumi
shirikishi ndio silaha dhidi ya umaskini.
8.
Kuimarisha ulinzi wa nchi na usalama wa raia na ujirani mwema.Itakuwa
nia yangu kuimarisha misingi iliyojengwa kulinda na kudumisha umoja na
amani nchini.
Kadhalika,
nitahakikisha kuwa usalama wa mipaka ya Tanzania unaimarishwa kwa
misingi ya ujirani mwema na kutanzua migogoro na matatatizo yoyote na
nchi jirani, kwa njia ya diplomasia na mazungumzo.
Hitimisho:
Hii
ndiyo misingi na dira ya uongozi wangu. Nachelea kusema kuwa haitakuwa
kazi rahisi. Lakini kwa ushirikiano wa kila mmoja na maamuzi magumu,
yote yanawezekana.
Tumeona
nchi nyingi zilizosimamiwa na utawala thabiti wa serikali za
kimaendeleo zikikabili na kupunguza umaskini katika kizazi kimoja. Kama
mataifa mengine yamefanikiwa, tena bila raslimali kama zetu, kwa nini
sisi tushindwe?
Tuna
kila sababu ya kufanya maamuzi magumu sasa ili kuwajengea Watanzania
matumaini mapya ya maendeleo. Naomba nisisitize kuwa katika uongozi
wangu hakutakuwa na nafasi ya majungu, na visasi. Hatutaangalia nyuma
bali tutasonga mbele kwani ndicho Watanzania wanakitarajiakutoka kwa
uongozi uliojengwa kwenye misingi bora.
Ndugu Watanzania:-
Ni maono yangu kuwa siku si nyingi nchi yetu itaanza safari yenye uelekeo wa matumaini na neema tele kwa wananchi.
Ni
maono yangu kuwa siku si nyingi sisi kama Watanzania kwa umoja wetu
tutajivunia kuishi katika nchi tunayoipenda na inayoendeshwa kwa misingi
ya utawala bora, chini ya serikali ya kimaendeleo iliyojengwa kwenye
fikra mpya za uzalendo, uadilifu, utendaji na uwajibikaji.
Ni
maono yangu kuwa Peke yangu sitaweza, lakini kwa maamuzi magumu na
ushirikiano wa kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na wagombea wenzangu
ndani ya CCM, inawezekana kuanza safari hii ya Matumaini Mapya.
Kabla ya kumaliza hotuba yangu hii fupi, kuna mambo matatu ningependa kuyaweka wazi hapa.
La
kwanza, linahusu msingi wa uongozi ninaouamini na ambao nimeusema mara
kadhaa hapa. Msingi huo ni UWAJIBIKAJI.Watanzania wananifahamu mimi si
mtu wa maneno, ni mtu wa vitendo. Naamini kwa dhati kabisa kwamba huwezi
kuwa na Uongozi imara utakaoweza kusimamia ujenzi wa Taifa imara iwapo
huna ujasiri wa kuwajibika. Mimi nimeongoza kwa mfano, na pale
ilipobidi, nilikubali kuwajibika na kubeba dhamana ya
uongozinilipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu.
La
pili, mimi si mtu wa visasi. Siamini katika kuangalia ya nyuma.
Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Na kwa nini tuangalie nyuma wakati
kama taifa tuna kazi kubwa sana mbele yetu inayohitaji kufanywa? Mimi
ni Mkristo; najifunza kutoka kwa Bwana Yesu ambaye alipoulizwa:
“Nisamehe mara ngapi?” Alijibu, “Samehe mara sabini mara saba”. Nitaenzi
na kudumisha utamaduni huu wenye sura ya utu na heshima.
La
Tatu, natambua kwamba dhamana ya Urais ni shughuli nzito hasa kwa taifa
ambalo lina changamoto nyingi. Nataka niwahakikishie Watanzania
wenzangu kwamba afya yangu ni njema kuweza kuwatumikia katika jukumu
hili zito. Pamoja na vijineno vinavyosemwa pembeni, mimi mwenyewe ndiye
ninayejijua zaidi. Nawahakikishia kuwa nisingekuja hapa leo na kueleza
nia yangu hii ingekuwa sina uhakika na afya yangu.
Natoa
RAI kwa Chama changu cha CCM, nadhani umefika wakati kwamba tutende
tofauti na mazoea, watu wote walionyesha nia ya kutaka kuongoza, liundwe
jopo la madaktari wa ndani na nje ya nchi tupimwe afya zetu, kwa hili
najitolea kuwa wa KWANZA KUPIMWA afya yangu
Safari tuianze leo, hatuna kesho nyingine.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment