Zaidi ya abiria Arobaini wa basi la kampuni ya Majinja linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam wamefariki dunia kwenye ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la Changarawe wilayani Mufindi huku abiria wengine 22 wakijeruhiwa baada ya basi hilo kugongana uso kwa uso na lori namba T.689 APJ mali ya kampuni ya Cipex ya Dar es Salaam lililokuwa limebeba kontena.
Mashuhuda wa jali hiyo iliyohusisha basi la majinja lenye namba za usajiri T438 CDE.lililokuwa linatokea mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam wameeleza kuwa lori hilo lililokuwa katika mwendo kasi ghafla liliingia kwenye mashimo makubwa ya barabarani na kupoteza mwelekeo hivyo kulifuata basi kwenye upande wake na kusababisha ajali hiyo.
Baadhi ya majeruhi walionusurika kwenye ajali hiyo iliyotokea majira ya saa tatu na dakika 40 wamesema awali walimuonya dereva wa basi hilo kupunguza mwendo lakini hakuwasikiliza na walipofika katika eneo la Changarawe kilometa chache kutoka mjini mafinga ndipo walipokumbana na dhahama hiyo.
ITV imeshuhudia miili ya watu 42 ikishushwa katika hospitali ya wilaya ya Mufundi huku majeruhi sita waliokuwa katika hali mbaya kati ya 22 wakihamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa ambapo mkuu wa mkoa wa Iringa Bibi Amina Masenza amezungumzia ajali hiyo na kusema kuwa ni moja ya tukio la ajali mbaya ya barabarani kuwahi kutokea katika mwaka huu.
Zoezi la uokoaji katika eneo la tukio lilihusisha vyombo karibu vyote yaani jeshi la zima moto na uokoaji, jeshi la kujenga taifa JKT kutoka kikosi cha 841 kj.huku uongozi wote wa mkoa wa Iringa ukikusanyika katika eneo la tukio ambapo baadhi ya wananchi walimzonga mkuu wa mkoa wa Iringa kulalamikia mashimo hayo ambayo yanaelezwa kuwepo kwa zaidi ya mwezi mmoja.
No comments:
Post a Comment