Wadau wapania kukwamisha Muswada wa Habari bungeni - LEKULE

Breaking

21 Mar 2015

Wadau wapania kukwamisha Muswada wa Habari bungeni

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga  akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitoa tamko la wadau wa habari kuhusu azma ya Serikali kupeleka muswada habari kwa utaratibu wa hati ya dharura. Katikati ni Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena na Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria.


Dar es Salaam. 
Jopo la wadau wa habari kutoka asasi, taasisi na vyombo vya habari nchini, limepanga kuwatumia wabunge kuwashawishi wakatae kupitisha muswada wa sheria ya habari uliopangwa kuwasilishwa bungeni kwa hati ya dharura.
Hatua hiyo inatokana na mipango ya Bunge hilo kuweka ratiba ya uwasilishaji wa miswada miwili ya habari kwa njia ya hati ya dharura, huku utata ukiibuka kutokana na usiri uliopo ndani ya miswada hiyo.
Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015. Jopo hilo chini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), limekubaliana kutua Dodoma kuanzia kesho ili kuendesha vikao vya ushawishi ndani na Kamati za Bunge, wabunge na uongozi wa Bunge ili kuhakikisha miswada hiyo haipitishwi kwa dharura.
Mbali na hatua hiyo, wadau hao wamekubaliana kusambaza nakala nne za tamko hilo katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Ofisi ya Mpango wa Ubia wa Uwazi Serikalini (OGP).
Jana, katika mkutano kati ya wadau hao na waandishi wa habari, walisema lengo la kutoa tamko hilo ni kulitaka Bunge kusitisha uwasilishaji wa miswada hiyo kwa utaratibu wa hati ya dharura ili kutoa fursa kwa wadau na wananchi kuiona miswada, kuisoma, kuichambua na kutoa maoni yao.
Walioshiriki kuandaa tamko hilo ni wadau kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Sahara Media Group, Policy Forum, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kampuni ya The Guardian, Mwananchi Communications Ltd, Free Media Ltd, Hali Halisi Publishers, Taasisi ya Twaweza, Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), Tanzania Citizens’ Information Bureau na Shirika la Sikika.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Bara (Jukata), Deus Kibamba alisema wadau wa habari wanaamini kuwa Serikali na Bunge hawatakuwa tayari kupokea lawama za wananchi kwa upitishaji wa miswada hiyo bila kufuata utaratibu wa kawaida.
“Hatutegemei kuona Serikali ikipuuza tamko hili ila inawezekana tukachukua hatua nyingine, endapo itashindika kwa njia hii ya tamko,” alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Sikika, Irinei Kiria alisema: “Hatuamini kama Serikali iko tayari kuona ikichonganishwa na wananchi kwa sababu ya miswada hiyo, wabunge wetu pia hatuamini kama watakubali kuona miswada hiyo ikipitishwa kwa hati ya dharura bila kushirikisha wadau.
“Miswada hiyo haiwahusu wanahabari pekee, bali hata wadau wengine, hata CCM hatuamini kama inaweza kukubaliana na upitishwaji wa miswada hiyo kwa usiri usiojulikana kwa wahusika.”
Akijibu swali kuhusu athari za kutaka kukwamisha miswada hiyo, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema ni heri kuzuia kuliko kuruhusu miswada iliyojaa usiri.
Alisema uvumilivu wa harakati za kuhitaji mabadiliko hayo zimeanza miaka minane iliyopita, hivyo ni vyema kuvumilia ili kuhakikisha miswada hiyo inazingatia masilahi kwa Watanzania na vyombo vya habari.
“Miswada hii ni mfano wa mtu aliyekuwa na njaa ya miaka mingi, halafu leo hii unamletea chakula kikiwa kimefichwa bila kujua unamwandalia chakula gani,” alisema Meena.
Tamko la wadau hao linaelekeza Serikali kupitia mkutano wa 19 wa Bunge kusoma miswada hii kwa mara ya kwanza kama hatua ya kuifanya iwe tayari kwa maoni ya wadau kwa miezi inayokuja.
Vyanzo vya ndani ya Bunge hilo vinaeleza miswada hiyo inatarajiwa kuwasilishwa, kusomwa, kujadiliwa kabla ya kupitishwa Machi 27 mwaka huu katika vikao hivyo vya Bunge.
Hofu ya wadau ilichagizwa zaidi na kauli ya Spika wa Bunge hilo, Anne Makinda ambayo alilinukuliwa akisema miswada hiyo haijamfikia mezani kwake.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ambaye alikuwa mwenyekiti wa tamko hilo, alisema wadau wanatamani kuona miswada hiyo ikipelekwa bungeni kwa utaratibu wa kawaida.

No comments: