Uganda kujadili Muswada wa Ndoa, Talaka - LEKULE

Breaking

5 Mar 2015

Uganda kujadili Muswada wa Ndoa, Talaka

Nini kinachafua ukombozi wa wanawake? Ni masilahi ya wanaume au wanawake wenyewe? Katika Uganda wanawake wa tabaka la kati kijamii, kisomi na kimapato, wameshtumiwa kutumia mbinu za umamluki kupigania haki za wanawake katika ndoa.
Mwandishi wa BBC, Alli Mutasa anaripoti kuwa wakereketwa wanawake wanakana hayo, na kusema wanatetea haki ya mwanamke iliyotunzwa na katiba ya mwaka 1995.
Ni sababu hii wanafurahia hatua ya kurejeshwa, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, Muswada wa Ndoa na Talaka, kujadiliwa katika bunge lenye wingi wa wanaume.
Mara ya mwanzo Muswada wa Ndoa na Talaka kufikishwa bungeni, ilikuwa miaka sita iliyopita. Mara ulizimwa ili kwayo wabunge, na kiinua mgongo cha shilingi milioni tano kila mmoja, wakashauriane na wana-jimbo wao. Muswada ukakwama.
Rani Ismail, mkurugenzi Msaidizi mahusiano ya vyombo vya habari, Ofisi ya Spika anabainisha.Anasema Spika wa bunge mwezi uliopita aliwakumbusha wabunge kuwa mwaka 2013 walipewa ruhusa na uwezeshaji warudi kwa wananchi ili kupata maoni kuhusu vifungu kadha vyenye utata katika muswada huo. Na maoni yaliyokusanywa yalitakiwa kuwasilishwa bungeni ili kujadiliwa ili kupitishwa au kukatiliwa.
Moja ya asasi za kiraia, ambazo zimepigania muswada huu urejeshwe kwa mjadala bungeni ni Uganda Women Network - UWONET. Mkurugenzi Mtendaji wa Uwonet ni Rita Aciro anabainisha kosa lililofanyika na kukwamisha muswada huo. "Kosa pekee tulilofanya kama nchi na ambalo wabunge walilifanya kuwa baya zaidi ni pale walipopewa fedha milioni tano kwenda kushauriana na wananchi, wakautoa muswada na kusema wanawake hawa wa Kampala wanataka kunyakua waume zenu....."anasema Rita.
Kwa hilo tu Bi Rita Aciro hajakosea. Kwani hizi ndio fikra kwa mfano utazisikia mitaani miongoni mwa wanaume kwa jumla, kuhusu Muswada wa Ndoa na Talaka wakiwa na maoni mbalimbali kuhusu muswaada huo, huku wengine wakiunga mkono na wengine kupinga.
Ama hoja ya Waislamu ilipatiwa muswada tanzu Muslim Personal Bill, au Muswada wa Nafsi Muislamu, ambao unatia maanani ndoa za Kislamu. Lakini muswada ambao spika anaurejesha bungeni pia una ubishani - kama mahari yasiwe shuruti ya ndoa na kuharamisha mtu kudai arejeshewe mahari wakiachana. Kuna hoja za kurithi wajane. Isitoshe, mwandishi wa siku nyingi kuhusu Muswada wa Ndoa na Talaka.
Kwa mujibu wa wafurukutwa, ikiwa muswada huo utajadiliwa na kupitishwa, utaimarisha sana haki za wanawake. Na makundi ya wanawake yamesubiri miongo minne kwa sheria bora ya ndoa. Lakini Machi mwaka juzi, Rais Museveni alishauri kwamba mchakato wa kuupitisha muswada huo unaharakishwa mno na kutoa hadhari kabla ya kuufanya sheria. Matumaini ya wakereketwa ni kwamba hadhari isije-geuka ulemavu wa kutenda.

No comments: