Mzee Wa Miaka 68 Auawa Na Wananchi Kwa Kupeleka Waganga Kijijini Kilimanjaro - LEKULE

Breaking

9 Apr 2015

Mzee Wa Miaka 68 Auawa Na Wananchi Kwa Kupeleka Waganga Kijijini Kilimanjaro




Mzee mwenye umri wa miaka 68, Celestine Mushi, mkazi wa kata ya Motamburu wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, ameuawa na wananchi wanaotajwa kukasirishwa na kitendo chake cha kupeleka waganga wa jadi kijijini kwa lengo la kuifanyia zindiko nyumba yake.

Mushi anadaiwa kuwatoa waganga hao wawili jijini Dar es Salaam na kuwapeleka Rombo kwa kazi hiyo maalumu.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Godfrey Kamwela aliyesema mauaji hayo yalitokea juzi saa 2.30 usiku nyumbani kwa Mushi katika kitongoji cha Mbomai Juu, wakati waganga hao wakiendelea na zindiko lao.

Kamwela aliwataja wanaodhaniwa ni waganga wa jadi kuwa ni Ashraf Mjengwa (22) na Peter Mmaka (25), wote wakazi wa Magomeni, Dar es Salaam.

Alisema waganga hao walifika nyumbani kwa Mushi juzi saa 10 jioni, na ilipofika saa 11 walianza shughuli ya zindiko na walipomaliza, Mushi alitaka kuwapeleka katika nyumba ya mkwe wake aitwaye Priscila Hilment, ili nayo ifanyiwe zindiko.

Kamwela alisema kitendo hicho kilikataliwa na mama mkwe, ambaye alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi ili wawaondoe waganga hao, ambapo wananchi walifika na kuwashambulia waganga hao.

Alisema kutokana na tafrani hiyo, raia mmoja alitoa taarifa katika kituo cha polisi, ambapo polisi walifika eneo la tukio na kufanikiwa kumwokoa mganga mmoja, Mjengwa, ambapo mwenzake alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Kamwela alisema ilipofika saa 2 usiku, kundi la wananchi wasiojulikana idadi yake walirudi nyumbani kwa mzee huyo na kuanza kumpiga kwa fimbo kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake, na kisha kuondoka na kumwacha akivuja damu nyingi.

Alisema kutokana na damu kuendelea kuvuja, mtoto wa mzee huyo alimchukua baba yake na kumpeleka katika kituo cha afya cha Tarakea, ambapo alifariki dunia kabla ya kupatiwa matibabu na Jeshi la Polisi limeanza msako wa kuwatafuta wahusika.

No comments: