Butiku: Yaliyonyofolewa Katiba Mpya yarudishwe - LEKULE

Breaking

7 Apr 2015

Butiku: Yaliyonyofolewa Katiba Mpya yarudishwe





Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusogeza mbele tarehe ya Kura ya Maoni ya Katiba inayopendekezwa, iwe mwanzo wa kutafakari na ikiwezekana kurejesha mambo ya msingi yaliyoondolewa katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alitangaza kusogezwa mbele kwa tarehe hiyo, hadi itakapotangazwa tena. Awali, ilipangwa kuwa Aprili 30.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Butiku aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, alisema kuahirishwa kwa upigaji Kura ya Maoni ni nafasi pekee kwa NEC kujipanga upya na kuhakikisha wananchi wanaandikishwa kwa kiwango kikubwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Alisema pia ni wakati mwafaka kuwapo kwa majadiliano ya kina ili kuangalia nini kinatakiwa kirudishwe kutoka katika vile vilivyoenguliwa kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba kama itawezekana.

Wakati Butiku akisema hayo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema kipindi hiki cha kusitishwa Kura ya Maoni, kitumike kuingiza mambo makuu manne yaliyonyofolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa.

Jana gazeti hili liliripoti kuwa kuahirishwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kumewafungulia viongozi wa Ukawa kuishinikiza Serikali kuiboresha Katiba ya mwaka 1977 katika maeneo manne ili kuondoa mvutano katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Mambo manne yanayodaiwa na Ukawa ni; ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50, kuwapo kwa mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya uchaguzi na matokeo ya urais kupingwa mahakamani. Umoja huo unasema mambo hayo ni sehemu ya maafikiano baina yake na Rais Jakaya Kikwete Septemba 8, mwaka jana.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ni ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa Katiba Mpya na kuondoa uwezekano wa vurugu.

Katika kikao hicho, Mbatia alisema walitiliana saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari, jambo ambalo pia halikufanyika.

Kauli ya Butiku

“Rasimu ya pili ya Katiba iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo mimi nilikuwa mjumbe, ilikuwa imebeba mambo mengi na muhimu ya wananchi ambayo yaliondolewa, hivyo huu ni wakati mwafaka kutafakari kwa kina jinsi ya kuyarudisha,” alisema Butiku.

Alisema hiyo pia ni nafasi kwa wananchi ambao baadhi yao walikuwa wanaburuzwa, ama na chama au na mtu fulani kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa ambayo hawajaisoma na kuielewa kufanya hivyo.

Alisema licha ya kuahirishwa kwa upigaji wa Kura ya Maoni wa Katiba hiyo, bado kuna maswali mengi yanayohitaji majadiliano ikiwamo vipengele kadhaa vilivyonyofolewa ambavyo visipoangaliwa kwa kina wakati huu, utakapotajwa muda wa kuipigia kura kila mtu atamlaumu mwenzake kwa kutokuwa makini kuyafahamu mambo hayo.

Alisema mojawapo ya maswali hayo mengi yasiyokuwa na majibu hadi sasa ni Tunu za Taifa ambazo hadi sasa zinazungumzwa tu, mwananchi akiuliza ni zipi haijulikani.

Alieleza kuwa vitu muhimu vinavyohusu maadili ambavyo wananchi waliyataka yameondolewa, ikiwamo miiko ya uongozi iliyokuwapo hata katika Azimio la Arusha, huku akishangazwa na kuondolewa kwa miiko hiyo ambayo itazalisha viongozi wasio waadilifu wanaofanya wanachokitaka badala ya kile wanachotaka wananchi waliowachagua.

Alilitaja jambo jingine ambalo bado ni kitendawili kinachohitaji majadiliano kuwa ni rais kuwa na madaraka makubwa na kushindwa kufanya kazi na mamlaka nyingine ikiwamo Polisi.

“Kuna wakati najiuliza maswali mengi na sidhani kama nitampata wa kunijibu, ndiyo maana nasisitiza majadiliano. Inakuwaje unaondoa hata kipengele cha kupima uwajibikaji wa wabunge. Wabunge wana nguvu kuliko waliowachagua ndiyo maana hawaonekani majimboni, lakini wananchi kama walivyotaka kuwa wasipomuona mbunge wao wamuondoe, hili nalo linahitaji majadiliano kuliangalia upya,” alisema Butiku.

Butiku ambaye alikuwa Katibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa miaka 21, alisema majadiliano ya kina pia yanahitajika katika suala la Muungano, badala ya kuishi kwa historia kwa kusema: “Mwalimu Nyerere alisema, Karume.”

“Muungano kwa Zanzibar bado unahitaji mazungumzo na majadiliano ili kuhakikisha tunapokwenda kuipigia kura Katiba Iliyopendekezwa kunakuwa hakuna maswali kama haya yaliyopo sasa.”

No comments: