Mtunisia: Nyota Yanga laini sana - LEKULE

Breaking

20 Apr 2015

Mtunisia: Nyota Yanga laini sana



Dar es Salaam. Beki wa kati wa Etoile du Sahel, Bedoui Rami amesema tatizo kubwa la Yanga ni wachezaji wake kuwa legelege, hawana nguvu na kwa staili hiyo hawawezi kupiga hatua kwenye soka la kimataifa.

Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga walikubali kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Etoile du Sahel ya Tunisia katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya pili, lililofungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa mkwaju wa penalti baada ya kipa wa Etoile, Mathlouthi Aymen kumuangusha Simon Msuva katika eneo la hatari.

Etoile walisawazisha mwanzoni mwa katika kipindi cha pili kupitia kwa Ben Amor Med Amine aliyepiga shuti la chini chini akiwa umbali wa mita 20.

Akizungumza na gazeti hili Rami alisema sisi Waafrika tunasifika kwa kucheza mpira wa nguvu, hivyo mashindano yetu ya kimataifa ya bara letu yamekuwa yakimalizika kwa timu zenye wachezaji wenye nguvu kushinda.

“Yanga ni timu bora na ilitupa changamoto, lakini ubora wao si kitu kama wanacheza bila nguvu,” alisema Rami.

“Wachezaji wenyewe wanatakiwa kutengeneza nguvu kwa kufanya mazoezi, lakini klabu iwe na programu nzuri kwa wachezaji na wakifanya hivyo wataweza kupambana kirahisi na timu yoyote ya barani Afrika kwani timu nyingi zinacheza mchezo wa nguvu licha ya kwamba kila mchezaji anakuwa na kipaji chake.

“Kwa mtazamo wangu wachezaji wengi wa Yanga hawana nguvu hivyo kwetu sisi ilitusaidia kwani tuliwazidi zaidi kwa kutumia nguvu na si kitu kingine. Uwezo wa Yanga unaweza kuwa bora zaidi iwapo wachezaji wataongeza nguvu,” alisema Rami.

Hata hivyo pamoja na mtazamo huo wa Mtunisia huyo bado kuna mambo mawili; kwanza katika mpira lolote linaweza kutokea, mpira unadunda, hivyo Yanga inatakiwa kujipanga upya kimbinu kwa ajili ya kukabiliana na Etoile katika mechi ya marudiano.

Pili, Etoile ilimiliki mpira zaidi na kutengeneza nafasi nyingi za mabao ikiwa ugenini katika mechi dhidi ya Yanga iliyochezwa juzi hivyo Etoile inaweza kufanya vizuri zaidi ikiwa nyumbani.

Katika mechi ya juzi, Etoile iliwalazimisha Yanga kucheza mchezo wanaoutaka, mchezo wa kupooza mpira wakati Yanga huwa inacheza mchezo wa kasi.

Kitendo cha Yanga kukubali kupoozeshwa kiliwawezesha Etoile kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za mabao na kushindwa kuzitumia nafasi hizo.

Pia, katika mechi hiyo wachezaji wa Etoile walionyesha nidhamu kubwa ya utekelezaji wa mbinu zao kwani walikuwa wakijilinda kwa idadi kubwa ya wachezaji na walikuwa wakishambulia wote.

Etoile vilevile iliua sehemu ya kiungo ya Yanga hasa kiungo wa juu kwa sababu ilikuwa ikichezesha viungo wakabaji wawili ambao ni Franck Kom na Ben Amor Med Amine raia wa Cameroon.

Viungo hao hawakuwaruhusu viungo wa Yanga, Hassan Dilunga na Haruna Niyonzima kutengeneza nafasi kwa Msuva wala Mrisho Ngassa ambao ndiyo huanzisha mashambulizi ya kasi ya Yanga hivyo Yanga kujikuta ikiinga mara chache katika eneo la hatari la Etoile. Pia, Etoile iliwadhibiti mabeki wa pembeni wa Yanga, Juma Abdul na Oscar Joshua kushindwa kupanda kwani walikuwa wakiwatumia vizuri mawinga wao Mouihbi Youssef na Alaya Brigui ambao walikuwa wakipewa mipira mara nyingi na viungo wao huku wakisaidiwa na Mcameroon Alkhaly Bangoura.

Katika safu ya ulinzi, ukuta wa Etoile uliongozwa na Bedoui Rami na ulikuwa ukitengeneza mtego wa kuotea kwa washambuliaji wa Yanga, Amiss Tambwe, Msuva na Ngassa hivyo mashabiki wa Yanga kumlaumu mshika kibendera kuwa anawahujumu.

No comments: