TAMBO ZA KABURU LEO TUTAIFUNGA YANGA KWA MRADI WA VIJANA - LEKULE

Breaking

8 Mar 2015

TAMBO ZA KABURU LEO TUTAIFUNGA YANGA KWA MRADI WA VIJANA



Kwanza ningependa kumpongeza makamu wa rais wa klabu ya Simba SC, Ndugu, Geofrey Nyange Kaburu, kwa namna alivyo muelewa amedirika kusema wazi kuwa anafurahishwa na namna mtandao huu unavyotoa habari zake, lakini kama mtu mwenye upeo mkubwa zaidi ameshahuri kubadilisha baadhi ya mambo katika uandishi wetu, kwa maana ya kupunguza matumizi ya ‘ lugha za moja kwa moja’ ambazo wakati mwingine hutafasiriwa kwa namna tofauti na wasomaji ambao ndiyo walengwa wetu wakuu.

Mtandao huu ulifanya mahojiano na makamu huyo wa rais wa mabingwa hao mara 19 wa kihistoria. Kaburu amezungumza mengi sana kuhusu klabu na mwenendo wa timu katika ligi kuu, lakini kwa kutazama mchezo wa Jumapili hii kati ya Simba na Yanga SC ningependa tushee wote sehemu tu ya mahojiano hayo hasa akizungumzia zaidi maandalizi ya Simba kuelekea katika mchezo huo….

lekule; Baada ya timu kuanza kwa kusuasua katika ligi kuu, Je, bado uongozi una imani na sera ya wachezaji vijana?

Kaburu; Imani yetu kwa wachezaji vijana ni kubwa na tunajua kwamba kwa uzoefu walionao kwa sasa ndiyo unaowafanya wacheze ‘ kwa mtindo wa homa ya vipindi’, mara nyingi wanacheza vizuri kipindi cha kwanza na kuharibu katika kipindi cha pili kutokana na kujisahau lakini ni jambo la kupita tu, na likiondoka hilo basi Simba itasimama.

Watazame vijana kama Said Ndemla, Ibrahimu Ajibu, William Lucian, Abdallah Seseme, Ramadhani Singano, Jonas Mkude, mtazame ‘ capten mtoto’ Hassan Isihaka ni wachezaji ambao hawajawahi kucheza ligi daraja la kwanza zaidi ya U20 na sasa wanacheza kikosi cha kwanza cha timu kubwa.

lekule; Unawaambia nini mashabiki wa Simba, timu ilipotoka, ilipo na matarajio msimu huu.

Kaburu; Cha kwanza niwaambie tu, kama uongozi bado una imani kubwa sana na timu tunafahamu ‘ tuna mapungufu ya matokeo’, lakini tuna imani kwamba hilo ni jambo la ‘ mpito’, ni jambo la muda tu kwa sababu tuna timu ambayo kwa bahati mbaya licha ya kuwa na vipaji vya hali ya juu, lakini bado hatuna uzoefu mkubwa wa ligi kwa sababu wachezaji wengi ni wapya, kwa maana kuna vijana kutoka timu ya pili waliopandishwa na wachezaji wapya ambao tumewasajili kutoka timu nyingine. Timu yoyote yenye wachezaji wapya inahitaji muda ili kutengeneza ‘ combination’. Tulijua tunaweza kupita katika wakati mgumu lakini imani yetu ni kubwa kwa timu hii.

Tunaamini kuwa timu hii itafanya vizuri, itatubeba msimu huu. Hadi sasa vijana wanacheza tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu. Waipe sapoti timu yao, ni vijana wetu hawa na lazima ‘ tujivunie’ kuwa nao. Hawa ni zao la klabu. Haya matokeo ya sasa ni suala la muda, lakini timu hii sit u kwa ajili ya kutubeba katika ligi kuu pekee, hapana, ni timu ya Afrika ambayo itaibeba nchi.

lekule; Tuzungumzie kuhusu mechi ya Jumapili hii dhidi ya ‘ watani wenu’ Yanga SC. Simba haijaifunga Yanga katika ligi kuu kwa msimu wa tatu sasa. Katika michezo mitano iliyopita Yanga wameshinda mara moja na mara nne mfululizo mmetoka sare. Nini tutarajie katika mchezo wa Jumapili hii?

Kaburu; Nakumbuka mara ya mwisho sisi ( Simba) kuishinda Yanga katika ligi ilikuwa ni Mei, 2012 tulipowafunga mabao 5-0. ‘ Tuliwakamata’ mara mbili katika ‘ Mtani Jembe’ ( 2013 na 2014). Kwa maana ya Simba, Hawa vijana hawana ‘ presha’ yoyote, wameandaliwa vizuri na si mara yao ya kwanza kucheza na Yanga. Ni sehemu kubwa ya vijana ambao msimu uliopita walikuwepo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao hadi ‘ Half Time’ tulikuwa nyuma kwa magoli 3-0.

Kipindi cha pili nakumbuka Mwalimu,’ King’ Abdallah Kibadeni aliwaingiza vijana watatu, William Lucian, Said Ndemla na Abdallah Seseme, wale waliingia na kwenda kubadilisha mchezo kisha timu ikasawazisha mabao yote na kutengeneza sare ya 3-3, hiyo ni ishara kwamba hii timu haiiogopi Yanga na hawa vijana wana uwezo mkubwa wa kuifunga Yanga.

La Pili, tayari wameshacheza na Yanga mara nne, na ukiangalia mara zote ambazo vijana hao wamecheza wameweza kufunga goli/magoli dhidi ya Yanga. Walikomboa goli tatu, wakashinda katika Mtani Jembe mara mbili na mara moja walitosa sare ya kufungana bao 1-1 ( mechi ya mwisho msimu uliopita) ni mara moja tu hawajafunga goli. Ni vijana ambao wana ifahamu Yanga vizuri sana, wameandaliwa vizuri kisaikolojia, upande wangu sina shaka na matokeo.

Hii ni sehemu ya kwanza ya mahojiano yangu na Makamu wa rais wa klabu ya Simba SC, Geofrey Nyange Kaburu, endelea kutembelea website hii utafahamu mengi mazuri kuhusu klabu ya Simba…

No comments: