Dar es Salaam yapangiwa siku 12 uandikishaji wapiga kura - LEKULE

Breaking

23 May 2015

Dar es Salaam yapangiwa siku 12 uandikishaji wapiga kura


Dar es Salaam. Hatimaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeweka hadharani ratiba nzima ya uandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) huku mkoa wa Dar es Salaam ukipangiwa siku 12  tofauti na mwezi mmoja uliotumika katika mikoa mingine.
NEC imetoa ratiba hiyo baada ya kuwepo mashinikizo kutoka kwa wadau na ikiwa ni miezi mitatu tangu ilipoanza kuandikisha kitaifa mkoani Njombe, Februari 23 kwa kuandikisha watu 300,800.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu kwa Mpiga Kura, Ruth Masham, wakazi wa Dar es Salaam wataanza kujiandikisha kuanzia Julai, 4 hadi Julai 16 mwaka huu.
Siku hizo ni pungufu kwa siku 16 kutoka katika wastani wa siku 28 ambazo zinatumika Lindi na Mtwara au Ruvuma na Iringa licha ya jiji hili kuwa na watu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kupiga kura zaidi ya 2.93 milioni, kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Takwimu (NBS).
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva aliiambia Mwananchi kuwa Dar es Salaam imewekewa siku chache kwa kuwa mashine zote za BVR zilizokuwa mikoani zitakuwa zimesharudishwa kufanikisha mpango huo kwa haraka.
“Dar es Salaam tumeiacha mwisho kimkakati kwa sababu karibu mashine zote zitakuwa zimesharudi. Tutaandikisha wananchi wote watakaojitokeza katika vituo vya kujiandikisha.
“Ikitokea wakabaki wengi ndani ya siku zilizopangwa, ratiba hii siyo msahafu,  tutaongeza siku kuhakikisha wanaandikishwa wote waliokuwa wamefika vituoni na hii ni kwa nchi nzima…isipokuwa waelewe kuwa NEC haiwezi kuwafuata watu majumbani wakajiandikishe wanatakiwa wajitokeze kwa wingi,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema Jumanne hii walipokea mashine za BVR 1,580 na kufanya idadi ya vifaa hivyo kufikia 6,450 na kwamba umebaki mkupuo mmoja tu utakaokamilika Mei 30 kwa kuingiza mashine 1,550 ili kutimiza idadi ya mashine 8,000.
Alisema baadhi ya mikupuo imekuja na BVR chini ya 1,600 kwa kuwa ndege nyingine za kukodi hazitoshi kubeba kiasi hicho ila wamekuwa wakifidia katika safari zinazofuatia hadi walipofikisha kiasi hicho.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa uandikishaji katika mikoa ya Lindi na Mtwara unamalizika kesho wakati mkoa wa Ruvuma unatarajia kukamilisha Mei, 28 mwaka huu.
Mjini Iringa uandikishaji huo ulioanza Aprili 29 utachukua mwezi mmoja na kukamilika Mei, 29.

Hivi karibuni, Mratibu wa kazi hiyo mkoani Iringa ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi, Wilfred Myuyu alisema hadi kufikia Mei, 14 mkoa huo ulikuwa umeandikisha kwa kuvuka lengo la matarajio na kufikia asilimia 55 ndani ya wiki mbili.
Myuyu alibainisha kuwa walikuwa wameshaandikisha watu 271, 228 dhidi ya matarajio ya watu 492,277 huku uandikishaji ukiwa umesalia kwa siku 14.
Wakazi wa mkoa wa Rukwa kuanzia kesho watakuwa wakijipanga mistari kwenda kujiandikisha hadi Juni, 23 wakati Katavi walioanza kujiandikisha Jumatatu hii watakuwa wakimaliza Juni, 17.
Masham alisema kuwa mikoa ya Kigoma, Kagera, Singida, na Tabora iliyoanza uandikishaji juzi itamaliza kazi hiyo siku moja baada ya Katavi.
“Mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu itaanza kuandikisha Juni, 2 hadi Julai, 4 wakati mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mara na Manyara itaanza Juni 12 hadi Julai, 12,” inasomeka sehemu ya ratiba hiyo.
Wiki moja ya mwisho ya uandikishaji katika mikoa ya Kaskazini itakuwa ikienda sanjari na Dar es Salaam licha ya Lubuva kubainisha kuwa takriban mashine zote za mikoani zitakuwa zimerudishwa jijini hapa.
Wakazi wa Morogoro, Pwani na Tanga wao wataanza kujiandikisha Juni 18 na kutumia mwezi mmoja hadi Julai, 18. Takwimu za NBS zinakadiria Morogoro kuwa na watu wanaostahili kupiga kura zaidi ya 1.28 milioni wakati Tanga ina watu zaidi ya 1.12 milioni.
Zanzibar yenye mikoa mitano, kwa mujibu wa ratiba hiyo NEC itatumia siku tatu kuandikisha wapiga kura kuanzia Juni, 14 hadi Juni 16. Zanzibar yenye Mikoa ya Kusini Pemba, Kaskazini pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Mjini Magharibi inakadiriwa kuwa na jumla ya wapiga kura 720,491.
Kuhakiki majina
Jaji Lubuva alibainisha kuwa NEC imeweka utaratibu wa kuanza kuhakiki majina mara tu mikoa husika itakapokua imemaliza uandikishaji ili kutoa fursa ya wale waliobaini makosa kurekebisha.
“Hata Njombe ambako tulishamaliza kuandikisha tutaweka bayana majina yao na kuwaruhusu wananchi waje wathibitishe na kurekebisha na hii itaendelea mikoa yote kuhakikisha na tunamaliza kwa wakati,” alisema.

No comments: