Wabunge watano wa viti maalumu wasaka majimbo - LEKULE

Breaking

20 Apr 2015

Wabunge watano wa viti maalumu wasaka majimbo



Dar es Salaam. Joto la harakati za kuwania ubunge, linazidi kupanda, baada ya wabunge kadhaa wa viti maalumu wa kambi ya upinzani na chama tawala CCM, kujipanga kutetea nafasi zao za ubunge kupitia majimbo.

Miongoni mwa wabunge hao ni Dk Prudenciana Kikwembe (CCM) ambaye anajipanga kuwania ubunge katika jimbo la Katavi ambalo sasa linawakilishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mbali na Dk Kikwembe, wabunge wengine ni Ester Bulaya (CCM) anayeenda jimbo la Bunda kupambana na Stephen Wasira, Susan Kiwanga, (Chadema) anayewania Jimbo la Kilombero kupambana na Abdul Mteketa, Susan Lyimo, (Chadema) anayejipanga kupambana na Idd Azzan katika Jimbo la Kinondoni na Dk Mary Mwanjelwa, (CCM) anayekwenda Mbeya Mjini kupambana na Joseph Mbilinyi (Chadema).

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wabunge hao wamesema, tayari wametia nia kuachana na ubunge wa viti maalumu, wamejipanga vyema na wanatarajia kupata ushirikiano mzuri kutoka kwenye vyama vyao.

Dk Kikwembe alisema ameamua kugombea jimbo hilo, baada ya kusikia kuwa Pinda anatajwa kuwa miongoni mwa wenye nia ya kugombea urais.

“Ingawa najua ninakabiliana na changamoto ya mfumo dume miongoni mwa jamii, naamini nitaweza,” alisema.

Kwa upande wake Bulaya alisema miaka mitano kuwa mbunge wa viti maalum, imemsaidia kumjengea hali ya kujiamini kisiasa na kushiriki katika hatua za kutafuta maendeleo.

“ Nikijipanga kwamba nitagombea baada ya kumaliza kipindi cha miaka mitano ingawa ningeweza tena kugombea kwa tiketi ya viti maalum, lakini nataka jimbo, kwa jinsi nilivyowatumikia wananchi wa Bunda, naamini wamenitambua vyema,” alisema Bulaya.

“Baada ya kujitathimini na kutambua kwamba ninaweza kutumia fursa ya uongozi huo katika kuwasaidia wananchi kupambana na umasikini. Najua ushindani ni mkubwa kwani kuna watu 12 ndani ya chama wanaotaka nafasi hiyo,” alisema Kiwanga.

Kiwanga alisema katika kipindi cha ubunge wa viti maalumu, amekuwa akiwasaidia wananchi kupambana na umasikini alioeleza kuwa mahala pengine uliwafanya watoto washindwe hata kwenda shule.

Lyimo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanawake Tanzania, alisema ameamua kugombea ubunge wa jimbo, baada ya kutumikia ubunge wa viti maalum kwa vipindi viwili.

“Mimi ni mkazi wa Kinondoni najua nitaweza kusaidia wakazi wa jimbo hili kujikwamua katika changamoto mbalimbali zinazowakabili. Nimekuwa nikiwasaidia vijana na kina mama, hivyo naamini nitaweza kuwa mbunge wa jimbo na nitafanya vizuri,” alisema Lymo.

Dk Mwanjelwa alisema amehamasika na mafunzo ya semina za mara kwa mara walizokuwa wakipewa chini ya wadhamini wao wa UN Women, hivyo anajiona ana kila sababu ya kugombea jimbo hilo.

“ Mafunzo yale yalikuwa yanalenga kutufanya tutambue jinsi gani ya kuwa viongozi bora kwa wananchi, kutovunjwa moyo na mfumo dume yamenisaidia binafsi nawashukuru sana UN Women, UNDP na wengine wote wametujengea uwezo zaidi,” alisema Dk Mwanjelwa.

No comments: