Amfumania na Kumpasua Tumbo Mgoni Wake - LEKULE

Breaking

1 Apr 2015

Amfumania na Kumpasua Tumbo Mgoni Wake

POLISI mkoani Katavi inamshikilia mkazi wa kitongoji cha Ntumba, kijiji cha Mnyengele wilayani Mpanda, Deogratius Pastory (30) kwa kumjeruhi vibaya mkewe kwa kumkata mkono wake wa kushoto na kupasua tumbo la mpenzi wa mkewe kwa panga.

Mtu huyo aliwatendea unyama huo baada ya kuwafumania mkewe aitwae Tabu Nestory (20) na mpenzi wake wa kiume aitwaye Masaga Elias (28 wakifanya mapenzi katika jiko la nyumbani kwake kijijini humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha mkasa huo. Alisema tukio hilo ni la Machi 23, mwaka huu saa tano usiku katika kitongoji cha Ntumba katika kijiji cha Mnyengele.

Akielezea mkasa huo, Kidavashari alidai kuwa jioni ya siku hiyo ya tukio, mtuhumiwa alimuaga mkewe Tabu kuwa anakwenda kijiji ambacho kiko umbali mrefu kutoka kijijini hapo kwa ajili ya kuangalia shamba lao.

Inadaiwa mtuhumiwa huyo alitumia baiskeli yake katika safari yake hiyo. Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wakati mtuhumiwa huyo akiendelea na safari yake ghafla baiskeli yake aliyokuwa akiitumia katika safari yake hiyo iliharibika, wakati huo ilikuwa tayari imetimu saa tatu usiku .

“Kwa sababu alikuwa bado amebakiza mwendo mrefu kufika alikokuwa akienda aliamua kugeuza na kuanza kurejea nyumbani kwake, ambako alifika saa tano usiku …na alipofika kwake alimkuta mkewe na mpenzi wake wakifanya mapenzi katika jiko nyumbani kwake,” alieleza.

Inadaiwa kuwa kitendo hicho kilimkasirisha mtuhumiwa, ambaye alimwamuru mkewe na mgoni wake kuingia ndani, ambapo alimkamata mwanamume huyo na kumfunga kamba mikononi, kisha akachukua panga na kumchana tumbo chini ya kitovu hadi utumbo wake ‘ukamwagika’ nje .

Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, mtu huyo alitumia panga hilo alilotumia kuchana tumbo la mgoni wake, kukata mkono wa kushoto wa mke wake.

Kidavashari alidai kuwa majeruhi wote wawili, walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda mjini hapa, ambako wamewalazwa kwa matibabu, ambapo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi wa awali wa shauri lake utakapokamilika.

No comments: