Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Bunge lilipitisha sheria ya takwimu ya mwaka 2013, inayotoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya shilingi milioni 10 au vyote kwa pamoja kwa mwandishi au chombo cha habari kitakachotoa kimakosa takwimu za serikali wakati wakitekeleza wajibu wao
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
Sheria hiyo ya takwimu pia inazuia taasisi binafsi zilizokuwa zikikusanya na kutangaza takwimu za tafiti mbalimbali nchini kutofanya hivyo bila ya idhini ya mtakwimu mkuu wa serikali.
Sheria hizi zimetengenezwa ili kuwaziba midomo waandishi na watafiti binafsi wanaofanya kazi kwa masilahi ya nchi, ambao hukosoa taarifa potovu zinazotolewa na maofisa wa serikali katika idara mbalimbali.
Wakati serikali ikiwasilisha muswada huo ambao una ukakasi, sheria hiyo haisemi lolote juu ya ofisa wa serikali atakayetoa taarifa hizo potofu kwa mwandishi au chombo cha habari na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju (pichani) alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alijibu kirahisi kuwa mwandishi au chombo cha habari vitalazimika kwenda kujieleza polisi au mahakamani.
Kwa maana nyepesi ni kuwa ofisa wa serikali, anaruhusiwa kudanganya, lakini uongo huo ukichukuliwa na mwandishi na kuandikwa, imekula kwake!
Huu ni uonevu tunaofanyiwa waandishi kwa lengo la kutuziba midomo, serikali haitaki takwimu sahihi zifahamike kwa umma, kwa sababu kama wao serikali basi hawataki kutoa takwimu, kwa nini wasiziachie taasisi binafsi zenye uelewa wa kufanya tafiti?
Wanaogopa tafiti pinzani kwa sababu zitawaumbua uongo wao, ndiyo maana wanataka wafanya tafiti wote lazima kwanza wapate kibali cha mtakwimu mkuu, ambaye kabla ya kutoa kibali, bila shaka ataweka mbele masilahi ya serikali na kutoa maelekezo.
Hivi ni vitisho ambavyo ni aibu kwa taifa linalojiita la kidemokrasia kama letu. Afadhali basi vikwazo kama hivi vinavyowekwa kwa wanahabari, vingewekwa pia kwa wezi wengi walio serikalini ambao kila siku wanafanya usanii na kuiba mabilioni, lakini hatuoni wakipeleka sheria bungeni za kuwabana.
Ninachotaka kuwakumbusha watawala ni kwamba siku zote hakuna lenye mwanzo likakosa mwisho, watatufunga leo, lakini kesho na keshokutwa vizazi vyao vitalipia dhambi hii na sisi hatutaogopa kusema ukweli kwa sababu tunaitetea nchi ambayo wote tumeikuta!
No comments:
Post a Comment