Minja: Serikali haiwezi kutatua mgogoro uliopo - LEKULE

Breaking

7 Apr 2015

Minja: Serikali haiwezi kutatua mgogoro uliopo





Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja amesema hakuna dalili zinazoonyesha kuwa mgogoro uliopo kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) utaweza kumalizwa na Serikali iliyopo madarakani.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Minja alisema baadhi ya viongozi waliopo madarakani wanashindwa kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo kwa kuwa wananufaika na biashara ya kuuza mashine za risiti za kieletroniki (EFD) ambazo zinapingwa na wafanyabiashara.

Pia, mwenyekiti huyo alisema kuwa viongozi hao wanajinufaisha kutokana na mapato yanayopatikana kwenye kodi inayolipwa kwa njia isiyo sahihi.

Akifafanua Minja alisema tangu kuingizwa kwa mashine za EFD nchini, kumekuwapo na ‘misuguano’ kati ya wafanyabishara na TRA kwa kuwa mashine hizo zinakata kodi kwenye mauzo ya bidhaa na si kwenye faida kama ilivyo kwenye mashine za aina hiyo katika nchi nyingine.

Akitoa mfano, Mwenyekiti huyo alisema: “Ukienda kununua sahani ya ndizi ambayo inauzwa Sh10,000 ile mashine ya EFD ukiitumia itaonyesha mauzo ya bidhaa hiyo kwa Sh10,000, lakini mpaka ile sahani ikafika mezani ina maana kwamba ulinunua ndizi, nyama, nyanya, vitunguu na mafuta lakini hakuna namna ya kuweza kupata uthibitisho wa stakabadhi kwenye vitu vyote ulivyovinunua.”

Alisema kwamba kwa Sheria ya Mapato, kodi inayopaswa kukatwa ni asilimia 30 ya ile Sh10,000 ambayo ni sahani moja ya ndizi, ingawa mfanyabiashara hakupata faida hata Sh1,000.

Minja ambaye kitaaluma ni mhasibu, aliongeza kuwa wafanyabiashara wanahoji namna ambavyo Serikali ilifikia uamuzi wa kuuza mashine za EFD kwa Sh800,000 wakati bei yake halisi haizidi Sh50,000.

“Tulipowauliza (TRA) walituambia mashine za EFD zinazotumika Tanzania hazipatikani sehemu nyingine yoyote ulimwenguni, lakini ukilinganisha na tulizo nazo sisi zinatofautiana sehemu ya kuweka kadi tu,” alisema.

Huku akionyesha kujiamini, mwenyekiti huyo alidai kuwapo kwa njia mbili za kulipa bidhaa zinazochukuliwa bandarini, utaratibu ambao unawanufaisha baadhi ya vigogo nchini.

Akitoa mfano wa kuingiza kontena bandarini, Minja, alisema: “Ukitaka kulipa mwenyewe utajikuta unaambiwa kodi ni Sh200 milioni lakini kuna watu fulani ukiwatumia ambao wana uhusiano na watu fulani bandarini utalipa Sh40 milioni lakini utapewa stakabadhi ya Sh10 milioni.

“Sasa mtu ataenda wapi, akalipe Sh200 milioni au Sh40 milioni akapewe stakabadhi ya Sh10 milioni? Wote watakwenda kwenye Sh10 milioni halafu anapotakiwa kuonyesha gharama zake zilizotumika hataweza kuionyesha ile Sh40 milioni kwa sababu stakabadhi aliyonayo ni Sh10 milioni,” alisema.

TRA yafafanua

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kazi ya mashine ya EFD ni kutunza tu kumbukumbu na kwamba gharama nyingine hujulikana baada ya kufanyika kwa mahesabu.

“Huo ni utaratibu dunia nzima, labda kama wao (wafanyabiashara) wanataka zitengenezwe mashine za aina nyingine. Mashine hizi zinamsaidia mfanyabiashara kutunza taarifa zake, lakini kama umekula hotelini gharama hizo haziingii kwenye mashine,” alisema Kayombo.

Kuhusu gharama ya kulipia kodi makontena, Kayombo alisema kila kontena linatozwa bei yake kulingana na aina ya mzigo lililobeba hivyo iwapo kuna mtu atafanya kinyume anapaswa kuchukuliwa hatua.

“Huo ni udanganyifu, wahusika watajwe. Ni sawa na mtu anayekata viungo vya albino halafu tunabaki kusema yupo miongoni mwetu bila kumtaja. Kama kuna kontena limetolewa kwa utaratibu huo, hatua zitachukuliwa.

Rushwa bandarini

Minja alisema sakata nzima la kutokuelewana kati ya Serikali na wafanyabiashara nchini kuhusu matumizi ya mashine za EFD linachochewa na watu wachache wenye masilahi binafsi.

”Kuna ubadhirifu mkubwa sana, kuna rushwa kubwa sana bandarini nadhani unasikia makontena ya vitenge yamekamatwa yaliyotakiwa kulipiwa ushuru Sh64 milioni, lakini unaambiwa kuwa iliandikwa mlikuwa na bidhaa ambazo bado hazijakamilika (raw material), mwisho wa siku linalipiwa ushuru wa Sh3 milioni.

“Kwa hiyo, Serikali inaibiwa Sh61 milioni, sasa jiulize Tanzania zimeingizwa kontena ngapi, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amekamata makontena 20 ambayo gharama yake ni Sh1.5 bilioni.”

Alisema siku zote wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kutokuwapo kwa uwazi katika kutoa bidhaa bandarini. Pia alisema Serikali imekuwa ikipata hasara kutokana na kupoteza fedha ambazo zilipaswa zipatikane kwa njia ya kodi.

No comments: