Serikali Yapata Kigugumizi Shule za Sekondari Kufungwa Kutokana na Kukosa Chakula - LEKULE

Breaking

14 Apr 2015

Serikali Yapata Kigugumizi Shule za Sekondari Kufungwa Kutokana na Kukosa Chakula



Kizungumkuti kimezidi kujitokeza katika suala la kufungwa kwa shule za sekondari za bweni za serikali kwa kile kinachoelezwa ni ukosefu wa chakula kutokana na wazabuni kugoma, baada ya serikali kutoa tamko ikieleza kuwa kuwa imelipa fedha za wazabuni hadi Machi, mwaka huu.

Katika tamko hilo, serikali inazikana taarifa zinazotolewa na baadhi ya wakuu wa shule hizo kuwa zinakabiliwa na uhaba wa chakula na kulazimisha kuzifunga.

Hata hivyo, licha ya kukana taarifa za wakuu wa shule zilizoathirika, serikali inathibitisha kuchelewa kutolewa kwa fedha za chakula za Machi, mwaka huu, ambazo zilipaswa kulipwa shuleni mwishoni mwa mwezi huo na kwamba kwa sasa zipo kwenye akaunti za halmashauri.

Kutokana na hali hiyo, serikali imewaomba wazabuni hao kuendelea kutoa huduma wakati serikali inafanya utaratibu wa kuwalipa fedha hizo ambazo zimeshafika kwenye akaunti za shule.

Kauli ya serikali imetolewa siku chache, baada ya baadhi ya wakuu wa shule hizo kueleza kuwa wameshindwa kuwaweka wanafunzi shuleni bila chakula na kuwataka kurudi nyumbani hadi chakula kitakapopatikana.

Katibu Mkuu wa Tamisemi, Jumanne Sigini, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, aliagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa na Majiji kuwachukulia hatua walimu hao kwa kuwa hawakustahili kutangaza kufungwa kwa shule, bali kuwasiliana nao (wakurugenzi) ambao ndiyo wenye mamlaka.

“Ninaposikia mtu anasema tumekosa chakula tunafunga shule napata shida, haiwezekani fedha ziende kwenye akaunti zao halafu wazabuni waseme hawajalipwa,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa kipindi cha Julai, mwaka jana hadi Machi, mwaka huu, serikali imelipa zaidi ya Sh. bilioni 28.1 (asilimia 66.7) za chakula kwa shule za sekondari za bweni, shule za msingi elimu maalum za bweni.

Alisema kwa mwaka 2014/15 fedha zilizotengwa kwa ajili ya chakula ni zaidi ya Sh. bilioni 42.1 na kwamba kiasi ambacho hakijalipwa ni zaidi ya Sh. bilioni 13.9 ambazo ni (asilimia 33.23) za kumalizia miezi minne iliyobaki.

Katibu Mkuu huyo aliweka bayana mchanganua huo na kiasi cha fedha ambacho kililipwa kwa kila mwezi kwenye mabano kuwa ni Julai (Sh. bilioni 3.5), Septemba (bilioni 3.5), Oktoba (bilioni 3.5), Novemba (bilioni 2.1), Januari (bilioni 3.5), Februari (bilioni 3.5) na Machi (bilioni 8.4).

Sagini alisema zipo taarifa za kufungwa kwa baadhi ya shule na mikoa yake kwenye mabano ambazo ni Rugambwa, Kahororo, Nyakato, Ihungo (Kagera); Lyamungo (Kilimanjaro); Mpwapwa na Abeid Karume (Dodoma) na Kazima, Milambo, Tabora Wasichana na Wavulana, (Tabora), kwa madai ya kukosa chakula.

“Napenda kutumia nafasi hii kuweka bayana kuwa wenye shule za sekondari ni mamlaka za serikali za mitaa ambazo watendaji wake wakuu ni wakurugenzi. Wakuu wa shule ni viongozi wasimamizi hawana mamlaka ya kutangaza kufunga shule kwa sababu yoyote bila kibali cha mwenye shule. Wakati wowote kunapotokea changamoto za uendeshaji wanatakiwa wafanye mawasiliano na wakurugenzi wa Halmashauri,” alisema na kuongeza:

“Ikumbukwe kuwa shule huendeshwa kwa vipindi maalum na kutokana na miongozo iliyopo, mwanafunzi anatakiwa kusoma darasani siku 194 kwa mwaka, kwa vyovyote vile idhini ya kufunga shule kabla ya tarehe zilizopagwa katika muhula, inatakiwa kutolewa na Katibu Tawala wa Mkoa baada ya maelekezo ya Katibu Mkuu Tamisemi.”

Katibu Mkuu huyo alisema hadi sasa serikali haijatamka kufunga shule na kwamba wakuu hao wamefanya makosa kwa kuwa hawakuwasiliana na mamlaka husika ili kupata kibali, na kama kungekuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, waliotaka kujua kama Tamisemi imefuatilia kujua fedha hizo ziliingia kwenye akaunti za shule husika, kiasi cha madeni ya nyuma ya wazabuni, idadi ya wazabuni na lini madeni hayo yatalipwa, Sigini alisema wamezungumza na wakurugenzi wa halmashauri husika ambao wamedai kupeleka fedha kwenye shule husika na kwamba Wizara inafuatilia kama fedha hazikupelekwa Wakurugenzi watachukuliwa hatua stahili.

Kuhusu madeni ya miaka ya nyuma ya wazabuni, Sigini alisema hawana kumbukumbu sahihi kwa wakati huu, lakini ni kweli wanadaiwa na kwamba serikali inafanya uhakiki wa madai hayo kabla ya kuanza kulipa.

Alisema kumekuwa na udanganyifu katika kuorodhesha madeni ya wazabuni hao kwa kuweka fedha nyingi ambazo siyo za kweli na ndiyo maana serikali imeamua kuhakiki kabla ya kulipa na mara zoezi hilo litakapomalizika watalipwa.

Shule za sekondari zilifungwa Machi 28, hadi Aprili 12, mwaka huu, kwa ajili ya mapumziko na shule nyingi zilifunguliwa kati ya Aprili 08 na 12, mwaka huu.

Aidha, kutokana na uhaba wa chakula katika baadhi ya shule waliongeza siku za likizo na kuna shule ambazo hazijafunguliwa hadi sasa.

Shule hizo zilizopo katika mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro, Kagera, Dodoma, Tabora, Mtwara na Lindi, baadhi ya wanafunzi walieleza kuwa baada ya kufika shule walitangaziwa kuwa hakuna chakula, hivyo wanaotakiwa kubaki ni wanaotakiwa kufanya mitihani ya Taifa.

No comments: