MTIFUANO! Kwa hatua lilipofikia bifu zito kati ya mastaa mashosti wa zamani, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ na Kajala Masanja ‘Kay’, imebainika kwamba hakuna ambaye yupo tayari kumzika mwenzake, Amani limesheheni data.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini ambacho ni mtu wa karibu wa waigizaji hao, mtafaruku huo umechukua sura mpya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Madam kuanika ubaya aliotendewa na Kajala aliyewahi kumlipia faini ya shilingi milioni 13 na kumuepusha na kifungo cha miaka 7 jela, Machi 25, 2013.
“Hali ni tete, Madam ameibua bifu upya alipofunguka kupitia kipindi chake cha In My Shoes kinachorushwa na Runinga ya EATV, hapo ndipo ilipodhihirika kwamba wawili hao hawawezi kuzikana wala kusameheana.
TIMU KAJALA WAJA JUU
“Wafuasi wa Kajala hawakufurahishwa na maneno ya Wema ambayo walidai yalikuwa na lengo la kumvua nguo mwenzake, yale matumaini ya kusameheana hayapo tena, ni bifu hadi wanakwenda kaburini,” kilisema chanzo hicho.
WEMA ALIFUNGUKA NINI?
Kwenye kipindi hicho, mbali na mambo mengine, Wema alieleza kuwa Kajala hakuwahi kuwa rafiki yake lakini alijitolea kumlipia faini kumuepusha na kifungo kutokana na kuguswa na kuingiwa na moyo wa huruma kama msanii mwenzake.
“Sikuwahi kuwa na urafiki na Kajala, kilichonifanya niwe karibu naye ni mwanaye ambaye alikuwa akinipenda na kutaka kukutana na mimi...,” alisema Madam.
KIINI CHA UGOMVI WAO
Kupitia kipindi hicho, Wema pia alizungumzia kiini cha ugomvi wao ambapo alianika kinagaubaga kwamba alichukizwa na suala la Kajala kumsaliti kwa kutembea na mchumba wake aitwaye CK (yule kigogo aliyesumbua mjini kwa kutapanya fedha).“Kajala hana fadhila, huwezi amini mtu ambaye niliamua kujitolea kwa moyo wangu kumlipia Sh. milioni 13 huyohuyo aje kutembea na mchumba wangu, huku ni kukosa ubinadamu kulikopitiliza,” alisema Wema.
TIMU KAJALA WAMCHANA WEMA
Saa chache baada ya Wema kufunguka, wafuasi wa Kajala mitandaoni walimjia juu Wema kwa kumwambia kuwa hana busara na ndiyo maana ameamua kutamka maneno hayo waliyoyaita kuwa ‘ni ya aibu’.
“Wema hana busara, mtu mwenye busara zake hawezi kuzungumza hadharani mambo ya kuibiana mabwana, ni ujinga tu. Unazungumza ili iweje?” aliandika mfuasi wa Kajala mtandaoni.
KAJALA AFURA
Jitihada za kumpata Kajala aweze kuzungumzia mashambulizi hayo ya Wema hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa lakini shosti yake wa karibu alisema Kajala amechukizwa na maneno hayo ya Wema na kamwe hatakuja kukaa naye meza moja, achilia mbali kumzika.
“Kajala hakufurahishwa na maneno ya Wema, hali ni mbaya, amesema kamwe hawezi kukaa na Wema meza moja maana amekuwa mtu wa kumdhalilisha kila kukicha, alianza kwa kumwambia ana nuksi na sasa amemdhalilisha katika kipindi chake, kamwe hatamsamehe na hayuko tayari kumzika wala kuzikwa na Wema,” alisema shosti huyo.
WEMA AZIDI KUPIGILIA MSUMARI
Baada ya kipindi hicho kuruka hewani, baadaye mwanahabari wetu alimvutia waya Wema ambaye alizidi kusimamia msimamo wake kuwa kamwe hawezi kumsamehe Kajala kwa kuwa hakuonesha ubinadamu kwa kitendo cha kumkwapulia bwanaa’ke.
“Mengi nimeyasema kwenye kipindi changu, najuta kumfadhili Kajala hivyo hata akifa mimi pia siwezi kuhusika chochote maana hana fadhila na hata yeye asipokuja kwangu sawa tu,” alisema Madam.
MAMA ZAO WATAKIWA KUINGILIA KATI
Msanii mwenye taito kubwa Bongo Movies ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini, aliwaomba mama wa wawili hao kutumia busara za kiutu uzima kumaliza bifu hilo.
“Haya mambo ni ya wanawake, mama zao wanatakiwa kukutana na kulijadili ili waweze kulimaliza tatizo hili sugu,” alisema msanii huyo.
Jitihada za kuwatafuta wazazi wa wasanii hao ili kusikia wanazungumziaje bifu hilo, hazikuzaa matunda kwani simu ya mama Wema, Mariam Sepetu iliita bila kupokelewa huku mama Kajala akikosekana hewani.
TUJIKUMBUSHE
Kabla ya kuachiwa huru kwa faini, Kajala alihukumiwa kwenda jela miaka 7 au kulipa faini ya shilingi milioni 13 kwa kesi ya kuuza nyumba iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya mumewe, Faraji Agustino kukumbwa na tuhuma za kutakatisha fedha haramu.
No comments:
Post a Comment