Wizara yalia na kodi ya vinyago, yataka isitishwe - LEKULE

Breaking

23 Mar 2015

Wizara yalia na kodi ya vinyago, yataka isitishwe

Wizara ya Maliasili na Utalii, imetaka kusitishwa kwa kodi mpya ya vinyago ambayo imeanza kukusanywa hivi karibuni katika viwanja vya ndege kwa watalii wanaoondoka nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Adelhelm Meru alitoa wito huo jana alipokuwa akizungumza na wauzaji wa vinyago katika maduka ya Mount Meru Curios and Graft yaliyoteketea kwa moto hivi karibuni.
Meru alisema wanataka kodi hiyo isitishwe kwani ni kero kwa watalii na inaweza kuathiri biashara ya vinyago na ni kubwa ikilinganishwa na bei ya kinyago.
“Kuna mtalii mmoja ametulalamikia kuwa amenunua kinyago kwa Sh10,000, lakini anatakiwa kulipia kodi ya Sh30,000, tumeamua kulifuatilia tatizo hili ili lifanyiwe marekebisho au kodi hiyo iondolewe kabisa,”alisema Meru.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema Wizara kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), itatoa pole ya Sh100 milioni.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Ally Kondo alisema moto huo umeteketeza maduka 223 ya wafanyabiashara ya vinyago.
ambao vinyago vyao vyote vimeteketea na mali nyingine zikiwamo fedha katika maduka yao.
Kondo aliishukuru Serikali na Tanapa kwa msaada walioutoa kwao toka walipopatwa na janga hilo.

No comments: